January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nkurunziza aruka kigingi, arejea Burundi kwa shangwe

Wafuasi wa Nkurunziza wakimlaki rais wao aliporejea nchini mapema leo

Spread the love

SIKU mbili baada ya kutangazwa kuwepo mapinduzi dhidi ya Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, hatimaye jaribio hilo limezimwa na wanajeshi watiifu kwake na hivyo kiongozi huyo amefanikiwa kurejea nchini leo.

Kwa mujibu wa BBC, Rais Nkurunziza amewasili katika makao ya rais mjini Bujumbura kupitia msafara mkubwa wa magari ya wafuasi wa chama chake ambao walikuwa wamevaa mavazi ya bendera za chama hicho huku wakicheza dansi.

Mashahidi wameiambia BBC kwamba, Rais Nkurunziza ameanzia kwao huko eneo la Ngozi na amekuwa akiendeshwa katika gari la wazi upande wa juu huku raia wakimlaki kwa shangwe na vigelegele.

Shirika la habari la AFP, pia limeripoti kwamba, Rais Nkurunziza amerudi nyumbani kwao huko Ngozi yapata kilomita 140 kazikazini mwa mji mkuu wa Bujumbura, kulingana na duru ambazo hazikutaka kujulikana zilizo karibu na kiongozi huyo.

”Aliwasili katika eneo la Ngozi siku ya Alhamisi. Ni hapa ambapo anatarajiwa kulihutubia taifa kuhusu jaribio la mapinduzi lililofeli,”AFP lilimnukuu aliyetoa habari hizo.

Kiongozi wa kundi la kiraia linalopinga hatua ya Rais Nkurunziza kuwania muhula wa tatu, amewataka raia nchini humo kuendelea na maandamano kulingana na shirika la habari la AFP.

Vital Nshimiriman amesema kuwa licha ya kundi hilo kupinga jaribio hilo la mapinduzi, vile raia walivyowashangilia wanajeshi wa jaribio hilo kulionyesha kwamba kuna hamu kubwa ya mabadiliko.

Nukuu muhimu kutoka kwa Gervais Abayeho, msemaji wa Rais Nkurunziza, akizungumza na kipindi cha BBC cha Newsday.”Mapinduzi hushirikisha watu wengi. Kuna wanajeshi wa nyadhifa za chini ambao wamesalimu amri na ambao wanawasaidia maafisa wa poisi na uchunguzi wao,lakini ninaamini watu waliopanga mapinduzi hayo,wale viongozi hilo ni swala jingine ni lazima washtakiwe.

“Hakuna mgawanyiko katika jeshi.Iwapo unaweza kuwaangalia wale waliokuwa wakipanga kutekeleza mapinduzi ni wachache …kundi dogo la jeshi,”alisema.

Majenerali wawili waliotekeleza jaribio la mapinduzi hayo wamekamatwa. Hata hivyo, kiongozi wa mapinduzi hayo, Jenerali Godefroid Niyombare, ametoroka na anasakwa kulingana na msemaji wa rais.

Awali, Jenerali Niyombare aliambia AFP kwamba yeye na wafuasi wake watajisalimisha akiongezea kuwa ”natumai hawatatuua”.

Rais Nkurunziza amesema kuwa amerudi nchini Burundi na kwamba anatarajiwa kulihutubia taifa.

error: Content is protected !!