July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NIDA: Mradi wa kunufaisha wakubwa

Mkurugenzi wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maumi

Spread the love

DICKSON Mwaimu, mtendaji mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ameliibua upya sakata la mradi wa vitambulisho vya taifa. Anaandika Saed Kubenea(endelea).aifa (NIDA0, Dickson Maumi

Amenukuliwa akisema, uandikishaji mpya mikoani haufanyiki kutokana na uhaba wa fedha na rasilimali watu; NINDA imeshindwa kufanya usaili na utambuzi wa watu na ugawaji wa vitambulisho hivyo.

Mwaimu alikuwa akihutubia mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la NIDA.

Mradi wa vitambulisho vya taifa, unadaiwa kubuniwa mahususi na baadhi ya wanamtandao wa Rais Jakaya Kikwete, mara baada ya kiongozi wao kuingia madarakani. Lengo ni“…kuneemesha baadhi ya watu.”

Awali serikali ilisema mradi huu utagharimu sh. 152 bilioni. Baadaye ikasema hadi unakamilika utachukua kiasi cha sh. 250 bilioni.

Lakini sasa, kuna kila dalili kuwa utaweza kuchota, kutoka hazina ya taifa, zaidi ya sh. 500 bilioni. Sababu ni hizi.

Ukisoma nyaraka mbalimbali za serikali na kumbukumbu za Bunge – hansard – utabaini haraka jinsi viongozi wa serikali walivyobuni mradi huu gizani.

Utaona hata baadhi yao walivyotanguliza mbele maslahi binafsi. Kwa mfano, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha alituhumiwa mapema kuingilia mchakato wa zabuni.

Alidaiwa kukutana na wakuu wa kampuni ya Sagem Securite ya Uswisi, ambayo ilikuwa moja ya wazabuni.

Tuhuma zilikuwa kwamba Masha alikwenda kinyume cha sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi serikalini (PPRA) ya mwaka 2004 na kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 na Kanuni 101 (6).

Katika mchakato wa vitambulisho vya taifa wa mwaka 1998, Masha akiwa wakili kutoka kampuni ya IMMMA Advocates, aliwakilisha moja ya kampuni zilizoshiriki katika zabuni ya vitambulisho na kuingia katika mgogoro.

Mteja wa Masha aliishinda serikali. Lakini pamoja na madai hayo kuwekwa wazi, serikali ilimkingia kifua Masha.

Akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alitaka wabunge wavute subira ili mchakato huo ukamilike kwanza; ndipo anayetaka kuhoji afanye hivyo.

Jibu la Pinda lililenga moja kwa moja, kuficha ukweli. Lilithibitisha kuwa serikali imeingiza mabilioni ya shilingi katika mradi huu bila maandilizi.

Kukosekana kwa maandalizi, ndiko kulilenga kutoa mwanya kwa baadhi ya watendaji wa serikali na viongozi wake, kutafuta fedha kwa maslahi binafsi kwa kisingizio cha vitambulisho vya taifa.

Ndiyo sababu, baadhi ya makampuni yaliyopewa zabuni ya upembuzi yakinifu, hayakuwa na sifa ya kufanyakazi hiyo. Hayakuwa na uwezo kifedha, ujuzi wala utaalamu.

Waliojiita mameneja wa mradi, ndio sasa wamepewa kazi ya ushauri kwenye mradi. Baadhi yao ni watumishi wa serikali kutoka wizara za mambo ya nje na ofisi ya rais (Utumishi).

Huko walikotoka wamejilipa mabilioni ya shilingi kwa wanachoita, “Ushauri kwenye mradi.” Wanafahamika hata kwa majina na sasa, wamepewa ulaji mwingine kupitia NIDA. Miongoni mwa waliopewa ulaji, ni pamoja na Mwaimu mwenyewe.

Aidha, mradi wa vitambulisho vya taifa umebuniwa bila kufanyika kwanza uhakiki wa nani raia wa Jamhuri ya Muungano na yupi si raia. Serikali haiwezi kusema kazi hiyo inafanywa na NIDA.

Taasisi hii haina nyezo za kufanyakazi hii kubwa. Haina mamlaka. Kazi ya utambuzi wa nani ni raia na yupi si raia, yaweza kufanywa kwa uthabiti na wakala wa usajili wa serikali wa vizazi na vifo (RITA).

Lakini RITA pamoja na kupigiwa chapuo na wananchi wenye dhamira njema na fedha za umma, haikupewa kazi hii na serikali. Sababu zinaweza kuelezwa vema na wahusika wenyewe.

