Saturday , 20 April 2024
Home Kitengo Habari Kimataifa Nini kitafuata baada ya Mahakama kuamua hatima matokeo uchaguzi Urais Kenya?
KimataifaTangulizi

Nini kitafuata baada ya Mahakama kuamua hatima matokeo uchaguzi Urais Kenya?

Spread the love

LEO Jumatatu tarehe 5 Septemba, 2022 Mahakama ya Juu ya Milimani ya Kenya inatarajiwa kutoa maamuzi yake kuhusu kesi ya urais iliyosikilizwa kuanzia wiki iliyopita.

Wiki iliyopita majaji saba wa Mahakama ya hiyo; CJ Martha Koome, DCJ Philomena Mwilu, Njoki Ndung’u, Smokin Wanjala, Isaac Lenaola na William Ouko waliwasikiliza mawakili kutoka upande wa  Raila Odinga, William Ruto na Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na wahusika wengine kisha kupumzika na kuandika hukumu watakayoitoa leo.

Majaji hao walitumia wikendi nzima kuandika uamuzi wao kuhusu masuala tisa yaliyowasilishwa mahakamani kwa muda wa siku tatu katika ombi la kupinga kuchaguliwa kwa Naibu Rais William Ruto kuwa Rais Mteule.

Tarehe 15 Agosti, 2022, siku sita baada ya Uchaguzi Mkuu, mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati alimtangaza Ruto kuwa Rais mteule baada ya kuzoa kura 7,176,141 (50.49%) dhidi ya milioni 6,942,930 za Raila (48.85%).

Baadae Raila alielekea katika mahakama ya juu Milimani na kupitia mawakili wake akadai kuwa kura hiyo ilibadilishwa ili kumpa ushindi mwembamba mpinzani wake William Ruto katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkali. Mawakili wa Ruto na tume ya uchaguzi hata hivyo wamekanusha madai hayo.

Kesi hiyo ilianza Jumanne kwa kikao maalumu baada ya walalamika na walalamikiwa kumaliza kuwasilisha hati zao za kiapo kufikia Jumatatu.

Baada ya kusikiliza pande zote zinazohusika katika kesi hiyo, mahakama ya milimani inatarajiwa kutoa uamuzi wa iwapo ushindi wa Ruto katika kinyang’anyiro cha tarehe 9 Agosti, 2022  ulikuwa halali au kulikuwa na udanganyifu.

NINI KITAFUATA?

Katika uamuzi ambao umepangwa kutolewa kuanzia saa sita mchana, Mahakama hiyo inaweza kuamua yafuatayo, Kwanza; Kuidhinisha matokeo ya urais au pili, kubatilisha matokeo ya urais.

Iwapo mahakama itaamua kuwa matokeo yaliyotangazwa tarehe 15 Agosti, 2022 ni ya halali na kushikilia ushindi wa Ruto, hiyo ina maana kwamba naibu rais huyo  anayemaliza muda wake, atajiandaa kuapishwa kuwa rais wa Kenya.

Kuapishwa kwa rais mteule kunatakiwa kufanyika siku saba baada ya mahakama kuidhinisha ushindi wake. Hii inamaanisha kuwa iwapo mahakama itaidhinisha ushindi wa Ruto basi ataapishwa tarehe 15 Septemba mwaka huu.

Kwa upande mwingine, iwapo mahakama itaamua kutupilia mbali matokeo hayo, basi hakutakuwa na kingine zaidi ya kurudi sanduku la kura kwa mara nyingine kumchagua rais mpya.

Kisheria, matokeo ya urais yanapobatilishwa, uchaguzi mwingine unapaswa kuandaliwa ndani ya siku 60 baada ya uamuzi kutolewa. Hii inamaanisha tume ya uchaguzi inapaswa kuandaa uchaguzi mwingine wa urais kabla ya tarehe 4 Novemba, 2022.

Mwaka wa 2017 mahakama hiyo iliweka historia kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kubatilisha uchaguzi wa rais. Makala haya yamendaliwa na Mwandishi Wetu kwa msaada wa mitandao ya kimataifa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!