August 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Ni siku ya tafakari, si maasi’

Spread the love

WATANZANIA kote nchini wametakiwa kutotumia usiku wa leo (usiku wa mwaka mpya) kwa anasa, anaandika Dany Tibason.

Na kwamba, wanapaswa kutafakari wapi walikosea au walikopatia katika kutenda mambo mema ya kimaendeleo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mustafa Rajabu Shabani, Shehe wa Mkoa wa Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari mjini humo.

Shekh Shabani amesema walio na tabia ya kutumia siku ya mwaka mpya kukufuru Mungu kwa kufanya anasa na uchafu ambao kimsingi haumpendezi Mwenyezi Mungu.

Amesema siku ya mwaka mpya itumiwe na wananchi wote kukaa kwa utulivu na familia zao au katika nyumba za ibada kutafakari ni wapi walipatia au walikosea ili katika kipindi cha mwaka 2017 iwe ni sehemu ya kujirekebisha.

Akizungumzia suala la amani amewataka Watanzania kuhakikisha wanaondoa tofauti zao kwa wale ambao wametofautiana kwa kuombana msamaha.

“Ili kuweza kusonga mbele ni vyema kwa wale ambao wanadhani wametofautiana na kukoseana wakaombana msamaha na wale watakaoombwa msamaha ni vyema wakaukubali.

“Kwa wale ambao ni waumini wa Dini ya Kiislamu mafundisho yanasema mtu akimchukia mwenzake na kukaa siku tatu bila kusema naye na akifa, anaenda moja kwa moja motoni hivyo hakuna sababu ya kufikia huko,” amesema Shekh Rajabu.

Akizungumzia hali ya uchumi amesema ni wajibu kwa kila mtu kujipanga upya na kutumia vyema fursa aliyonayo katika kujiendeleza yeye pamoja na jamii kwa ujumla badala ya kutawaliwa na malalamiko ambayo hayawezi kuwa na faida.

Amesema mwaka 2017 uwe mwaka wa mabadiliko kwa kila mtu, kila sekta, kila taasisi na uwe mwaka wa kujitathimini ili kuweza kusonga mbele zaidi badala ya kurudi nyuma.

Na kamba, nguzo pekee nchini ni kutunza amani kwa kuwa na umoja, upendo, mshikamano pamoja na kujenga tabia ya kusameheana.

error: Content is protected !!