January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nigeria yahairisha Uchaguzi Mkuu

Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan

Spread the love

Nigeria imesitisha uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge mpaka Machi 28 mwaka huu. Uamuzi huu umefikiwa kutokana na sababu za kiusalama kwani mapambano yanayoendelea kati ya majeshi ya serikali na Boko Haram (BH) yatahatarisha usalama wa wapiga kura. 

Tume ya Uchaguzu ya Nigeria ilitangaza mabadiliko haya siku ya Jumamosi, na kuna uwezekano mkubwa mabadiliko haya yakasababissha mvutano na vyama vya upinzani.

Maafisa wa serikali ya Rais Goodluck Jonathan kwa wiki kadhaa sasa wamekuwa wakiitaka tume kubadilisha siku ya uchaguzi, huku wakisema tume haipo tayari kusimamia uchaguzi na ni tofauti na ahadi zake  kuwa uchaguzi huo utaandika historia ya demokrasia katika Afrika.

 “Walio wengi wamechukizwa na kukasirishwa” haya yalisemwa na Attahiru Jega  mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi wakati akiongea na vyombo vya habari siku ya jumamosi. “ Ninataka niwahakikishie Wanigeria  kuwa hamna anayetulazimisha kufanya uamuzi huu, uamuzi huu ni mzito”.

Tume imesema katika uchaguzi huu majimbo manne ya kaskazini mashariki hayatafanya uchaguzi kwani ni maeneo yaliyoathirika zaidi na maasi ya Boko Haram.

Kwa historia uchaguzi wa Nigeria unakuwa na machafuko, na tayari kuna watu wameshapoteza maisha yao katika harakati hizo za uchaguzi. Watu 800 waliuwawa mwaka 2011 huko kaskazini kwenye idadi kubwa ya waislamu wakati wa uchaguzi mkuu kati ya Jonathan na Muhammadu Buhari.

Uchaguzi huu utawapambanisha tena Jonatahn na Buhari. Wapambe wote wa wawili hawa tayari wameshaanza kutishia kuwa fujo zitatokea endapo mgombea wao hatashinda uchaguzi huo.

Chama cha Jonathan kimeshatoa maoni yake juu ya usitishaji huo kwa kuilaumu tume.

Muungano wa vyama unaomuunga mkono Buhari inasemekana wamefanya mkutano ili kujadili madhara ya mabadiliko haya “hiki ni kipingamizi kikubwa sana kwa demokrasia ya Nigeria” muungano  huo umewataka wanigeria kuwa watulivu na kujizuia na fujo.

Usitishaji huu umekuja kutokana na hofu ya operesheni kubwa inayofanywa na  majeshi ya Nigeria na Chad dhidi ya BH kwa kutumia wanajeshi wa ardhini na ndege za kivita. Operesheni hii iliyoanza siku 10 zilizopita imeweza kuwaaondoa baadhi ya wanamgambo hao kutoka kwenye vijiji mbalimbali.

Maofisa wa Umoja wa Afrika wamemaliza mkutano wa siku tatu huko Yaounde, Cameroon wakipanga mkakati jinsi ya kupeleka wanajeshi 8,750 huko Nigeria kutoka nchi jirani za za Benin, Cameroon, Niger na  Chad ili kuweza kuwakabili BH.

Mikakati hii imewafanya wanamgambo hao kujibu kwa kufanya mashambulizi  kwenye mji mmoja huko Cameroon na kwenye miji miwili huko Niger. Taarifa zinasema watu takribani 100 wameuwawa na 500 wamejeruhiwa huko Cameroon. Huko Niger wanamgambo 100 na mwananchi mmoja wameuwawa kwenye shambulizi lililofanyika siku ya Ijumaa. Idadi kadhaa ya wanajeshi wa serikali kutoka nchi zote pia waliuwawa.