Badala yake, katika kufanikisha “mradi wake,” NIDA imeweka sharti dogo tu – anayetaka kitambulisho cha taifa – awasilishe kwa ofisa wa chombo hicho, kivuli cha cheti cha kuzaliwa au kivuli cha hati ya kiapo kinachothibitisha uraia wa mwombaji. Basi! Hiyo inatosha kumfanya akabidhiwe kitambulisho.

Mara baada ya kuwasilisha nyaraka hizo, taarifa za mwombaji huingiziwa kwenye daftari la utambuzi. Wenyewe wameita, “daftari la kielektroniki.” Kazi imekwisha. Mwombaji anasubiri kukabidhiwa kitambulisho.

Siyo kazi ya NIDA kufanya utafiti wa uhalali wa nyaraka zilizowasilishwa kwake. Wala siyo kazi ya NIDA kufanya utambuzi wa nani raia na yupi siyo raia. Nani anaishi “kimagumashi” na yupi anaishi kihalali. Nani yupo nchini na anafanyakazi kwa mujibu wa sheria na yupi ameingia mtaani kutengeneza nyaraka feki na kujipatia kazi.

Vilevile, siyo kazi ya NIDA kujua nani anatumia cheti cha marehemu na yupi anatumia cheti chake. Nani yuko hai; yuko wapi na anafanya nini; na nani amekufa na amezikwa lini na wapi.

Hizo siyo kazi zake. Kazi ya NIDA ni kugawa kitambulisho kwa yeyote, ili mradi amewasilisha nyaraka hizo kwake.

Kama NIDA haiwezi kufanya kazi ya utambuzi wa raia, nani atafanya kazi hiyo kabla ya kitambulisho kutolewa? Atafanya kwa gharama zipi? Nje ya bajeti ya sh. 250 bilioni au kutahitajika mabilioni mengine kufanya kazi hiyo? Haya ni maswali yanayohitaji majibu.

Kipi kilichoifanya serikali kushindwa kufanya uhakiki wa raia wake kabla ya kuanza kutoa vitambulisho? Si vema kwanza ingewatambua na kuwafahamu?

Ingejua huyu amezaliwa wapi. Baba yake ni nani. Mama yake ni nani. Babu yake ni nani. Je, anastahili kupewa kitambulisho au hastahili?

Katika mazingira ya sasa, kitambulisho kinaweza kutolewa hata kwa asiyehusika. Wala sharti la kuwasilisha kivuli cha cheti cha kuzaliwa au hati ya kiapo, haiondoi uwezekano wa wasiokuwa raia kupata kitambulisho.

Hilo likitokea na kwa hakika litatokea, mradi huu utakuwa uthibitisho wa utapeli uliokuwa unapigiwa kelele tangu mwanzo.

Wale waliokuwa wanaupigia debe wataishia kufunika nyuso zao kwa aibu. Tuombe Mungu tusifike huko.

Ilitarajiwa na kwa hakika, ndivyo ilivyoelezwa na hata na Rais Jakaya Kikwete – kabla na baada ya mradi kuanza – kuwa mradi wa vitambulisho vya taifa uende sambamba na uandikishaji wapigakura katika daftari la NEC.

Lengo ni kupunguza gharama kwa serikali na usumbufu kwa wananchi. Kwamba hatua hiyo itasaidia kuondoa usumbufu pale mtu mmoja kuitwa na watu walewale kujiandikisha mara nyingi ndani ya kipindi kifupi.

Lakini mradi huo umekwama. Katika muktadha huo, kulikuwa na umuhimu wa kutumia mabilioni yote haya ya shilingi, tena katika kipindi hiki kigumu cha anguko la uchumi wa taifa, kwa “kazi” hii inayoanza kuonekana kama kupeana ulaji?

Hivi hili lisingeweza kusubiri hata miaka 20 ijayo? Au ni kweli taifa linahitaji vitambulisho vya uraia kuliko nishati ya umeme? Linahitaji vitambulisho kuliko kuboreshwa kwa huduma kwenye hospitali zake za umma? Linahitaji vitambulisho kuliko kuziboresha shule zake za msingi, sekondari na vyuo vya elimu ya juu?

Taifa linahitaji vitambulisho kuliko kulipa madaktari, walimu na kuwapa mikopo wanafunzi wa elimu ya juu? Mbona taifa hili limekuwapo bila vitambulisho vya taifa kwa miaka 50 sasa?

Taifa linahitaji vitambulisho kabla ya kuboresha kilimo? Kitambulisho cha taifa, kina faida gani kwenye taifa la wajinga na ambalo watu wake, wanakufa njaa?

error: Content is protected !!