January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Njaa yapiga kambi Chamwino

Spread the love

WANAWAKE wa Kijiji cha Mazengo, kata ya Mvumi Makulu wilayani Chamwino, Dodoma wamekuwa wakipanda kwenye miti ya mizambarau ili kujipatia chakula kutokana na kukabiliwa na baa la njaa. Anaandika Dany Tibason, Chamwino … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Joel Miyomi amesema wanawake hao wamekuwa wakiparamia miti kwa lengo la kutafuta zambarau kwa ajili ya chakula.

“Akina mama hao wamekuwa wakiamka asubuhi na mapema kwenda kuparamia miti na kuchuma zambarau mbichi na wanapozipata huzikimbiza majumbani kwa ajili ya kuwapa watoto wao kama mlo wao wa siku,” amesema.

Amesema watoto hao hupatiwa zambarau hizo asubuhi kwa wale wanaoenda shuleni na wanaobaki nyumbani, kisha wao kuingia mashambani kutafuta vibarua vitakavyowawezesha kupata unga na fedha.

Hata hivyo pamoja na adha hiyo wakinamama hao wamesema kwa hivi sasa waume zao hawapo majumbani wamewakimbia kwenda mikoa ya nje kutafuta vibarua.

Mwenyekiti huyo hata hivyo aliitaka Serikali kupitia kitengo cha maafa kuwapatia chakula cha msaada ili kuondokana na baa hilo la njaa ambalo limewaathiri kwa kiasi kikubwa.

Naye Joyce Kojesa mkazi wa kijiji hicho amesema kutokana na baa hilo la njaa shughuli za kilimo zimesimama kwa hivi sasa hali itakayofanya mwaka huu kuwa tishio la kuwa na njaa zaidi.

“Shughuli za shamba haziendi kwa sababu muda mwingi sana tunautumia katika kutafuta matunda ya zambarau na vibarua ukizingatia kuwa waume zetu wamekwenda mikoa ya jirani kutafuta riziki,” amesema.

Kwa upande wake, Christopher Maduhu ambaye ni mkazi wa kijiji hicho aliitaka Serikali kuwapelekea mbegu zinazokomaa mapema ili kuendana na mvua hizi zinaendelea kunyesha.

error: Content is protected !!