May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NMB yamwaga misaada Mara, RC Hapi “hatutaanzisha makambi ya wanafunzi”

Spread the love

 

MKUU wa Mkoa wa Mara (RC), Ally Hapi amesema, mkoa huo hauna mpango wa kuanzisha makambi ya wanafunzi kwa ajili ya kuwaandaa na mitihani ya taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mara … (endelea).

Amesema, jitihada zinafanywa na Serikali na wadau wa maendeleo za kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ikiwamo kuajiri walimu wengi wa masomo mbalimbali zinatosha kuwaanda wanafunzi na mitihani.

RC Hapi ametoa kauli hiyo, mwishoni mwa wiki wakati akipokea madawati, vifaa vya kuezekea kwa sekta ya elimu pamoja na vitanda maalum kwa sekta ya afya vyenye thamani zaidi ya Sh.68 milioni, vilivyotolewa na Benki ya NMB.

Msaada huo ulitolewa kwa Wilaya za Musoma na Rorya mkoani humu, utazinufaisha Shule 11 za Msingi na Sekondari pamoja na Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere maarufu Kwangwa.

Aidha, msaada huo unahusisha madawati, vifaa vya kuezekea kwa sekta ya elimu pamoja na vitanda maalum kwa sekta ya afya.

Mara baada ya kupokea msaada huo kutoka kwa Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori, RC Hapi aliishukuru benki hiyo na huku akizitaka mamlaka husika mkoani humo kuhakilisha zinaboresha taaluma ili kuongeza ufaulu.

Hapi alisema, mkoa huo hauna mpango wa kuwa na makambi kwaajili ya kuwaandaa wanafunzi walio kwenye madarasa ya mitihani.

“Ni ukweli kuwa, hivi sasa hakuna uhitaji wa makambi hayo kwani serikali imejitahidi kupambana na changamoto za elimu ikiwemo kuajiri walimu wengi siku za hivi karibuni,” alisema Hapi.

Alisema mkoa wa Mara umejiwekea malengo ili kuhakikisha taaluma inaboreshwa hasa ikizangatiwa kumekuwepo na matokeo yasiyoridhisha katika mitihani ya kitaifa kwa matokeo ya darsa la saba, kidato cha pili na cha nne.

Kauli ya Hapi kuhusu makambi, ameitoa kipindi ambapo kumekuwa na kutofautiana baina ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.

Wakati Profesa Ndalichako akipiga marufuku makambi kwa wanafunzi, RC Mtaka yeye alisisitiza lazima makambi yawepo kwani wanaozuia makambi hayo watoto wao wanasoma shule nzuri.

Kwa upande wake, Kimori alisema, benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu na afya kwa kutoa misaada na vifaa kutokana na faida iipatayo kila mwaka.

Kimori alisema, changamoto za sekta za elimu na afya nchini ni jambo la kipaumbele kwa benki licha ya serikali kujitahidi kwa kiwango kikubwa kuboresha sekta hizo lakini bado ipo haja ya jitihada hizo kuungwa mkono.

“Sisi kama wa wadau tunao wajibu wa kuunga mkono juhudi hizi za maendeleo kwa kusaidia jamii kwani jamii hii ndio imeifanya NMB kuwa benki kubwa kuliko yoyote hapa nchini,” alisema Kimori

Kimori alisema benki hiyo kwa kutambua changamoto zinazozikabili sekta za afya na elimu nchini, tayari imekwishatumia zaidi ya Sh. 1.88 bilioni kuanzia Januari hadi sasa, kuzisaidia sekta hizo.

Alisema, kwa mikoa ya kanda ya ziwa msaada huo umezinufaisha shule na vituo vya kutolea huduma za afya 129 huku mkoa wa Mara ukiwa umepokea jumla ya madawati 587, mabati 2,580 na vitanda 8 katika kipindi hicho.

Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara, Dk. Joachim Eyembe alisema, msaada huo utasaidia kuboresha huduma zitolewazo hospitalini hapo hasa ikizingatiwa mwezi ujao hospitali hiyo iliyoanza kutoa huduma mwezi Novemba mwa mwaka jana inapanua huduma zake kutoka huduma za mama na mtoto za sasa na kuongeza huduma za kibingwa.

error: Content is protected !!