Spread the love

KATIKA kuthibitisha uwajibikaji wao kwa jamii, Benki ya NMB nchini Tanzania imetoa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya zaidi ya Sh.8 milioni kwa shule ya msingi Bwitengi, Kijiji cha Bwitengi Kata ya Manchira wilaya ya Serengeti mkoani Mara. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

 

Aidha, Benki hiyo imetangaza neema kwa wanafunzi watakaofaulu kujiuanga Chuo Kikuu kuwafadhili ikiwemo kugharamia ada, malazi na vitendea kazi.

 

Akizungumza katika hafla fupi ya makabadhiano iliofanyika leo Jumamosi tarehe 9 Aprili 2022 katika shule ya msingi Bwitengi, Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Ziwa, Baraka Ladislaus amesema wataendelea kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Serengeti kwenye shughuli za maendeleo.

 

“Tulipopata maombi kutoka shule hii, sisi kama NMB tukaona ni vyema tukawasaidia na leo tumeweza kuwaletea mabati 118, mbao 400, Kilogramu 80 ya Misumari na waya za kushikia kenchi Kilogramu 16,” amesema Ladislaus.

 

Amesema benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita chini ya rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan.

 

“Benki yetu itaendelea kuinua sekta ya elimu na kwa mwaka huu, tutaanza ufadhili kwa wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na chuo kikuu lakini wakishindwa kwa sababu za kiuchumi,” amesema na kuongeza:

 

“Benki ya NMB itawagharamia ada malazi pamoja na kuwapa vitendea kazi kama kompyuta kuwasaidia masomoni.”

 

Aidha, Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Dk Vicent Mashinji ameipongeza NMB kwa kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi.

 

Amewaomba wakazi wa kijiji cha Bwitengi na Wanaserengeti kwa ujumla kuendelea kushirikiana vyema na benki hiyo kwani ndie mshirika wakweli kwa maendeleo ya wilaya ya Serengeti.

 

Naye Mkuu wa shule ya msingi Bwitengi, Melau Mollel amesema anaishukuru benki ya NMB kwa kuisaidia shule yao huku akiwaomba wasichokee kuisaidia shule yao kwani bado wana mahitaji mengi ikiwemo mashimo 32 ya vyoo ili kukidhi idadi kubwa ya wanafunzi waliyo nayo.

 

Amesema wanakabiliwa na uhaba wa nyumba 18 za walimu, ofisi tatu za walimu na madawati 266.

 

Mollel ameomba kusaidiwa upatikanaji wa photocopy mashine mbili pamoja na matanki manne ya maji.

 

Amesema bado kuna ushiriki mdogo sana wa wazazi katika kusimamia Elimu kwa watoto wao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *