September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ni zamu yetu, baada ya miaka 39, Stars yatinga AFCON 2019

Spread the love

BAADA ya miaka 39 na takribani miaka 27 ya kuitwa, “kichwa cha Mwandawazimu,” hatimaye timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), imefanikiwa kufuzu kucheza fainali za michuano ya Kombe la Mataifa Afrika. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, kutoka Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam …. (endelea).

Stars imefuzu michuano hiyo, baada ya kuifunga timu ya taifa ya Uganda (The Cranes), mabao 3 -0, katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam, jioni ya leo ya Jumapili, tarehe 24 Machi.

Mara ya mwisho kwa Stars kufuzu fainali za Afrika, wakati huo zikiitwa, “mashindano ya mataifa huru ya Afrika,” ilikuwa mwaka 1980. Fainali ya mashindano hayo, zilifanyika jijini Lagos, nchini Nigeria.

Stars ilifika Lagos, baada ya kuifunga timu ya taifa ya Zambia – maarufu kama Keneth Kaunda (KK 11) – bao 1-0 katika mchezo uliofanyika jijini Lusaka. Bao la Stars katika mchezo huo wa kufuzu kwenye fainali za Lagos, lilifungwa na mshambuali hatari wa kimataifa wa wakati huo, Peter Tino.

Tokea wakati huo, Stars ilikuwa haijawahi kukanyaga fainali za michuano hii.

Katika mchezo wa leo, mabao ya Stars yalifungwa na Simon Msuva, katika dakika ya 20 ambaye alimalizia kazi nzuri ya John Bocco; wakati dakika ya 51 ya mchezo, Erasto Nyoni aliongeza bao la pili kwa penati.

 Bao la tatu lililoihakikishia Stars kuelekea Misri, lilifungwa na Aggrey Morris kwa kichwa akiunganisha krosi ya Bocco.

Taifa Stars imefanikiwa kufuzu hatua hiyo baada ya kufikisha poindi 8 (nane), ikiwa katika nafasi ya pili katika Kundi L nyuma ya Uganda iliyokuwa kileleni ikiwa na pointi 13. Lesotho imemaliza hatua hii ya makundi kwa kushika nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita na Carpe Verde ikimaliza mkiani ikiwa na pointi 4.

error: Content is protected !!