July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ni vigumu kura ya maoni kufanyika Aprili 30

Katiba Inayopendekezwa

Spread the love

BADO siku 41 kufika 30 Aprili 2015, tarehe ambayo taifa lilitarajia kupiga kura ya maoni kuhusu katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba. Anaandika Pendo Omary…(endelea)

Dalili za mkwamo wa kufanyika kwa kura ya maoni ulijitokeza baada ya serikali kutoa kauli zinazotofautiana ndani ya wiki moja, kuhusu tarehe sahihi ya upigaji kura hiyo.

Mwishoni mwa mwaka jana, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (CAG), Jaji Fredrick Werema aliyeng’oka 15 Disemba, 2014 kwa kashfa ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kura ya maoni ingefanyika Machi 30 mwaka huu.

Werema alienda mbali na kusema kuwa, upigaji kura utatanguliwa na kampeni za makundi yanayoiunga mkono au kuikataa katiba iliyopendekezwa.

Kampeni hizo zingefanyika kwa siku 30, kuanzia mwanzoni mwa Machi mwaka huu.

Aidha, kauli ya Jaji Werema ilipingwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva na kufafanua kuwa kura ya maoni isingeweza kufanyika 30 Machi mwaka huu.

Sababu aliyoitaja Jaji Lubuva ni kwamba, kazi ya uandikishwaji wa daftari la wapiga kura haitakuwa imekamilika.

Utata ulizidi kuongezeka baada ya mkutano wake na waandishi wa habari, ambapo alisema, daftari la kudumu la wapiga kura lingekamilika 18 Aprili mwaka huu. Huku taratibu zikieleza kuwa, kura ya maoni itafanyika baada ya elimu kutolewa kwa wananchi kwa muda wa miezi mitatu hadi sita.

Jumatano, 22 Oktoba mwaka jana, ikajitokeza kauli nyingine kuhusu tarehe ya kupigwa kura ya maoni. Vyombo vya habari viliinukuu taarifa kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu-Dar es Salaam ikisema, Rais Kikwete alitangaza rasmi kwamba, tarehe ya kura ya maoni ni 30 Aprili mwaka huu.

Kauli hiyo ilitolewa na Rais wakati alipokutana na kuzungumza na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao katika Jamhuri ya Watu wa China. Mkutano huo ulifanyika ndani ya nyumba ya kufikia wageni ya serikali ya Diaoyutai mjini Beijing.

Wakati rais akitoa tangazo hilo, kwa mujibu wa sheria ya kura ya maoni, NEC ndiyo wanapaswa kutanga tarehe rasmi ya kura ya maoni.

Kujitokeza kwa kauli za tofauti baina ya viongozi wa serikali, hakika kulitafsiri namna ambavyo viongozi hao hawana ushirikiano katika kutoa maamuzi hasa yahusuyo mstakabali wa taifa kwa kuzingatia muktadha uliopo kwa wakati husika.

Mkwamo mwingine unahusu uadikishaji wa wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga kura. Uandikishwaji huo unaendeshwa kwa mfumo wa teknolojia mpya ya Biometric Voters Registration (BVR).

Mpaka sasa uandikishwaji huo unafanyika katika mkoa mmoja wa Njombe, ambako utamalizika Aprili 12 mwaka huu, kwa mujibu wa ratiba ya NEC.

Kwa hali hiyo, zitakuwa zimebakia siku 18 pekee kufikia tarehe iliyopangwa kufanyika kwa kura hiyo bila wananchi wa mikoa 29 iliyosalia kuwa wameandikishwa kwenye daftari hilo.

Pengine ni kutokana na kasoro hiyo, Jaji Lubuva kila mara amekuwa akisisitiza kwamba hakuna kura ya maoni bila wananchi wote wenye sifa kuandikishwa kwenye daftari la kudumu.

Zimebaki siku 41 kupigwa kura ya maoni; tarehe 9 Machi mwaka huu, NEC ilitangaza mashirika yasiyo ya Kiserikali ambayo yamepata fursa ya kutoa elimu baada ya kukidhi vigezo.

Kulingana na Sheria ya kura ya maoni, mashirika haya yanapaswa kutumia siku zisizopungua 60 kutoa elimu ya mpiga kura. Hapa napo kuna mkorogano wa kisheria unaonipa uhakika wa kusema bila kuuma meno kwamba kura ya maoni haipo.

Tumeshudia malalamiko kutoka asasi za kiraia, wananchi, vyombo vya habari, baadhi ya wanasisa hasa wa vyama vya upinzani, wasomi mbalimbali, wanaharakati, wadau wa maendeleo na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) wakitaka kura hiyo isogezwe mbele.

error: Content is protected !!