January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nkurunziza aapishwa ‘chapchap’

Spread the love

PIERRE Nkurunziza wa Burundi, ambaye ameanza kutengwa na jumuiya ya kimataifa, leo aliapishwa kushika upya wadhifa wa rais bila ya shamrashamra. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Sherehe ya kuapishwa kwake, ilihudhuriwa na wageni wachache mno kwa kuwa ilitarajiwa hasa ingefanyika Agosti 26, siku ambayo ndiyo ya ukomo wa muhula wake wa pili wa uongozi. 

Tayari kulikuwa shinikizo la kumtaka awe ameachia ngazi kabla ya siku hiyo ili kuruhusu kuanza kwa majadiliano ya kutatua mgogoro ulioibuka baada ya yeye kulazimisha aidhinishwe kugombea kwa muhula wa tatu kinyume na mkataba wa amani wa Arusha, nchini Tanzania.

Rais Nkurunziza alichaguliwa Juni 26 mwaka huu akitangazwa na Tume ya Uchaguzi kuwa amepata ushindi wa asilimia 67 katika uchaguzi uliosusiwa na vyama vya upinzani.

Taarifa iliyotolewa na ofisi yake imesema kwamba sherehe ya kuapishwa iliwahishwa na wageni waliokuwa wamealikwa kwa sherehe ambayo ingefanyika Agosti 26, wameombwa radhi.

Mchambuzi mmoja wa siasa za eneo la Maziwa Makuu, amesema haikuwa lazima kusubiri ifike Agosti 26 ambapo muhula wake wa pili wa uongozi ungemalizika, kwa sababu katiba inashurutisha tu kwamba sherehe isiwe zaidi ya siku hiyo.

Nkurunziza ameharakiza kuapishwa bila ya shamrashamra akijua kuwa Umoja wa Mataifa na Marekani zimekuwa zikihimiza aruhusu majadiliano ya kutafuta muafaka wa mgogoro ulioibuka tangu alipoanza kuhangaikia kuidhinishwa kugombea tena urais kwa muhula wa tatu, ikiwa ni ukiukaji wa mkataba wa amani uliosainiwa Arusha, nchini Tanzania mwaka 2002.

Alifanikiwa kushawishi chama chake cha CNDD-FDD kumpitisha kugombea, na akashinikiza Mahakama ya Katiba imuidhinishe, hatua zilizoleta mivutano kiasi cha baadhi ya majaji wa mahakama hiyo kukimbia nchi kwa kuhofia usalama wao.

Makumi ya watu wameuawa kutokana na maandamano na harakati za kumpinga kwa uamuzi wake huo. Wakati ameapishwa harakahara (chapchap) ametoa ahadi ya kurudisha utulivu ndani ya miezi miwili, huku akiwa ameshindwa ahadi ya kutoa taarifa ya uchunguzi wa mauaji ya maofisa waandamizi wawili wa usalama.

error: Content is protected !!