PROFESA Sospeter Muhongo, Mbunge wa Musoma Vijijini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameshauri serikali kujikita katika miradi ya nishati mchanganyiko, badala ya kutegemea umeme wa maji pekee. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Amesema, miradi ya umeme kwa kutumia maji, huchukua fedha nyingi lakini pia huchukua muda mrefu kurejesha faida.
Prof. Muhongo ametoa ushauri huo leo Ijumaa tarehe 9 Aprili 2021, wakati akichangia mjadala wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo waTaifa kwa miaka mitano (2021-2025), bungeni jijini Dodoma.
“Umeme tulionao ni mdogo, kila siku tunaimba hydropower (umeme wa maji), ukweli ni kwamba anayejua mambo ya umeme, hydro kukupatia faida uwe umewekeza hela nyingi. Unahitaji miaka mingi upate faida, ndio umeme wa maji uwe wa bei ya chini.”
“Sio kwamba tu leo nikimaliza bwawa na hapohapo bei ni ndogo, labda kama hutaki kurudisha hizo hela,” amesema Prof. Muhongo.

Waziri huyo wa zamani wa Nishati na Madini amesema, makadirio yanaonesha kuwa, Bara la Afrika siku za usoni litakabiliwa na ukame, hivyo Tanzania inatakiwa ijikite katika miradi ya nishati ya umeme mchanganyiko.
Ametaja nishati hizo kuwa ni gesi ya Nitro, mkaa, upepo na nishati ya jua.
“Na projection (makadirio) ni kwamba, Bara la Afrika kutakuwa na ukame. Tutakuwa tunapoteza kati ya DGP (Pato la Taifa) asilimia 1 hadi 2, je mabwawa yetu yakikumbwa na ukame nini kitatokea? Ndio maana tunahitaji energy mix (mchanganyiko wa nishati),” amesema Prof. Muhongo.
Kwa sasa Serikali ya Tanzania inatekeleza ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika Mto Rufiji (Mradi wa Kufua umeme wa Julius Nyerere), unaokadiriwa kutumia Sh. 6.5 Trilioni.
Mradi huo uliozinduliwa Julai 2019 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania, Hayati Dk. John Magufuli, unatarajiwa kukamilika Juni 2022.
Leave a comment