Tuesday , 26 September 2023
Home Kitengo Biashara NMB, MCL wazindua Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake
Biashara

NMB, MCL wazindua Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake

Spread the love

BENKI ya NMB na Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), imezindua Jukwaa la Wanawake Mtandaoni ‘Rising Woman Network, lenye lengo la kuwawezesha, kuwaendeleza na kubadili taswira za wafanyabiashara, wajasiriamali na wataalam wanawake nchini. Anaripoti Mwananchi Wetu…(endelea).

Uzinduzi huo ambao ni zao la ‘The Citizen Rising Woman’ iliyokuwa ikiendeshwa na gazeti la The Citizen, umefanyika leo Jumatano jijini Dar es Salaam, ambako Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa NMB,  Ruth Zaipuna, walisaini hati za ushirikiano huo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kulia) akibadilishana nakala za makubaliano ya ushirikiano wa Jukwaa la “Rising Woman Online” na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Bakari Machumu (wapili kushoto), wakati wa uzinduzi wa Jukwaa hilo lenye lengo la kuwawezesha na kuwaendeleza wanawake wajasiriamali, wafanyabiashara na wafanyakazi. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Digitali wa kampuni ya Mwananchi, Happiness Watimanywa na kulia ni Mkuu wa Idara ya Bidhaa wa Benki ya NMB, Aloyse Maro.

 Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa MCL, NMB na Viongozi wanawake wa taasisi binafsi, Zaipuna amesema benki yake inaamini katika ushirikiano na ndio siri ya uwepo wa makubaliano mengi ya mashirikiano hususani ya kidigitali na taasisi mbalimbali nchini, kwani inaamini hiyo ndio njia kuu na ya haraka kuifikia jamii ambayo ndio wawezeshaji wao.

 Alibainisha ya kwamba NMB haitosita kuunga mkono jitihada zozote zinazolenga kurahisisha utendaji na uendeshaji wa shughuli za wadau wao, hasa wanapogundua kuwa kufanya hivyo kutawapa fursa ya kuyafikia makundi mengi zaidi ya kijamii, kwa haraka zaidi, kwa wepesi zaidi na kwa muda sahihi.

“Ndio maana Mwananchi Communications walipokuja kutuomba ushirikiano wa kuwawezesha wanawake wa Kitanzania, hatukusita tulikubali mara moja kwa sababu tuliona ni moja ya fursa muhimu za kuhudumia wanawake ambao ni kundi muhimu kwetu kama benki.

“Tutaendelea kusapoti mawazo Chanya yenye kuongeza thamani na kutoa masuluhisho ya changamoto mbalimbali kwa jamii inayotuzunguka. Tunaamini jukwaa hili litawezesha wanawake mbalimbali, wawe wafanyabiashara, wajasiriamali, wafanyakazi na viongozi wa kada zote.

“Ni jukwaa ambalo litawakutanisha pamoja, kupeana ushauri na kuwawezesha kufanya biashara. 

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kulia) akipeana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Bakari Machumu (wa pili kushoto), baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano wa Jukwaa la “Rising Woman Online” wakati wa uzinduzi wa Jukwaa hilo lenye lengo la kuwawezesha na kuwaendeleza wanawake wajasiriamali, wafanyabiashara na wafanyakazi. Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Digitali wa kampuni ya Mwananchi, Happiness Watimanywa na kulia ni Mkuu wa Idara ya Bidhaa wa Benki ya NMB, Aloyse Maro.

 Tayari tumeambiwa tunazindua jukwaa hili tukiwa na wanawake zaidi ya 70, sisi NMB tunaahidi kupitia Mwamvuli wa Jasiri, tutakuwa kule na fursa zetu zinazowahusu wanawake ambazo ni sehemu ya Jasiri, zote zitapatikana huko, ikiwemo mikopo na nafasi za kazi, tenda na nyinginezo,” alisema Zaipuna na kuwakaribisha wanawake.

 Kwa upande wake, Machumu amesema, baada ya miaka mitatu ya The Citizen Rising Woman ya kianalogi, wanajisikia fahari kubwa kupiga hatua na kuiweka kidigitali chini ya uwezeshaji wa NMB.

 “Tulikuwa na miaka mitatu ya mafanikio, ikihusisha hadithi zaidi ya 200 kutoka kwa wanawake mbalimbali nchini, na sasa tunauleta mfumo huu kidigitali, lengo likiwa kuwajengea ujuzi na maarifa muhimu wanawake kufanikiwa katika uongozi na usimamizi wa shughuli zao katika taasisi za umma na binafsi.

 “Kwa kufanya hivyo, tunaamini Rising Woman network inaenda kuharakisha ukuaji na ustawi wa kibiashara na kiuchumi, sambamba na utambuzi wa fursa zinazo wazunguka wanawake, sanjari na kuchochea ari ya uongozi kwa kundi hili kubwa kwa jamii.

 “Tunaishukuru NMB kwa kukubali kuungana nasi kuhuisha wazo hili ambalo huenda lingekwama. Huu ni ushirikiano wa kimkakati unaoifanya NMB kuwa mshirika pekee miongoni mwa taasisi za fedha nchini, wakiunagan nasi kupitia bidhaa yao ya NMB Mwanamke Jasiri,” alibainisha Machumu.

 Aliongeza ya kwamba, ushirikiano huo ambao unathibitisha dhamira ya pamoja ya MCL na NMB katika kukuza viongozi na uwezeshaji wanawake nchini, huku akizitaja sifa kuu za jukwaa hilo kuwa ni pamoja na ushirikiano na jamii, fursa za biashara na uwezeshaji kifedha.

Jukwaa hilo pia limebeba dhima ya kuelimisha, kutambua, kusherehekea na kukuza utamaduni wa uongozi kwa wanawake na uwezeshaji kifedha mtandaoni, yote hayo yakitarajiwa kufanyika chini ya Kaulimbiu isemayo; Wezesha Uhusiano Wake; Kukuza Uongozi na Kuimarisha Ushirikiano.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Biashara

NBC kuchochea ustawi biashara kati ya Tanzania na Afrika kusini.

Spread the loveBENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imesisitiza kuhusu dhamira yake...

Biashara

NMB yazindua hati fungani mpya ya trilioni 1

Spread the loveBENKI ya NMB imezindua rasmi programu mpya yenye hati fungani...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Serikali kununua mitambo 15 ya kuchoronga miamba

Spread the loveSerikali kupitia Wizara ya Madini imepanga kununua mitambo 15 ya...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Mtanzania aweka rekodi kimataifa kwa kiwanda cha kusafisha dhahabu

Spread the loveIMEELEZWA kuwa Kiwanda cha Kusafisha dhahabu cha Geita Gold Refinery...

error: Content is protected !!