July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ni mwisho wa enzi kwa Polepole?

Humphrey Polepole

Spread the love

 

KATIKA uteuzi wa vigogo mbalimbali wa Serikali ambao umefanywa na Rais Samia Suluhu Hassan tarehe 14 Machi, 2022, jina la Humprey Polepole ndiyo gumzo kwa kila anayezungumzia uteuzi huo.

Mjadala kuhusu Polepole ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi, umeibuka kutokana na mambo muhimu matatu, kwanza uteuzi wake umeacha fumbo kwa baadhi ya Watanzania kuhusu nafasi yake ya ubunge, kwamba ametenguliwa au lah!

Pili ni namna alivyokuwa ameibuka kuwa kinara wa ukosoaji wa Serikali ya Awamu ya Sita tofauti na wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Tatu, kwa kuwa Polepole ni moja ya wabunge na wanasiasa ambao wametamka hadharani kuwa hawatochanja chanjo ya COVID -19 ilihali nchi anayoelekea imeweka vigezo kwamba ni lazima kuchanja na kupimwa maambukizi ya virusi hivyo.

SAFARI YAKE KISIASA

Hayo yote yamejiri baada ya Polepole kupaishwa vilivyo kisiasa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli aliyeanza kwa kumteua kuwa mkuu wa wilaya ya Musoma kisha Ubungo, baadaye akamteua kuwa Katibu wa NEC- Itikadi na Uenezi CCM na mwishowe mbunge.

Licha ya kwamba Rais wa Awamu ya Nne Dk. Jakaya Kikwete ndiye aliyemuibua kwenye uwanja wa siasa kwa kumteua kuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba mwaka 2014 maarufu kama ‘Tume ya Jaji Warioba’, yamkini Hayati Rais Magufuli alimuongezea mwendo kisiasa.

Polepole aliyeanza safari ya uanaharakati katika taasisi moja ya utetezi wa masuala ya vijana nchini, baada ya Rais Magufuli kufariki tarehe 19 Machi, 2021 alitafsiriwa kuwa amegeuka mwiba kwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongoza na Rais Samia Suluhu.

Humphrey Polepole, Balozi wa Tanzania nchini Malawi

Misimamo yake aliyoionesha nyakati za uanaharakati katika masuala ya vijana, Tume ya Jaji Warioba, ulirejea na kuibua minong’ono mingi kuhusu hatima yake ndani ya CCM.

Kwanza Polepole alipinga hadharani suala la chanjo za COVID-19 na kushikilia msimamo wa Rais Magufuli ambaye hakunuia kuingiza chanjo hizo nchini.

Polepole aliandika hivi kupitia ukurasa wake wa Facebook “Kuchanja ni hiari, lakini siyo kila kitu, mimi nitaimarisha kinga ya mwili wangu na chanjo kwangu hapana. Sasa baadhi yenu msihangaike na mimi, hangaikeni na rai yangu hapo juu.”

Msimamo huo ulisababisha mijadala kiasi cha kuwaibua makada wa CCM akiwamo Katibu mkuu wa UVCCM, Kenani Kihongosi ambaye alimkemea.

Pili, Polepole alitafsiriwa kupinga baadhi ya taratibu za kuwahamisha wamachinga kutoka kando ya barabara na maeneo yasiyorafiki.

“Suala la machinga wanasema nimesema uongo, tena kwenye hilo nitasema na mengine ambayo sikutaka kusema, nina ushahidi, nimepeleka watafiti wilaya zote za Dar es Salaam, mtu amehamishwa na kupelekwa kwenye karo la choo, hivi Mhe. Rais aliwatuma hivyo?” alisema Polepole.

Wakati hayo yakiendelea kupoa, Polepole aliibuka na kipindi cha ‘Shule ya Uongozi’ ambacho kilionekana kukosoa vilivyo baadhi ya sera za Serikali ya Awamu ya Sitta.

Humphrey Polepole, akiwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM

Hali hiyo ilisababishwa kipindi hicho ‘kupigwa nyundo’ na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwamba kimeanzishwa na kuendeshwa kinyume na taratibu.

Harakati zake zilizokuwa na kauli mbiu ya ‘Kataa wahuni’ ziliendelea kiasi cha kuhojiwa na CCM kuhusu mwenendo wake kisiasa.

