Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Nimekomaa zaidi kisiasa katika miaka 9 ya ACT Wazalendo
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nimekomaa zaidi kisiasa katika miaka 9 ya ACT Wazalendo

Spread the love

 

LEO tarehe 5 Mei, ni ACT Dei. Ni siku ambayo Chama cha ACT Wazalendo kilipata usajili wa kudumu. Tunaadhimisha siku hii kwa sababu ndio siku ambayo tulikabidhiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa Cheti cha kututambua rasmi kama Chama cha siasa chenye haki za kufanya shughuli za kisiasa kwa mujibu wa Sheria za Tanzania.

Hata hivyo mchakato wa kuzaliwa kwa chama chetu ulianza siku nyingi kabla ya siku ya kupata cheti na uliendelea miaka kadhaa baada ya kupata cheti. Wazo la kuwa na chama kipya cha siasa lilianza kuzaliwa baada ya baadhi yetu kuanza kupata misukosuko katika vyama tulivyokuwamo.

Kwangu binafsi haikuwa rahisi, na kwa kweli ilinichukua muda sana, kuamua kushiriki kuundwa kwa chama kipya na kujiunga na chama hicho. Watu wengi walishiriki kwa njia moja ama nyengine kunipa nguvu ya kufanya maamuzi magumu sana katika maisha yangu ya siasa.

Hata hivyo watu watatu walikuwa na msukumo zaidi. Mmoja ni mbunge sasa, ambaye yeye pamoja na mwanamama mwanaharakati za haki za binaadam kupitia mitandao ya kijamii walinikalisha chini nyumbani kwangu na kunieleza kuwa hapakuwa na sababu ya kusitasita. Mwana mama huyu ndiye hata alipendekeza jina la Chama kwamba liwe, kwanza Alliance for Change Tanzania, lakini baadaye ilipoonekana kuwa litafanana na Asasi aliyokuwa anaongoza likaongezeka neno Transparency ikawa Alliance for Change and Transparency yaani ACT Tanzania.

Sisi watatu tulipoafiki jina lile, Prof Kitila Mkumbo na Bwana Samson Mwigamba wakawa na jukumu la kusimamia usajili. Kazi hii waliifanya kwa weledi mkubwa sana. Usajili ulipatikana kabla mimi sijawa mwanachama wa chama hiki. Nilikuwa bado mahakamani napigania uanachama wa chama nilichokuwamo.

Chini ya siku 30 tangu chama kipate usajili wa kudumu nilimpoteza mama yangu mzazi Hajjat Shida Salum Mohamed ambaye alikuwa mshirika wangu mkubwa kisiasa na mshauri. Ombwe hili la ushauri kwa kiasi kikubwa lilibebwa na mwanamama huyu mwanaharakati na kwa hakika alifanya kazi kubwa kipindi hiki kigumu sana kwangu.

Yeye nilikuwa naye katika Bunge la Katiba ambapo kuingia kwake kulitokana na maombi maalumu nilifanya kwa Rais wa wakati ule Jakaya Kikwete ili kupanua wigo wa wajumbe kutoka mitandaoni. Nilimwomba Rais nafasi mbili, akanipa moja.

Prof Kitila Mkumbo alikuwa ndiye kama Kiongozi wa chama kipya kwa ukweli kwani alitoa miongozo yote ya kiitikadi. Alikuwa Marcelino Dos Santos wetu kwa hakika.

Pamoja na hatua zote hizo kubwa tulizokuwa tunafanya bado nilikuwa nasita kujiunga na ACT Tanzania. Nilikuwa ninaamini kuwa kutatokea mtu mzima mmoja ambaye angeweza kutusuluhisha na uongozi wa chama changu ambacho nilifikiri kuwa nimewekeza sana kukijenga.

Zitto Kabwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo akibadilishana mawazo ya Bernard Membe, Waziri wa zamani Mambo ya Nje Tanzania

Afisa mmoja wa Serikali ambaye sasa ni Balozi akiwakilisha nchi yetu nje alikuwa muhimu sana kwangu wakati huu. Ni mtu ninayefahamiana naye muda mrefu na nina mahusiano naye ya kindugu. Nadhani alifuatwa na wenzangu kuambiwa kuwa miye bado nasita. Sitaki kuondoka chama nilichokuwamo. Akaniweka kitako katika moja ya mazungumzo ambayo yalibadili kabisa mtazamo wangu wa kisiasa na namna ninapaswa kufanya maamuzi.

Akanieleza kuhusu A Grain of Wheat, kwamba ili mbegu ya ngano iote lazima ioze kwanza. Akanikumbusha fasihi ya shule ya sekondari. Baada ya mazungumzo yale sikurudi nyuma. Hata hotuba yangu ya kujiuzulu ubunge ili nijiunge na chama kipya cha siasa niliita, ‘a grain of wheat’. Huyu Balozi na mwanamama mwanaharakati waliniandalia hotuba ile ambayo huwa nikiisoma nasisimka mwili. Juzi nimeona vijana wa ACT Wazalendo wameirudia kuweka hotuba ile kwenye mitandao ya kijamii.

