Thursday , 2 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Ni mwaka mmoja wa uhuru na kuponya makovu
Habari za SiasaTangulizi

Ni mwaka mmoja wa uhuru na kuponya makovu

Rais Samia Suluhu Hassan
Spread the love

 

WAKATI Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inatimiza kipindi cha mwaka mmoja tangu iingie madarakani tarehe 19 Machi 2021, tayari imefanya mambo ambayo yanaweza kufanyiwa tathmini na kuonesha mwelekeo wake katika nyanja mbalimbali ikiwemo demokrasia na utawala bora. Anachambua Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ingawa ni kipindi cha muda mfupi cha awamu yake lakini mambo aliyoyafanya katika Nyanja ya demokrasia na utawala bora, yanaweza kutumika kama kipimo cha kuweza au kushindwa kutimiza yale aliyoahidi mara baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo.

Katika hotuba yake ya kulihutubia bunge kwa mara ya kwanza Rais Samia aliahidi kuhakikisha Serikali yake inakwenda kuendelaza mazuri ya mtangulizi wake na kuanzisha mapya mazuri katika kuhakikisha analeta umoja wa kitaifa na kuponya majeraha.

Kwa mantiki hiyo, kisiasa unaweza ukauita mwaka wa uhuru na kutoka vifungoni, kufuatia Serikali hiyo ya Rais Samia, kuwaacha huru mahabusu waliokuwa wanakabiliwa na kesi za kubambikizwa, ikiwemo Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar na wafanyabiashara maarufu, Habinder Sethy na James Rumegarila.

Hatua hiyo iliyosukumwa na agizo la Rais Samia, kwa vyombo vya kisheria kuwaacha huru wafungwa na mahabusu wanaokabiliwa na kesi za kubambikizwa, pia ilimuacha huru Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na walinzi wake watatu, Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Uhuru huo haukugusa wananchi peke yake, lakini pia umegusa vyombo vya habari baada ya magazeti yaliyofungwa kwa muda usiojulikana, ikiwemo MwanaHALISI, Mawio na Tanzania Daima, kuondolewa vifungoni.

Mahusiano kati Serikali na wadau wengine wa maendeleo, yameanza kurudi kwa kushuhudiwa viongozi wa Serikali, akiwemo Rais Samia mwenyewe kukutana na wahariri wa vyombo vya habari, viongozi wa dini pamoja na wadau wa demokrasia ya siasa ya vyama vingi na makundi mwengine mengi.

Lakini pia, umekuwa ni mwaka wa uhuru kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s), ambapo baadhi yake, ikiwemo Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), ukifunguliwa akaunti zake za benki zilizokuwa zimefungwa Agosti 2020 na kufunguliwa Aprili 2021.

Wakati hayo yanajiri, mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa iko mbioni kutoka kizuizini, baada ya Rais Samia hivi karibuni kuagiza kanuni za kuiongoza ziundwe.

Ni mwaka uliowafungua wakosoaji wa Serikali waliofungwa midomo kwa miaka mitano iliyopita, baada ya Rais Samia, kuruhusu watu wamkosoe kwa staha, kitendo ambacho awali hakikuwepo kwa kuwa wakosoaji walionekana kuwa hawana uzalendo.

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa

Nia ya Rais Samia kutaka watu wawe huru kukosoa Serikali yake, imeonekana zaidi alipowakaribisha Ikulu ya Dar es Salaam, viongozi wa dini walio kinara katika jambo hilo, akiwemo Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Kagera, Dk. Benson Bagonza.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani, ameonesha nia ya kushirikiana kwa karibu na vyama vya siasa vya upinzani, kufuatia hatua yake ya kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama hivyo.

Akiwemo Mbowe na makamu mwenyekiti wake Bara, Tundu Lissu, ambapo walikubaliana kushirikiana katika kuijenga nchi.

Hali kadhalika, ndani ya Serikali hiyo, mkutano wa wadau wa siasa wa kujadili hali ya kisiasa nchini ulifanyika mwishoni mwa 2021, ambao ulitoa maazimio ya namna ya kumaliza changamoto zilizopo, hasa upatikanaji wa tume huru ya uchaguzi, katiba mpya na kurudisha mikitano ya hadhara ya vyama vya siasa.

Pia, mkutano mwingine umeitishwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), nacho kimeitisha mkutano wa vyama vya siasa utakaofanyika mwishoni mwa Machi 2022, jijini Dodoma,ambapo Rais Samia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Askofu wa Dayosisi ya Karagwe, ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Benson Bagonza

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani, matukio ya watu kutekwa, kukamatwa na kuuawa na watu wasiojulikana, yamepungua na hayasikiki kama ilivyokuwa miaka mitano iliyopita, ambapo ilikuwa kawaida kwa watu kutekwa, kukamatwa na au kupotea kabisa.

Ikiwa tofauti na Serikali ya Awamu ya Tano, Serikali hii imefanikiwa kupunguza vitendo vya wateule wa Rais kuwa wababe kwa wananchi, kufuatia hatua ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, kutumbuliwa kisha kufunguliwa mashtaka kwa matumizi mabaya ya ofisi akiwa madarakani.

Serikali hiyo imefanikiwa kurejesha mahusiano ya Tanzania na mataifa pamoja na mashirika ya nje ya nchi, kutokana na hatua ya Rais Samia kufanya ziara nje ya nchi, zilizokwama katika Serikali ya mtangulizi wake.

Lengai ole Sabaya

Hali kadhalika, imefanikiwa kupunguza ukata katika mifuko ya wananchi, pamoja na kuwapandisha madaraja baadhi ya watumishi wa umma, ambao hawakupandishwa kwa miaka kadhaa.

Mwaka huo pia umerejesha mazingira mazuri ya wawekezajina wafanyabiashara nchini kutekeleza shughuli zao, kufuatia Serikali ya Rais Samia kuwatengenezea mazingira mazuri ya uwekezaji.

Licha ya mwaka huo kuzungukwa na matukio yaliyowapa uhuru wananchi, kuna matukio mengine yaliwapa vilio wananchi hasa wafanyabiashara wadogo ‘wamachinga’ walioondolewa kufanya biashara pembezoni mwa barabara na katikati ya mji.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kamati ya Bunge yaitaka Serikali ichukue hatua kudhibiti mfumuko wa bei

Spread the love  SERIKALI ya Tanzania imetakiwa kufanya tathimini dhidi ya changamoto...

Habari za Siasa

Bunge lataja kinachokwamisha Mradi wa Mchuchuma na Liganga

Spread the love  MRADI wa uchimbaji chuma cha Liganga na Makaa ya...

Habari za Siasa

Chongolo aagiza watendaji wanaoonyesha mianya ya rushwa wakamatwe

Spread the love   KATIBU mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa...

Habari za Siasa

TRA iweke mfumo wa msamaha wa kodi kutekeleza miradi

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Taifa kimeitaka Mamlaka ya Mapato...

error: Content is protected !!