MWISHO WA ENZI?

Aidha, baada kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi, baadhi ya wanazuoni wameutafsiri uteuzi wake kuwa sasa mwisho wake kisiasa umeiva.

Hayo yanajiri kutokana na historia kuonesha kuwa kuna utamaduni wa kuwapa ubalozi baadhi ya vigogo na wanasiasa ‘wasumbufu’ ili kuwafunga mdomo.

Mathalani Balozi John Nchimbi ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 alitafsirika kuwa tishio kwenye uongozi wa Rais Magufuli baada ya kuonesha nia ya kuendeleza harakati za urais alizozianza mwaka 2015.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kiraia ya kufuatilia Utendaji wa Bunge (CPW), Dk. Marcossy Albanie ambaye anasema ni dhahiri uteuzi huo wa Polepole ni wa kimkakati.

Aidha, Dk. Albanie anasema nafasi ya Ubalozi imeonekana kuwa nafasi ya kumuondoa kigogo anayeonekana kuwa mwiba kwa Serikali.

“Kwa mfano Polepole, ni sawa na kusema wamemuondoa kichwani alipokuwa amewakalia na sasa wamemuweka mabegani, hivyo katika cheo cha balozi muda wowote Rais ana uwezo wa kukutengua,” anasema.

Humphrey Polepole

Kuhusu fumbo la mbunge mteule kutenguliwa na Rais, Dk. Albanie anasema Rais hana mamlaka hayo kikatiba ila hutumia ibara ya 67(2)(g) ya Katiba ambayo imesema; ubunge utakoma ikiwa mtu huyo ameshika madaraka ya afisa mwandamizi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Anasema kitendo cha Polepole kukubali uteuzi huo wa Ubalozi, ni dhahiri sasa hatoweza kuendeleza harakati zozote za kisiasa nchini alizokuwa akizifanya kutokana na kubanwa na mazingira pamoja na taratibu kibalozi.

Hoja hiyo inaungwa Mhadhiri Mwandamizi wa masuala ya Diplomasia, Abbas Mwalimu ambaye anasema watanzania wametafsiri kuwa teuzi za ubalozi ni sawa na kufungwa mdomo kwa sababu wanaorejea kutoka kwenye nafasi hizo huwa wakimya.

“Hii ni kutokana na mazingira na taratibu za kazi, hata Polepole akienda kule baada ya miaka miwili akirejea hatakuwa Polepole mwanaharakati, kwa sababu bado ana umri mdogo hajafikisha miaka 50 ataweza kutumika zaidi kwenye nafasi nyingine,” anasema.

Akizungumzia kuhusu vigezo vya COVID-19 katika nchi ya Malawi ambayo tangu Januari mwaka huu imeweka masharti kuwa mgeni anayeingia kuishi nchini humo lazima apatiwe chanjo au awe amechanjwa, Mwalimu anasema kwa mujibu wa taratibu za teuzi za ubalozi hayo yatakuwa yamezingatiwa.

Anasema Mkataba wa Viena umebainisha kuwa Balozi anapaswa kuheshimu sheria na taratibu za nchi anayoelekea lakini pia ana kinga kama Balozi akiwa kwenye majukumu yake.

Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, Humphrey Polepole
Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, Humphrey Polepole akitoa ufafanuzi juu ya muundo wa Serikali katika Rasimu ya Katiba Mpya

Ameongeza kuwa kabla ya uteuzi, mtu anayetarajiwa kuteuliwa hufuatwa kwa siri na kuulizwa iwapo anaridhia uteuzi na taratibu zake, ambapo akikubali ndipo jina hupelekwa kwa siri nchi atakayoelekea na kufanyiwa mchujo.

Anasema nchi hiyo ikisharidhia ndipo jina la mtu huyo hutangazwa kuwa umma ameteuliwa na Rais kuwa Balozi.

Kwa mantiki hiyo Mwalimu anasema ni lazima Polepole atakuwa amekubaliana na masharti ya kuchanja chanjo ya Corona ndio maana atapelekwa shule ya Diplomasia pamoja na kukutana na viongozi wote wa Serikali akiwamo Rais Samia mwenyewe.

Makala haya yameandaliwa na Gabriel Mushi.

error: Content is protected !!