August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NMB yapiga tafu milioni 20 kinara wa ubunifu UDSM

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa, Eliamani Sedoyeka akimpongeza Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk Aldo Kitalika baada ya kumkabidhi mfano wa Hundi ya Sh milioni 20 iliyotolewa na Benki ya NMB kwa mshindi wa jumla katika Wiki ya maonyesho ya 7 ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa pili kutoka kushoto ni Meneja Utafiti Masoko na Ubunifu wa Benki ya NMB, Prochest Kachenje

Spread the love

BENKI ya NMB nchini Tanzania, imekabidhi mfano wa hundi ya Sh.20   milioni kwa kinara wa ubunifu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ikiwa ni motisha kupitia mradi wa asili wa saruji unaotumia mabaki ya mimea na miamba. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Mradi huo wa UDSM ulitangazwa mradi bora wakati wa kilele cha Wiki ya Utafiti na Ubunifu jana Alhamisi iliyofanyika na kaulimbiu ‘Tafiti na Ubunifu kwa maendeleo ya kijamii nchini Tanzania’.

Hundi hiyo ilikabidhiwa na Meneja Utafiti Masoko na Ubunifu wa Benki ya NMB, Prochest Kachenje kwa Mpelelezi Mkuu wa Mradi huo, Dk Aldo Kitalika na kushuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Eliamani Sedoyeka.

Mradi huo unalenga kuzalisha saruji inayoweza kutumika mbadala ya saruji ya jadi na saruji hiyo mbadala inatengenezwa kutokana na mabaki ya mimea na mabaki kutoka migodini kwa maana ya mawe na udongo mbalimbali na saruji hiyo ikizalishwa inaweza kuuzwa kwa nusu bei ukilinganisha na bei ya sasa ya saruji.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya hundi hiyo, Kachenje alisema dhamira ya benki yake katika kuendeleza mipaka ya ubunifu wa kiteknolojia nchini Tanzania huku akiongeza benki hiyo imejizatiti kuendelea kuchangia ukuaji wa utafiti na ubunifu.

“Benki yetu ya NMB imedhamiria wendelea kuchangia kujenga uchumi bora kwa kutoa bidhaa za kibunifu za kifedha. Kwa miaka mingi, benki imewekeza katika mipango kadhaa na utafiti unaolenga kuboresha utoaji wa huduma za kifedha huku ikitoa majukwaa kwa wapenda teknolojia kufanya uvumbuzi na kuleta matokeo makubwa katika jamii,” alisema.

Kachenje alisema benki hiyo inajivunia kuwa mwanzilishi wa ufumbuzi wa masuala mbalimbali ya kifedha nchini Tanzania na tayari imetengeneza mfumo maalum unaojulikana kwa jina la NMB Sandbox Enviroment ambao unatoa fursa kwa wabunifu wa masuala ya kifedha hususani katika nyanja ya kidijitali kuja na suluhu yao ya kibunifu na kuongeza kuwa benki yake itashirikiana vyema na wavumbuzi watakaofaulu.

“Kwa kuwekeza katika utafiti na uvumbuzi, tumechangia kwa kiasi kikubwa hatua ambazo nchi imepiga kwenye sekta ya kifedha ya na ukuaji wa uchumi kwa ujumla. Tutaendelea kubuni na kusambaza bidhaa za kidijitali zinazoendana mahitaji ya wateja wetu na soko la Tanzania,” alisema.

Akipokea tuzo hiyo, Dk Aldo Kitalika aliishukuru benki hiyo kwa mchango wake na kusema fedha hizo zimepatikana wakati muafaka hulu akiongeza zitatumika kuufanya mradi huo kuwa wa kibiashara.

“Tunaishukuru sana Benki ya NMB kwa kutupiga tafu. Fedha hizi zimekuja kwa wakati muafaka kwani tayari tumesha agiza mashine kutoka Uturuki yenye thamani ya 47m/-. Lengo letu sasa ni kuuboresha mradi wetu na kuufanya uwe wa kiuchumi. Tunatarajia kuanza uzalishaji Julai mwaka huu,” alisema.

Awali, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Utafiti, Profesa, Bernadeta Killian alisema mwitikio wa shindano la ubunifu mwaka huu ulikuwa mkubwa sana na kuongeza kuwa taasisi hiyo ilitenga Sh.7.4 bilioni kuwezesha miradi mbalimbali ya utafiti inayofanywa na chuo hicho.

Naye Katibu Mkuu wa Wizari wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Eliamani Sedoyeka alisisitiza nafasi ya utafiti na ubunifu katika maendeleo ya nchi yoyote na kuongeza Serikali itaendelea kuwekeza katika utafiti ili kukuza uwezo unaohitajika na kusisitiza kuwa lazima nchi ibuni tekinolojia yake yenyewe.

“Serikali imetenga Sh.5.5 bilioni mwaka huu kusaidia utafiti na ubunifu. Kama nchi, tunahitaji kuja na teknolojia yetu wenyewe na kuitumia vyema ili kupiga hatua zaidi ,” alisema.

error: Content is protected !!