BENKI ya NMB imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono juhudi za kukuza maendeleo ya sekta ya utalii nchini ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuhakikisha sekta hiyo inachangia zaidi katika Pato la Taifa (GDP). Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Hayo yalisemwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa wakati wa kongamano la wadau wa sekta ya utalii lililofadhiliwa na benki hiyo jijini Arusha mwishoni mwa wiki na kuwakutanisha mawakala wa utalii kutoka nchini China waliopo katika ziara ya kuifahamu Tanzania na wadau wakuu kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii nchini,

Alisema benki yake itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wa utalii ili kuhakikisha kuwa nchi inafikia lengo lake la kufikia watalii milioni tano kwa mwaka.
“Kwa niaba ya menejimenti na bodi ya Benki ya NMB, nachukua fursa hii kuwahakikishia tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau wote wa sekta ya utalii na mnyororo wake wa thamani ili kukuza maendeleo ya sekta hii kwa uwezo wetu wote,” alisema Baragomwa.

Baragomwa alisema benki imejidhatiti kutoa huduma za kibenki zenye viwango vya juu na masuluhisho ili kukidhi matarajio ya watalii nchini Tanzania na kuongeza kuwa benki tayari imeanzisha bidhaa zinazotengenezwa mahususi kwaajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za kibenki ambazo ni rahisi na zakipekee si tu katika soko la Tanzania bali pia nje ya mipaka ya Tanzania.
“Kama mmoja wa wadau wa sekta ya utalii, NMB inaelewa wateja wanahitaji huduma za kifedha pamoja na masuluhisho yanayopatikana kirahisi. Kama benki, tutaendelea kutoa huduma zisizo na kifani ili kuhakikisha kuwa watalii wanapata kumbukumbu nzuri wakiwa nchini Tanzania,” alisema Baragomwa
Wakati wa hafla hiyo, Baragomwa aliwahakikishia mawakala wa utalii kutoka nchini China na vyombo vya habari vya China waliohudhuria kongamano hilo kuwa benki yake kwa makusudi ilianzisha dawati maalumu la Kichina la kushughulikia wateja kutoka China huku akiongeza kuwa banki hiyo ina uhusiano mkubwa na benki za China zikiwemo ICBC, Benki ya China na Benki ya Mawasiliano.
“Kwa makusudi, hivi karibuni tumeanzisha akaunti maalum ya Yuan ya China (CNY) ambapo wateja wetu wa China wanaweza kupokea CNY nchini China na kutuma CNY kutoka China kutoka ndani na nje.
Kama benki namba moja nchini Tanzania, tuna uwezo wa kutoa mikopo na dhamana na kwa mkopaji mmoja sasa tunatoa hadi dola milioni 135 kwa mkupuo moja,” alibainisha.
Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa alisema Tanzania imejipanga kuonyesha uzuri wake wa asili na urithi wake wa kitamaduni na kuongeza kuwa Serikali tayari imeweka mikakati ya kuingia katika masoko mapya.
Mcehgerwa alisema wizara yake kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Ubalozi wa China wanaandaa Programu ya “Tanzania Ready” ambayo pamoja na mambo mengine itasaidia kuongeza ukarimu na kuongeza idadi ya wageni kutoka Mashariki ya Mbali hasa China.
Alibainisha programu hiyo imeundwa makusudi ili kuhakikisha kwamba maeneo ya Tanzania yanajitayarisha kikamilifu kuwakaribisha watalii wa China na kuwapa uzoefu wa kukumbukwa na usiosahaulika.
“Tunaamini kuwa mpango huu utasaidia kuweka mazingira ya kukaribisha wezeshi kwa watalii wa China na kuwarahisishia kutalii na kujionea maajabu ya Tanzania,” alisema.
Alibainisha kampeni ya ‘Royal Tour’ ambayo iliongozwa na Rais Samia Suluhu Hasssan katika kuitangaza Tanzania kwa ukubwa zaidi tayari imepata mafanikio makubwa sio tu katika kuongeza idadi ya watalii kutoka nje bali pia uwekezaji kutoka nje ya nchi.
“Mawakala hawa wa watalii kutoka China waliyopo hapa wana utaalam na rasilimali ambazo zinaweza kutusaidia kuongeza ufanisi na kupiga hatua zaidi katika sekta yetu ya utalii. Tunawakaribisha kuchunguza fursa nyingi za uwekezaji zinazopatikana katika sekta ya utalii ya Tanzania,” alisema.
Alibainisha katika jitihada za kuwezesha uwekezaji huo, tayari Serikali imeainisha maeneo ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya hifadhi ndani na nje ya hifadhi za Taifa, mapori ya akiba na kuongeza kuwa Serikali imedhamiria kuweka mazingira rafiki ya biashara kwa wawekezaji watarajiwa nchini.
Aliongeza Serikali ya Awamu ya Sita tayari imetekeleza mageuzi ya kisera ambayo yanahakikisha urahisi wa kufanya biashara na kulinda maslahi ya wawekezaji.
“Tunatambua umuhimu wa kujenga ushirikiano imara na tumedhamiria kukuza utalii endelevu unaohakikisha uhifadhi wa maliasili za nchi kwa vizazi vijavyo,” aliongeza.
Hafla hiyo iliwakutanisha wadau wakuu wa sekta ya utalii kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Chama cha Waendeshaji watalii Tanzania (TATO), na Ubalozi wa China nchini China pamoja na wengine.
Leave a comment