May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ni miaka 37 kicho cha Sokoine

Edward Sokoine

Spread the love

 

EDWARD Moringe Sokoine, aliyekuwa waziri mkuu wa Tanzania, amefikisha miaka 37 tangu alipofariki dunia, Alhamisi ya tarehe 12 Aprili 1984, katika ajali ya gari eneo la Dakawa, Mvomero mkoani Morogoro, akiwa safarini kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Sokoine alifikwa na umauti akiwa na miaka 45 na taarifa za kifo chake, kutolewa na aliyekuwa rais wa wakati huo, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Msafara wa Sokoine, uliondoka mapema Alihamis, tarehe 12 April 1984, uliondoka Dodoma, akiwa ndani ya gari aina ya Mercedes Benz. Msafara huo uliongozwa na gari la polisi, ambapo kila ulipopita magari yalikuwa yakiupisha kwa kukaa pembeni.

Msafara huo ulipofika eneo la Dakawa, ghafla kilisikika kishindo kikubwa, ambapo gari lililombeba Sokoine liligongana uso kwa uso na gari aina ya Toyota Landcruiser lililokuwa likiendeshwa na Dumisani Dube, aliyekuwa mpigania uhuru wa chama cha ANC aliyekuwa akiishi Mazimbo, Morogoro.

Inaelezwa, Dube licha ya kusimamishwa na polisi, hakusimama kwavile alikuwa kwenye mwendo kasi.

Sokoine, ambaye alikuwa amekaa kiti cha nyuma, inadaiwa hakuwa amefunga mkanda, alirushwa na kugonga kioo cha mbele, ambapo aliumia sana kifuani na shingoni na kufariki kabla ya kufikishwa hospitali ya serikali mkoani Morogoro, ambako madaktari walithibitisha kifo chake.

Yusto Chuma, aliyekuwa mlinzi wake, aliyekuwa amekaa kiti cha mbele kushoto, aliumizwa vibaya na Ally Abdallah,ambaye alikuwa ndiye dreva wake, alivunjika mguu.

Hayati Mwalimu Nyerere, alitangaza kifo cha Sokoine kupitia, Radio Tanzania.

Mwalimu Nyerere, baada tu ya wimbo wa Taifa kupigwa, kwa uchungu mkubwa lakini kwa ujasiri wa hali ya juu, akalitangazia Taifa msiba huo wa kihistoria nchini humo.

“Ndugu wananchi, leo hii, ndugu yetu, kijana wetu, Edward Moringe Sokoine, waziri mkuu wa Tanzania, alipokuwa akirudi Dar es Salaam toka Dodoma, gari lake lilipata ajali na amefariki dunia. Ndugu Watanzania, naomba muamini Edward amefariki kwa ajali na si kitu kingine,” alisema Mwalimu Nyerere

Mwili wa Sokoine, ulizikwa nyumbani kwake, Monduli mkoani Arusha.

error: Content is protected !!