July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nisha: Tuwasaidie watoto wa mitaani

Spread the love

MSANII nguli wa vichekesho kwenye Tasnia ya Filamu nchini, Salma Jabu (Nisha) ameitaka jamii kutoa msaada kwa watoto waishio kwenye mazingira magumu badala ya kuendekeza starehe. Anaandika Regina Mkonde.

Amesema hayo jijini Dar es Salaam leo wakati akitambulishwa rasmi na Taasisi ya New Hope Family Group kuwa balozi wa kudumu wa watoto waishio katika mazingira magumu Tanzania.

“Wengi hupoteza fedha kwa matumizi yasiyo muhimu na starehe badala ya kusaidia watu wanaoishi kwenye mazingira magumu ambao wanahitaji msaada wao,” amesema Nisha na kuongeza;

“Naumia sana nionapo watoto wanaoishi kwenye mazingira haya wakikosa chakula ilhali wengine hula na kusaza.”

Nisha amesema kuwa watu wanaoishi kwenye mazingira magumu kama watasaidiwa na kuoneshwa upendo, itasaidia kuwaondolea mawazo mabaya ya kwenda kufanya mambo yanayohatarisha maisha yao na jamii kwa ujumla.

“Sasa ni wakati wa kuwafuta machozi, tuache kuwapa majina mabaya kama panyaroad, vibaka, watukutuku bali tuwe karibu nao na kuwaonesha njia inayofaa,”amesema.

Nisha ameitaka jamii kuepuka migogoro ya ndoa, ngono zembe, dhuluma na tamaa ya mali za yatima na wajane ambapo imekuwa sababu ya ongezeko

la watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Omary Kombe, Mwenyekiti wa Taasisi ya New Hope Family Group amewaalika wadau na wapenzi wote wa balozi Nisha kujitokeza siku ya kumvisha joho la ubalozi itakayotangazwa siku za usoni.

“Nihitimishe kwa kuwaalika wadau na wapenzi wa balozi wetu kipenzi cha watoto waishio katika mazingira magumu, wajitokeze siku ya kumvisha joho la ubalozi na kupewa tuzo ya msanii mwenye huruma na upendo itakayotangazwa siku za usoni,” amesema Kombe.

error: Content is protected !!