November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

NMB, Selcom zaunganisha nguvu malipo kidijitali

Spread the love

 

BENKI ya NMB na Kampuni ya Selcom Tanzania wameanzisha ushirikiano wenye lengo la kusaidia kupunguza matumizi ya fedha taslimu nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)

Ushirikiano huo, wameutangaza leo Alhamisi, tarehe 18 Novemba 2021, jijini Dar es Salaam, mbele ya waandishi wa habari wakisema, kukuwa kwa teknolojia ya uchumi wa kidijitali ndiyo chanzo cha kuuanzisha.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Idara ya Biashara za Kadi wa NMB, Philbert Casmir amesema, benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kwenye mapinduzi ya malipo nchini.

Amesema ubia huo unawapa wateja wa NMB na Selcom pamoja na wamiliki wa simu za mkononi mawanda mapana zaidi ya sehemu za kufanyia malipo na kuchagua namna ya kulipia bidhaa na huduma mbalimbali.

Casmir amesema, wateja wa benki hiyo wanaweza kuvitumia vituo vya miamala vya Selcom kufanya manunuzi na wamiliki wa simu za mkononi kufanya malipo kupitia mfumo wa msimbo wa NMB (QR Codes) ambao pia utatumiwa na wateja wa Selcom.

Wakati NMB ina zaidi ya sehemu 53,000 kwenye mtandao wake wa mfumo wa malipo wa msimbo, Selcom ina karibu idadi kama hiyo ya vituo vya kufanyia miamala nchini kote.

“Ubia wa kimkakati na ubunifu kama huu ni muhimu katika kufikia ndoto ya kuifanya Tanzania kuwa jamii ambayo imeachana na matumizi ya fedha taslimu, na tutaendelea kujitolea kwa hali na mali kubuni suluhisho za malipo zinazoendana na hali halisi na mahitaji ya soko,” amesema Casmir

Aidha, amesema lengo mama la ushirikiano huo ni kuimarisha huduma jumuishi za kifedha nchini, kujenga mfumo mpana wa malipo, na kuongeza wigo wa suluhisho za malipo za kisasa.

Kufanikiwa kwa azma hii vile vile kunahitaji uwepo wa mazingira mazuri ya mfumo jumuishi wa kufanya malipo haraka, kitu ambacho Casmir amesema pia ni lengo mojawapo la ubia wa NMB na Selcom.

“Tunafurahi kushirikiana na Selcom ili kuimarisha zaidi mfumo jumuishi wa haraka wa kufanya malipo nchini Tanzania. Kupitia ushirikiano huu, tunawatengenezea wateja wetu na wa kampuni za simu fursa kubwa ya kufanya malipo kisasa zaidi,” amesema.

Hadi Juni 30, 2021, wamiliki wa simu za mkononi nchini walikuwa milioni 53.1 ambao kati yao takriban milioni 33.3 walikuwa wameuganishwa na huduma ya pesa mtandao.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Bidhaa wa Selcom, Gallus Runyeta aMEsema, mfumo wa msimbo (QR Code) unasaidia kurahisisha miamala katika biashara na teknolojia yake imekuwa nyeti kwenye kufanya malipo na kujenga uchumi wa kidijitali.

AMEsema QR Code inasaidia kuondoa haja ya mtu kutembea na fedha taslimu kwani huduma nyingi muhimu tayari zimeunganishwa na mfumo wake, mathalani maduka makubwa, sheli na hata migahawa.

Aidha, Runyeta aMEtabainisha ubia wa Selcom na NMB kwenye hili unasaidia kupanua zaidi mfumo jumuishi wa haraka wa kufanya malipo kidijitali na kuongeza fursa zinazopatikana ndani yake kutokana na wigo mpana wa sehemu na vituo vyao vya malipo.

error: Content is protected !!