August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NMB yakamilisha ujenzi wa zahanati iliyokwama miaka 10 Pwani

Spread the love

 

WAKAZI wa Kijiji cha Kiparang’anda Wilayani Mkuranga mkoa wa Pwani wameondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 16 kila siku kufuata huduma za afya nje ya eneo hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea).

Ni baada ya Benki ya NMB kutoa msaada wa mabati 210 kwa ajili ya ukamilishwaji ujenzi wa zahanati kijijini hapo.

Ujenzi wa zahanati hiyo ulianza miaka 10 iliyopita kwa nguvu za wanakijiji hao na kusimama kwa muda kutokana na kukosekana kwa fedha za kukamilisha jengo ili huduma ziweze kutolewa.

Awali wananchi walilazimika kutembea umbali huo kwenda kituo cha Afya Mkuranga au Hospitali ya Wilaya ambapo vifaa hivyo vilivyotolewa na NMB vitaondoa adha hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu.

 Zaituni Musa mmoja wa wananchi hao alisema msaada huo utawezesha zahanati yao sasa kukamilika na kuanza kutumika na kupunguza gharama walizokuwa wakitumia kusafiri mbali kufata huduma kwenye Hospitali ya Wilaya.

 “Tunashukuru benki hii kutukumbuka na sisi hapa kijijini  kwa sababu tunalazimika kutumia kati ya Sh7,000  na Sh11,000 kwa tripu moja ya bodaboda tukiumwa kwenda Hospitali ya Wilaya usiombe uwe na mgonjwa utachanganyikiwa,” alisema Zaituni.

Naye Edita Joel alisema kukamilika kwa zahanati hiyo italeta pia hamasa kwa wajawazito kuanza kliniki mapema.

Aidha alisema wazee na watoto kupata huduma stahiki kwa wakati  kwa sababu kituo kipo jirani na wao tofauti na sasa wanatembea zaidi ya kilomita 16  kwenda na kurudi.

Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard alisema hatua ya Benki ya NMB kutoa vifaa hivyo ni mwendelezo wa kurudisha kwenye jamii asilimia moja ya faida wanayoipata wao kama Benki.

 “Sisi leo tupo Mkuranga kwa ajili kutoa mabati 210 kwa ajili ya zahanati na kompyuta tano kwa ajili ya Shule ya Sekondari Kiparang’anda, niseme tu kuwa NMB tutaendelea kufanya hivi sababu tunaamini ni jukumu letu kama taasisi,” alisema Richard.

Katika Hatua nyingine Benki hiyo imetajwa kuwa kinara nchini katika matumizi sahihi ya Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), inakotumia fungu lake kusaidia harakati za kukuza elimu na kuongeza ufaulu mashuleni, sambamba na kutatua changamoto zinazoikumba Sekta ya Afya.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija, wakati akipokea misaada yenye thamani ya Sh.20 milioni  iliyotolewa na NMB, kwa ajili ya Shule za Sekondari Buguruni Motto, Shule ya Sekondari Misitu na Shule ya Msingi Umoja zilizoko wilayani Ilala.

Akizunguma katika hafla hiyo, DC Ludigija alisema, NMB imekuwa taasisi kinara wa uungaji mkono juhudi za Serikali katika kutatua changamoto na kuboresha miundombinu ya elimu na afya nchini, na kwamba shule, zahanati, vituo vya afya na hospitali zilizoko Ilala ni wanufaika namba moja wa CSR ya benki hiyo.

“Misaada hii ikawe chachu ya ufaulu kwa shule hizi na nichukue nafasi hii kusema kuwa NMB ni kinara wa matumizi sahihi ya sehemu ya pato lao wanalorejesha kwa jamii.”

“Haijawahi kuchoka kusaidia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kwa hakika benki hii ni mfano wa kuigwa katika Sekta ya Kibenki,” alisema.

Alibainisha wanaipongeza benki hiyo namna inavyoshirikiana na Serikali katika kuzitupia macho na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za elimu na afya, ambazo ni nyingi na haziwezi kumalizwa na Serikali pekee, bila nguvu ya wadau kama benki hiyo, huku akiyataka mashirika, makampuni na taasisi kuiga kwa NMB.

error: Content is protected !!