May 15, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Ni Prof. Lipumba ama Taslima CUF

Prof. Ibrahim Lipumba

Spread the love

NI Prof. Ibrahim Lipumba ama Twaha Taslima ndani ya Chama cha Wananchi (CUF). Jibu litapatikana Agosti mwaka huu, anaandika Regina Mkonde.

Agosti mwaka huu, chama hicho kimepanga kuitisha Mkutano Mkuu kujaza nafasi zilizoachwa wazi kwa sababu mbalimbali. Miongoni mwa nafasi hizo ni ya Mwenyekiti wa CUF-Taifa.

Katika nafasi hiyo, yapo makundi mawili; moja likimtaka aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho aliyejiuzuli kabla ya kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, Prof. Lipumba kwamba arejeshwe kutokana na chama kuyumba tangu ang’atuke.

Kundi la pili halijapata mwelekeo kwa kuwa, anayetarajiwa kuwa mshindani wa Prof. Lipumba, Taslim hajaoneshwa kuungwa mkono na kundi hilo.

Taslim amenukuliwa akiitaka nafasi hiyo. Kiongozi huo alikaimishwa nafasi hiyo muda mfupi baada ya Prof. Lipumba kujiuzuli kwa madai ya kuwepo kwa sintofahamu katika kumpata mgombea atakayewakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana. Prof. Lipumba hajaeleza chochote kuhusu kugombea nafasi hiyo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taratibu, baada ya Prof. Lipumba kuandika barua ya kujiuzulu na kuifikisha kwa katibu wa kikao Maalim Seif Sharif Hamad ili ifikishwe kwenye mkutano mkuu na uamuzi wa kukubali ama kukataa ufanyike, barua hiyo haijafikishwa sehemu husika jambo ambalo limesababisha kuwepo kwa mpasuko ndani ya CUF.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Shaweji Mketo, Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi CUF amesema kuwa, CUF imeanza harakati za kujipanga upya ili kufufua matumaini ya wananchi yaliyokatishwa na kile kilichoelezwa kuwa ni kutokana na utendaji mbovu wa serikali.

Amesema kuwa, chama hicho kimepanga kuitisha Mkutano Mkuu mwezi Agosti mwaka huu ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi.

“CUF kinapenda kuwahakikishia wanachama wake kwamba, viongozi tumejipanga upya ili kurudisha uhai wa chama na kwamba, nuru ya ukombozi wa taifa letu imekwishawaka kilichobaki ni kila mmoja kutimiza wajibu wake,” amesema.

Akizungumzia utawala wa Rais John Magufuli, Mketo amesema kuwa, tangu kuanza kwa utawala wake kumekuwepo na matukio mengi ya ukiukwaji wa haki za wananchi.

“Sakata la uhaba wa sukari hakuna asiyelijua sambamba na upandaji bei wake ambapo katika baadhi ya maeneo hata viongozi wenyewe wamekiri kuwa, be elekezi ya sukari haiwezi kutekelezeka kutokana na uhaba wa malighafi hiyo,” amesema na kuongeza;

“Nawapa pole Watanzania kwa madhila yanayoendelea kuwakuta kutokana na utawala wa Magufuli na CCM yake.”

Akizungumzia kauli ya Rais Magufuli wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu wanafunzi waliofukuzwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kuwa, baadhi yao ni vilaza, imekiuka haki za binadam.

“Kauli nyingine ni ile ya kuhamasisha wakuu wa mikoa na wilaya kwa hapa Dar es Salaam pamoja na Jeshi la Polisi kuhusu wanaovunja sheria za barabarani kwa kutumia barabara ya za mwendo kasi kwamba, wayakamate na kuyangoa matairi. Hii siyo haki,” amesema.

Aidha CUF imewataka wanachama wenye nia ya kugombea nafasi zilizowazi kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo.

“Wanachama wote wanakaribishwa kugombea ili tukijenge chama, zipo nafasi zaidi ya nne,” amesema.

error: Content is protected !!