June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nitakomesha unyanyasaji raia Karagwe – Rwazo

Spread the love

MGOMBEA ubunge katika jimbo la Karagwe kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) chini ya mwamvuli wa Ukawa, Princepius Rwazo ameamua kuvalia njuga tatizo la unyanyasaji wa sungusungu, polisi na mfumo wa mahakama katika jimbo lake la Karagwe. Anaandika Faki Sosi … (endelea).

Katika mahojiano yake na MwanaHALISI Online yaliyofanyika kwa njia ya simu juzi amesema atakomesha unyanyasaji huo unaofanywa na watendaji wa vijiji, kata, sungusungu, polisi na mfumo wa mahakama.

Amesema manyanyaso kwa wananchi yanawasababishia usumbufu kwa kuwa muda mwingi unapotea kufuatilia, muda ambao wangeutumia kushiriki kazi za uzalishaji mali, pia ni vitisho dhidi ya raia.

Rwazo ambaye alijiunga na Chadema 23 Novemba, 2012 amesema ameona umahiri, uzalendo, uwazi na upendo wa viongozi wa juu wa Chadema kwa Watanzania na hasahasa wanyonge.

Rwazo anaungwa mkono na UKAWA ambao wameafiki jimbo hilo kugombewa na Chadema katika uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba.

UKAWA inaundwa na vyama vinne vikiwemo Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).

Rwazo ana elimu ya Shahada ya kwanza ya Ualimu aliyoi pata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye amekuwa mwalimu wa sekondari ya Bugene, wilayani Karagwe amesema akichaguliwa kuwa mbunge, atasimamia kuinua uchumi wa watu Karagwe akitegemea zaidi sekta ya kilimo.

“Kilimo kinahitaji msukumo mpya ili kiwe mkombozi wa wakulima wa Karagwe. Wajitegemee kwa chakula na wapate soko la kuuza kwa ajili ya biashara,” alisema na kutilia mkazo matumizi ya trekta badala ya jembe la mkono ambalo tija yake imekuwa duni.

Amesema hali ya siasa wilayani ni nzuri kwa kuwa alianza muda mrefu kuwapatia wananchi elimu ya uraia kupitia mikutano ya hadhara na vipindi vya redio.

Rwazo ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Wilaya na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA) wilayani Karagwe, alizaliwa 4 Novemba, 1984 kijiji cha Rwambaiza, wilayani Karagwe.

Alihitimu elimu ya msingi mwaka 1999, akajiunga sekondari ya Mabira mwaka 2000, na kuhitimu 2003 sekondari ya Rwambaiza Karagwe. Alihitimu kidato cha tano mwaka 2005 sekondari ya Kibiti, mkoani Pwani na akahitimu kidato cha sita sekondari ya Ndanda mwaka 2006.

error: Content is protected !!