August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NIT inavyohamasisha wanawake kusoma Sayansi

Spread the love

IKIWA imebaki siku moja Dunia kuadhimisha siku ya wanawake duniani kesho Jumanne 8 Machi 2022, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimetoa hamasa kwa wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi kwa kuwa wao wana mchango kwenye maendeleo ya jamii. Anaripoti Faki Sosi…(endelea).

Akizungumza katika semina ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike, leo Jumatatu, tarehe 7 Machi 2022 chuoni hapo Mabibo jijini Dar es Salaam, Profesa Zacharia Mganilwa, Mkuu wa chuo hicho amesema, wanawake wakiwa mstari wa mbele kwenye masomo ya sayansi jamii itapata maendeleo haraka.

Amesema mfumo wa maisha wa jamii wanawake wamekuwa na majukumu mengi yanayoanzia nyumbani, kazini mpaka kwenye jamii.

Ameutaja mfano wa kukosekana ugunduzi wa mashine ya kupika ugali kwa sababu wanasanyasi wengi ni wanaume.

Amesema chuo hicho wiki mbili zilizopita kimetoa timu maalum ya hamasa iliyokwenda mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) iliyokwenda kwenye shule za mikoa hiyo kuhamasisha wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi.

“Tunaye mwanafunz wa kike hapa aliyepata daraja la juu la kwanza la hesabu ambaye tukimpatia ajira hapa anapokwenda kuhamasisha wanafunzi wengine wanaona mfano nzuri, na watahamisika kuona kuwa mtaalamu wa Sayansi ni Mwanamke” amesema Profesa Mganilwa.

Amesema chuo hicho kina mifano mingi yenye kutoa hamasa kwa wanafunzi wa kike kusoma sayansi, mathalan mkuu wa idara ya kompyuta na Mkuu Idara ya Hesabati na Sayansi ya jamii ni wanawake.

Profesa Mganilwa ametoa wito kwa wanafunzi wa kike kuyachukulia masomo ya sayansi kuwa ni kama masomo mengine.

Amesema 50\50 isiishie kwenye siasa mpaka kwenye masomo na mambo mengine yahusiayo maendeleo ya Sayansi.

Kuhusu semina hiyo, amesema imeandaliwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanawake kukabiliana na changamoto wanazokumbana nazo kazini, nyumbani na katika jamii.

Dk. Zainab Mshani, Naibu Mkuu Fedha Mipango na Utawala wa chuo cha NIT amesema chuo hicho kimefanya semina kwa ajili ya wanawake kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

Amesema kwenye semina hiyo kutawasiliswa mada mbalimbali ikiwemo matatizo ya afya ya akili na masuala ya kiuchumi.

error: Content is protected !!