Wanamgambo wa Boko wamefanya mashambulizi matatu katika kipindi cha wiki moja huko Maiduguri, mji unaoongoza kwa ukubwa huko kaskazini mwa Nigeria ambako maelfu ya watu waliukimbia siku ya Jumamosi huku wakijazana kwenye mabasi, malori na magari madogo wakiwa na mizigo yao kadiri walivyoweza kubeba.

Kujali kwa  swala hili kimataifa kumeongezeka, kwani kwa mwaka jana tu watu 10,000 wameuwawa , idadi hii ni kubwa ukifananisha na watu 2,000 waliopoteza maisha kwa kipindi cha miaka minne kabla ya mwaka jana, takwimu hizi ni kwa mujibu wa Halmashauri ya Mahusiano ya Kimataifa ya Marekani.

Marekani imeiomba Nigeria kuendelea na uchaguzi kama ilivyopangwa awali, haya yalisemwa na John Kerry alipotembelea Nigeria wiki mbili zilizopita. “moja ya njia mzuri kuendelea kupambana na BH ni kufanya uchaguzi halali na wenye amani katika muda muafaka” alisema.

Uchaguzi wa mwaka 2011 ulihairishwa pia na ukafanyika mwezi wa nne.

Uhairishani wa uchaguzi utaipa tume ya uchaguzi muda wa kusambaza karatasi za kupigia kuraa. Mpaka siku ya Ijumaa karatasi za kupigia kura milioni 45.8 tu zilishakuwa tayari kati ya milioni 68.8. Nigeria haina ofisi za posta zinazofanya kazi pamoja na kuwa nchi yenye uchumi mkubwa  katika Afrika.

Chama cha Rais Jonathan (PDP) kimekuwa kikishinda uchaguzi mkuu tangu mwisho wa utawala wa kijeshi ulioisha mwaka 1999. Hata hivyo kushindwa kwa Jeshi la Nigeria kuzima mashambulizi ya Boko Haram kwa miaka 5, ukuaji wa rushwa na uzorotaji wa uchumi wa Nigeria umemuweka Rais kwenye nafasi tete kwenye nchi hii inayozalisha mafuta kwa wingi katika Afrika na yenye watu wengi zaidi wanaofikia milioni 170.

Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika utawapambanisha Rais Jonathan na Muhammadu Buhari. Buhari mwenye umri wa miaka 73 kutoka chama cha CPC, ni mmoja wapo wa wagombea wenye nguvu atakayegombea kupitia muunganiko wa vyama unaoitwa ACN (Action Congress of Nigeria) umoja ulioundwa Februali 2013 ili kupambana na chama tawala cha PDP, unaoundwa na vyama vinne vya upinzani, hii ni mara ya kwanza kwa upinzani kuunda umoja.

Buhari ni Meja Generali mstaafu aliyepata kuwa Rais wa Nigeria kwa takribani miaka miwili baada ya kufanya mapinduzi ya kijeshi. Aliwahi pia kushiriki uchaguzi mkuu mwaka 2003, 2007 na mwaka 2011 alikuwa wa pili baada ya Jonathan kwa kupata kura 12,214,853 huku Jonathan akiongoza kwa kura 22,495,187.

Goodluck Ebele Azikiwe Jonathan (58) amekuwa Rais tangu Mei 2010 kufuatia  ya kifo cha Rais Umaru Yar’Adua. Mwaka 2011 aliingia tena kwenye nafasi hiyo baada ya uchaguzi mkuu. Rais Jonathan ana shahada ya sayansi ya Wanyama na Shahada ya Uzamili ya elimu ya viumbe wa majini na samaki, na inasemekana hakuweza ,kumaliza shahada ya Uzamivu. Kabla ya Siasa Jonathan alijikita kwenye ufundishaji, ukaguzi wa elimu na kama ofisa wa utunzaji wa mazingira.

Huu ni uchaguzi wa tano kwa Nigeria tangu imalize mapinduzi ya kijeshi hapo mwaka 1999, uchaguzi wa mwaka huu ulipaswa kufanyika Februari 14, 2015, na umeahirishwa kwa wiki sita mpaka Machi 28, 2015.

error: Content is protected !!