June 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nimepata ajira mpya CHADEMA

Vurugu Bungeni

Moja kati ya vurugu zilizotokea Bungeni

Spread the love

NINAYOSEMA leo sikutumwa na mtu, chama au kiongozi yeyote,  ni yangu mwenyewe na ninayasema kwa wadhifa wangu mpya kama Msemaji Mkuu wa CHADEMA kwa mambo ya mitaani, barabarani, vijiweni na vikao visivyo rasmi.

Haya ninayoyasema yametokana na sisi wanachama, washabiki, wapenzi na wafuasi wa CHADEMA tulio mitaani, mabarabarani, katika vijiwe vyetu na katika vikao vyetu visivyo rasmi kukutana, tukazungumza na kukubaliana kama ifuatavyo:

Kwanza, kwamba yote yaliyotokea bungeni wiki iliyopita, kwa wabunge wa upinzani kutolewa nje haikuwa bahati mbaya wala kiburi na vurugu za wapinzani, bali ilipangwa na ndiyo maana akapangwa Naibu Spika (wewe soma mwenyekiti wa CCM wa Bunge), Job Ndugai, ili aongoze bunge siku ile.

Pili, kwamba maspika wetu wanachokifanya kwa kuendesha vikao vya bunge hovyohovyo ili kuwaudhi na kuwachukiza wapinzani, lengo lake wapinzani wasuse na kutoka nje na kuwaachia wabunge wa CCM wakipitisha uozo kama ilivyofanyika.

Tatu, kwamba kiti cha spika kinapohamishia kazi za mwenyekiti wa CCM bungeni, ni sawa na kiti hicho cha spika kutema mate kwenye pombe ili inyweke kwa wana CCM tu na wapinzani waone kinyaa kunywa mate ya chama hicho.

Yaani kuwaudhi, kuwabughudhi, kuwakejeli, kuwaitia polisi na makada wa CCM kuwatoa nje wapinzani ili wasuse na kutoka nje na kuwaacha wanaCCM wanaupitisha muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba kishabiki, tena peke yao, ni sawa na kutemea mate pombe ya watanzania wote.

Nne, kwamba wanachokifanya wapinzani wanaposusia vikao vya bunge na kutoka nje wakiwaacha makada wa CCM wakipitisha mambo yao wenyewe, ni sawa na mtu kumsusia mlevi pombe na kumwacha anainywa yote kwa starehe.

Kwamba wabunge wa upinzani wanapaswa kupima kati ya kumsusia mlevi pombe kwa kutoka nje na kumwacha anainywa kwa starehe, (namaanisha mlevi hapa ni wabunge wa CCM na viongozi wao), na kubaki ndani ya vikao vya bunge na kuvumilia upuuzi ili angalau wapate fursa ya kusema na kusikika wanapinga nini.

Tano, kwamba sisi wanaCHADEMA wa mitaani, mabarabarani, vijiweni na kwenye vikao vyetu visivyo rasmi tunafahamu na kuamini kwamba wenzetu katika CCM wameteua baadhi ya wanachama wao wasiokuwa na aibu wala soni ili watemee pombe yetu mate.

Kwamba wanaCCM wasiokuwa na aibu walioteuliwa kutemea pombe yetu mate ili tuisuse ni pamoja na Katibu wa Itikadi Nape Nnauye, Naibu katibu Mkuu Bara, Mwigulu Nchemba na maspika wetu wote (Anna Makinda, Job Ndugai,         Jenista Mhagama na Sylvester Mabumba.

Kwamba watemaji mate wengine kwenye pombe yetu, ambayo ni sheria ya mabadiliko ya katiba, ni pamoja na Stephen Wassira, William Lukuvi, mtaalamu wa kupiga tu, Mizengo Pinda, mwanasheria mkuu Fredrick Werema na bingwa wa kuongea na wafuga mbwa, Juma Nkamia.

Hawa makada wa CCM wanaonekana kuifanya vizuri kazi yao ya kuitemea pombe yetu mate ili sisi tusiokuwa wanaccm tususe kuinywa ili wao sasa waweze kuinywa kwa kupitisha katiba itakayowawezesha kuendeleza wizi, ubadhirifu wa mali ya umma, ufisadi na uhujumu wa mali za umma.

