May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nizar Khalfan kwenye rada za Yanga

Nizar Khalfan

Spread the love

 

WAKATI kikosi cha Mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Tanzania Bara kikiingia kambini hii leo kujiandaa na michezo ya mzunguko wa pili bila kuwa na kocha msaidizi, huku jina la Nizar Khalfan likitajwa kwenda kuchukua mikoba ya Juma Mwambusi aliyejiondoa kwenye timu hiyo. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).

Mwambusi ambaye alikuwa kocha msaidizi kwenye kikosi hiko aliandika barua ya kuachana na timu hiyo kutokana na kuanza kusumbuliwa na matatizo ya kiafya wakati timu ikiwa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar.

Mara baada ya kuondoka kocha huyo uongozi wa klabu hiyo upo kwenye mchakato wa kumpata mrithi wa Mwambusi ambaye atapendekezwa na kocha mkuu wa timu hiyo Cedric Kaze.

Taarifa kutoka kwenye chanzo cha ndani kwenye klabu hiyo zinaeleza kuwa Nizar ni moja ya makocha wanaojadiliwa kwa ajili ya kuchukua nafasi hiyo huku uongozi wa klabu hiyo ukikutana naye leo kwa ajili ya mazungumzo.

Nizar Khalfan wakati anaichezea Yanga

MwanaHALISI Online ilimtafuta mchezaji huyo wa zamani wa klabu za Mtibwa na Yanga kwa njia ya simu, juu ya kuthibitisha taarifa hizo na kusema kuwa hawezi kuliongelea jambo hilo kwa sasa.

“Kwa sasa siwezi kuliongelea jambo hilo wala kusema chochote naomba tuliache,” alisema Nizar.

Ikumbukwe wakati Mwenyekiti wa klabu ya Yanga anathibitisha kuondoka kwa Mwambusi alieleza kuwa watakaa na kocha mkuu Kaze nakuona kama atahitaji msaidizi kwa sasa au ataweza kuimudu kazi hiyo mwenyewe.

Kabla ya kuja kwa Kaze nchini alimpendekeza Mwambusi kuwa msaidizi wake katika benchi la ufundi mwanzoni wa msimu wa 2020/21 na kufanikiwa mpaka sasa kuifanya timu hiyo kuongoza kwenye msimamo wa Ligi wakiwa na pointi 44.

Pengine kumpa mikoba Nizar kunakuja kutokana ni kuwa mchezaji wa zamani wa timu hiyo pamoja na kucheza kwa mafanikio kwenye timu ya Taifa ya Tanzania, pamoja na kucheza nje ya nchi kwenye klabu ya Vancouver Whitecaps ya nchini Canada.

Kwa sasa Nizar anakinoa kikosi cha African Lyion kinachoshiriki Ligi daraja la kwanza Tanzania Bara.

error: Content is protected !!