Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko NIT kushirikiana na NAS Tanzania
Habari Mchanganyiko

NIT kushirikiana na NAS Tanzania

Spread the love

 

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) nchini Tanzania, kimesaini mkataba wa ushirikiano na National Aviation Service (NAS) – Dar Airco Tanzania katika mipango chanya ambayo itawasaidia wanafunzi wa mafunzo ya anga na lojistiki katika usafirishaji kupata mafunzo kwa njia ya vitendo. Anaripoti Suleiman Msuya, Dar es Salaam … (endelea).

NAS iliyoanza shughuli zake nchini Kuwait mwaka 2003 na kuingia rasmi nchini Tanzania mwaka 2016, imebobea katika utoaji wa huduma mbalimbali kwenye zaidi ya viwanja 50 vya ndege duniani.

Mkataba wa makubaliano ulisainiwa mwishoni wa wiki iliyopita katika Kampasi ya chuo hicho Mabibo, jijini Dar es Salaam baina ya Mkuu wa Chuo, Profesa Zacharia Mganilwa na Meneja Mkuu wa NAS Dar Airco Tanzania, Miguel Serra mbele ya mjumbe wa bodi ya NAS Afrika, Prof. Costa Ricky Mahalu.

Akizungumza muda mfupi kabla ya hafla ya utiaji saini, Prof. Mahalu alisema: “Makubaliano haya yanakusudia kuanzisha ushirikiano kati ya NAS na NIT katika kusaidia wanafunzi wetu kupata mafunzo kwa vitendo.”

Prof. Mahalu aliongeza: “Programu ambazo zinatolewa NIT zinakwenda kukifanya chuo hiki kuwa taasisi bora kabisa katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na barani Afrika kwa ujumla.”

“Kwa hivyo, NAS Tanzania katika makubaliano haya itatoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya anga na lojistiki na usafirishaji kwa kuhakikisha kuwa wanapata mafunzo bora ambayo yatasaidia kufanya kazi nje ya nchi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo NIT, Profesa Mganilwa alisema: “Makubaliano haya yatatoa fursa kwa wanafunzi ambao wanasoma kozi za anga,lojistiki na usafirishaji kupata nafasi ya mafunzo kwa vitendo.

Prof. Mganilwa aliongeza: “Ushirikiano huu utaboresha na kuimarisha Shule kuu ya Usafiri wa Anga na Teknolojia ya NIT kutoa wataalamu zaidi ambao watasaidia nchi katika sekta ya anga.”

Makubaliano hayo yamekuja siku chache baada ya Taasisi hiyo kupata dola za Marekani milioni 21.25 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha mafunzo ya anga.

Alisema kupitia shule ya kuu ya Teknolojia ya Usafiri wa Anga iliyopo chuoni hapo wameanza kutoa mafunzo ya usafiri wa anga ya ubobezi ambapo mipango ni kuzalisha wataalamu wengi ambao watasaidia uendeshaji katika sekta ya anga nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mkuu wa NAS Dar Airco Tanzania Serra alisema: “NAS Tanzania inafurahi kuingia katika makubaliano haya na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji ili kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi.”

Meneja Mkuu aliongeza kuwa wanafunzi wa NIT watapata uzoefu wa kimataifa na wakati huo huo watapata nafasi za ajira katika ofisi zao zilizopo katika nchi zaidi ya 20 Duniani.

“Mbali na kupata nafasi ya mafunzo kwa vitendo, wanafunzi watapata nafasi ya kuajiriwa na ofisi zetu ambazo sasa ziko katika nchi 20 duniani na zaidi ya viwanja vya ndege 50 ulimwenguni,” alisema.

Serikali imeamua kuwekeza zaidi katika Chuo hicho ili kuboresha mafunzo ikiwa ni pamoja na kuweza kutoa wahitimu bora watakaoleta tija kwenye sekta ya usafirishaji ikiwemo sekta ndogo ya usafiri wa anga ambayo inakua kwa wastani wa asilimia 12 kwa mwaka.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB Pesa Akaunti yawavutia wakaguzi wa ndani Afrika

Spread the loveUbunifu wa bidhaa bora wa Benki ya NMB pamoja na...

error: Content is protected !!