Jambo la sita tuliloling’amua sisi wanaCHADEMA tulio mitaani, mabarabarani, vijiweni na kwenye vikao visivyo rasmi ni kwamba naibu spika Ndugai si mjinga wala mpuuzi, bali anazo busara, hekima na maarifa; lakini aliamua kwa makusudi kufanya mambo ya kijinga yasiyokuwa ya busara, hekima na maarifa.

Sisi wa mitaani na vijiweni tunafahamu kwamba Ndugai alipaswa kutoa majibu kwa miongozo ya hoja za wapinzani na kumsikiliza Mwenyekiti Freeman Mbowe kabla ya kuendelea na mjadala, badala ya kusubiri hadi mwisho ambapo majibu ya miongozo hiyo hayangekuwa na maana tena.

Hivi majibu ya mwongozo, kwa mfano rahisi, yakiwa kwamba Zanzibar haikushirikishwa, yatasaidia nini kama mjadala wa hoja umekamilika na muswada kupitishwa? Tunajua Ndugai si mjinga kiasi cha kutofahamu hili.

Ndugai, Nape, Wassira, Lukuvi, Werema, Pinda, Makinda, Mabumba, Mhagama, Nchemba na bingwa wa kuongea na mwenye mbwa – Nkamia – wanafahamu kabisa kwamba sisi sote pamoja na wao, tuliwahi kuwa watoto na tulicheza michezo ya kitoto kama wao walivyofanya walipokuwa watoto.

WanaCCM hawa wanapaswa kufahamu kwamba hata sisi wa CHADEMA mitaani, mabarabarani, vijiweni na katika vikao vyetu visivyokuwa rasmi tuliwahi kucheza michezo ya baba na mama, kujificha na kutemea mate vyakula ili kuwazuia wenzetu wasituombe.

Nape, Werema, Nkamia, Nchemba, Wassira, Lukuvi, Makinda, Mabumba, Mhagama, Ndugai na wengineo wanaotumika kutuvuruga wanawakilisha mawazo na tabia ya uchoyo, ubinafsi, uzandiki na unafiki.

Ni mnafiki, mchoyo na mbinafsi pekee anayetemea mate kipande chake cha mhogo ili mdogo wake baba mmoja mama mmoja asimwombe! Lakini hawa wamekubali kutumiwa na CCM kutemea mate pombe, mhogo au mkate wetu ili sisi wapinzani tusiwaombe.

Lakini mimi nikiwa msemaji mkuu wa wana CHADEMA wa mitaani, mabarabarani, vijiweni na vikao visivyo rasmi, nawaambia ukweli kwamba, katiba itakayopatikana kwa mtindo huu haitadumu. Bali, itabadilishwa na serikali itakayofuata.

Siku serikali yetu ikiingia madarakani lazima itaviondoa vifungu vyote vya katiba vitakavyoonekana kukaa kindugaindugai na vingine vyote vitakavyokuwa vikisomeka kiweremawerema.

Serikali yetu itakapoingia madarakani, bila kujali kama ni mwaka 2015, 2020 au hata 2025, kazi yake ya kwanza itakuwa kufuta vifungu vyote vya katiba vitakavyoonekana kusomeka kinapenape au kinchembanchemba bila kuacha hata kimoja.

Ndiyo maana nawashauri wenzetu hawa kwamba waachane na kutuchafulia pombe yetu kwa kuitemea mate kwani watasababisha ama katiba ikataliwe kwenye kura ya maoni au ibadilishwe pale uongozi ukibadilika na kuingia CHADEMA.

Ni muhimu kwa Ndugai, Makinda na Werema wafahamu kwamba kwa sasa hivi tunaona kinyaa na kichefuchefu kunywa pombe iliyotemewa mate, lakini hapo njaa na kiu vitakapozidi tutainywa hivyo hivyo na tutapata kichefuchefu na kuwatapikia kwenye suti na magauni yao.

Sasa si bora wakaachana na tabia hiyo mbaya ili kuepuka kutapikiwa na watu wenye hasira na kichefuchefu? Sawa mlevi ukimsusia pombe atainywa yote, lakini matokeo yake mlevi huyo atalewa kupindukia! Msije kusema sikuwaambia.

error: Content is protected !!