December 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Nichagueni nilete ajira Ubungo – Kubenea

Spread the love

MGOMBEA ubunge jimbo la Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Saed Kubenea ameahidi ajira za vijana wa jimbo iwapo atachaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba 25. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Kubenea, mwandishi wa habari na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hali Halisi Publishers Ltd inayochapisha gazeti la MwanaHALISI, alisema hayo mtaa wa Kanuni, Kata ya Mabibo, jimboni Ubungo, katika kampeni ya ubunge.

Amesema ajira 100,000 zitapatikana kupitia Mfuko wa Jimbo kwa lengo la kuwasaidia vijana kujitegemea.

“Ninataka kuwa mbunge kwa sababu ninajua kuna vijana wengi hawana ajira. Tunataka kutengeneza ajira laki moja ndani ya miaka mitano. Nina uhakika uwezo tunao,” amesema.

“Tutaweka mfumo rasmi wa ajira kupitia mfuko wa mbunge. Dhamira tunayo, uwezo tunao na wito wa Mwenyezi Mungu tunao… wapo vijana waliomaliza vyuo vikuu tutawatafutia ajira serikalini, kwenye mashirika ya umma na asasi za kiraia.

“Wapo vijana wamepata elimu ya kati nao watapata ajira… ambao hawakusoma kabisa, watakuwa na kazi hata ya kuzoa takataka katika mitaa yetu. Ajira zipo tatizo lililopo watu waliopo serikalini wamechoka kuwafikiria, wanajifikiria wenyewe,” amesema Kubenea.

Kubenea anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), amesema anafurahia ushirikiano wa vyama vinavyounda UKAWA – Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.

“Kupitia umoja huu, tutatengeneza taifa ambalo mtoto wa masikini anakuwa kiongozi kwa kuwa imeshindikana kufanyika ndani ya mfumo wa CCM,” amesema.

Amesema ameamua kugombea ubunge ili kupata fursa ya kuwanyoosha viongozi mafisadi kwa sababu kwa kubakia kazi ya uandishi wa habari lipo suala la sheria kandamizi zinamnyima uhuru wa kuandika maovu yanayofanywa na viongozi wa serikali.

Aliitaja Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, Sheria ya Magereza ya mwaka 1974, Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1968 na Sheria ya Polisi, “zote zinazuia haki ya wananchi kutoa na kupata taarifa kinyume na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kutoa  haki kwa kila raia kutoa na kupata habari.

“Serikali ilifungia gazeti langu la MwanaHALISI mwaka 2012. Nimeenda mahakamani nimeshinda kesi. Na Jumatatu litaingia mtaani. Kitu kinachosikitisha serikali italazimika kunilipa fidia ya zaidi ya Sh. 6 bilioni.”

“Fedha hizi ni za walipa kodi ambazo zingetumika kusomeshea watoto wetu na kusaidia huduma ya afya, lakini kwa uzembe na ubinafsi wa wateule wa Rais Kikwete, mahakama imesema nilipwe fidia ninayostahili,” amesema Kubenea.

Baada ya Waziri wa Habari, Dk. Fennela Mkangara kufungia gazeti hilo Julai 30, 2012, mahakama imemuona waziri huyo alikosea kisheria na kuamua serikali iachie gazeti lichapishwe bila ya kuingiliwa kwa namna yoyote ile na serikali.

error: Content is protected !!