Prof Kitila Mkumbo, Mwanamama mwanaharakati na Balozi kwa pamoja na watu wengine tofauti na hawa walinisaidia kufanya maamuzi ambayo leo imetimia miaka tisa nikiadhimisha. Tulitokaje ACT Tanzania kwenda ACT Wazalendo ilikuwa ni kazi ya kisayansi ilioshauriwa na binti wa Afrika Kusini ambaye ameishi Tanzania na akawa shabiki mkubwa wa maamuzi tuliyoyafanya.

Binti huyo sasa ni mwanamuziki mkubwa nchini Afrika ya Kusini. Alikuwa akiishi nchini Senegal na kufanya kazi katika Taasisi ambayo inafanya ushauri wa kisiasa. Tulifanya kazi na Taasisi ile na baada ya utafiti ambao ndugu Emanuel Mvula (Waziri Kivuli Fedha na Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo) alishiriki ilionekana kuwa Watanzania wanapenda sana uzalendo.

Tukashauriwa kuwa jina la chama liwe ACT Wazalendo badala ya Tanzania kwani utafiti ulionyesha kuwa linapotajwa neno uzalendo, wengi walipendelea. Mkutano Mkuu wa chama wa mwezi Machi mwaka 2015 ndio uliobadili rasmi jina la Chama na kuwa ACT Wazalendo. Mimi pia nilijiunga rasmi na Chama Mwezi huo wa Machi mwaka 2015.

Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini

Mchakato wa kuzaliwa chama chetu uliendelea baada ya kupata cheti kwa hatua hizo hapo juu zilizobadili jina la chama lakini pia hatua kubwa zaidi ambayo ilikipandisha chama ngazi ya juu kabisa ambayo tulipo sasa.

Mwezi Desemba mwaka 2018 Viongozi wa vyama vya siasa tulikutana katika hoteli ya Verde, Zanzibar kujadiliana hali ya demokrasia nchini Tanzania na hatua gani tuchukue. Wazo hili lilihusisha watu wengi sana lakini ndugu Ismail Jussa alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunafanya tafakuri hiyo ambayo ilihusisha pia watu wenye ushawishi kwenye jamii kama vile Ahmed “Eddy” Riyamy, Jenerali Ulimwengu na Wakili Fatma Karume.

Baada ya kikao kile tuliazimia kufanya kazi pamoja kuzuia mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa iliyokuwa inapelekwa bungeni mwaka 2019 mwezi januari. Kutokana na kazi ile na ushirika tuliyoujenga na waliokuwa viongozi wa chama cha CUF Imani kubwa ikajengeka na mnamo tarehe 19 Machi 2019 chama chetu kilizaliwa upya. Siku Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, alipojiunga na ACT Wazalendo, siasa za Tanzania zilibadilika kabisa na chama chetu kikawa miongoni mwa vyama vitatu vikubwa hapa nchini.

Mchakato wa Maalim Seif na wenzake kujiunga na ACT Wazalendo, maarufu kama SHUSHATANGA ni tukio muhimu sana, likihusisha kazi nzito iliyofanywa na timu mbili za kamati za majadiliano, chini ya Marehemu Mzee Aboubakar Khamis Bakari, pamoja na Wakili Omar Said Shaaban. Kazi ya timu hizi mbili ndizo zilizozaa tukio la Machi 19, 2019 (Shushatanga Dei).

Tangu wakati huo tumekuwa tofauti kabisa. Mimi binafsi nimekomaa zaidi kisiasa baada ya mwaka 2019 kuliko muongo mzima wa kufanya shughuli za kisasa.

Mei 5, 2024 sitakuwa Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo. Nitakuwa nimemaliza kipindi cha miaka miwili ya uongozi wangu kwa mujibu wa Katiba ambayo kwayo nilichaguliwa. Hivyo ninaandika maelezo haya kuhusu ACT Dei kwa mara mwisho nikiwa Kiongozi wa Chama, nikijivunia ukuaji wa chama hiki pamoja na ukuaji wangu. Ni jambo linalonipa furaha sana.

Nawatakia wanachama wote Heri ya Siku yetu. Tuisherehekee siku hii kwa kukumbuka wajibu wetu wa kuhakikisha tunasaidiana na Wazanzibari kuleta Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja, Yenye Mamlaka Kamili. Tuisherehekee siku hii kwa kukumbuka wajibu wetu wa kujenga Taifa (Tanzania) la Wote, yenye Maslahi ya Wote.

Kabwe Zitto Z. Ruyagwa
Kiongozi wa Chama – ACT Wazalendo
Dar es salaam
Mei 5, 2023

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwakyembe : Zanzibar waliongoza kutaka Serikali 2 za muungano

Spread the love  MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema mjadala wa...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

error: Content is protected !!