July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ni Makonda vs Kubenea Kisutu

Spread the love

SAED Kubenea, Mbunge wa Ubungo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers ana kesi ya kujibu katika kesi iliyofunguliwa na Jamhuri tarehe 15 Desemba mwaka jana, anaandika Faki Sosi.

Hatua hiyo, itasababisha Kubenea na Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kiondononi kuendelea kupambana kwenye Mahakama ya Mkazi Kisutu Jumatatu wiki ijayo ambapo kesi hiyo imefunguliwa.

Kesi hiyo ilifunguliwa baada ya Kubenea na Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kiondononi kugombana kwenye Kiwanda cha Nguo cha TOOKU kilichopo Ubungo, jijini Dar es Salaam tarehe 14 Desemba mwaka jana ambapo Kubenea alikamatwa na polisi kwa amri Makonda.

Ikiwa ni baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote kabla ya leo, Thomas Simba, Hakimu Mkazi Mahakama ya Kisutu amesema kuwa, Kubenea ana kesi ya kujibu kutokana na mashitaka yake.

Kwenye mahakama hiyo, Makonda alifungua madai matatu dhidi ya Kubenea ambayo ni lugha ya matusi, kuitwa mpumbavu, mjinga pamoja na cheo cha kupewa.

Hakimu Simba amesema, kwa mujibu Sheria Kifungu cha 230 sura 20 kinampa haki mshitakiwa ya kuachiwa huru endapo hana kesi ya kujibu na kwamba akiwa ana kesi ya kujibu basi anatakiwa kujibu kesi ya msingi.

Amesema kuwa, Kubenea anatakiwa kujibu mashtaka mahakamani akiambatana na mashahidi na kuwa, upande wa mshitakiwa utaleta utetezi wake.

Hata hivyo, Hakimu Simba amepokea ombi la wakili wa Kubenea, Peter Kibatala kuwa kesi hiyo isikilizwe 7 Machi mwaka huu.

Kibatala ameieleza mahakama kuwa, kwa upande wa mshitakiwa kuna mashahidi wa nne ambao watafika wote siku hiyo.

Ilivyokuwa

Katika mgomo huo kwenye Kiwanda cha Nguo cha TOOKU Kubenea alisikiliza kero za wafanyakazi ambao walikuwa wakivutana na menejimenti ya kiwanda hicho na baada ya makubaliano yaliyohusisha pande mbili, walikubali kuendelea na kazi.

Hata hivyo, wakati mbunge huyo pamoja na viongozi wa kiwanda hicho wakiwa katikati ya mazungumzo, Makonda aliwasili katika eneo hilo la kiwanda kilichopo ndani ya Mamkala ya Uwekezaji EPZ, Mabibo External.

Baada ya kufika, Makonda hakutaka kuhoji kuhusu kilichoendelea kwenye mgomo huo wa wafanyakazi na kutaka kuanza upya kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi licha ya Kubenea kuupatia ufumbuzi kwa mazungumzo yaliyohusisha pande zote.

Kutokana na hatua hiyo, Kubenea hakupinga hatua hiyo ingawa Makonda alipomaliza kuzungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho, alifunga mkutano bila kuruhusu hoja yoyote kutoka kwa mbunge huyo.

Hali hiyo ilimfanya Kubenea kuhoji sababu ya kutopewa nafasi ya kuzungumza wakati ndiye alikuwa wa kwanza kufika katika eneo la tukio saa nne asubuhi na kulimaliza suala hilo.

Pamoja na hali hiyo Makonda, alipinga hoja ya Kubenea kuzungumza na wafanyakazi hao na kusema kwamba tayari amekwisha kufunga mkutano, hivyo haruhusiwi mtu mwingine kuzungumza kwa kuwa ndiye alikuwa mzungumzaji wa mwisho na tayari alikuwa amefunga.

Hatua hiyo ilizua mabishano makali baina ya Kubenea na Makonda kwa kila mmoja kusimamia kile anachokiamini.

Wakati hayo yakiendelea, Kubenea aliendelea kuwasihi wafanyakazi hao watulie, lakini Makonda akasisitiza hatozungumza hali iliyosababisha polisi waliokuwapo katika eneo hilo na baadhi ya viongozi wa kiwanda kuingilia kati kusuluhisha mzozo huo.

“Huwezi kufunga mkutano nisiongee na wafanyakazi ambao ni wapiga kura wangu, nimekuja hapa tangu asubuhi nimepambana hadi tukafikia hapa na niliwaahidi nikitoka kwenye kikao cha utawala nitawapa mrejesho (yaliyojiri).

“Inakuwaje wewe umekuja sasa hivi unazungumza na kufunga mkutano kwa ubabe?,” alihoji Kubenea huku Makonda akiendelea kusimamia msimamo wake kwamba tayari amefunga mkutano.

“…mimi hawa wamenipigia kura, wewe umepata kura ngapi, huwezi kunifanya lolote wewe,” alisema Kubenea. Baada ya mabishano hayo, Makonda aliamuru Kubenea akamatwe pamoja na kuamuru mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Star TV kunyang’anywa kamera yake.

Polisi walimtaka Kubenea kupanda kwenye gari lao la polisi (Defender) lakini kukatokea mabishano makali, kwani Kubenea alipinga kupanda gari lao umuazi waliokukubali na hatimaye askari wawili wenye silaha na mmoja ambaye hakuwa na silaha waliingia kwenye gari la mbunge huyo hadi Kituo cha Polisi cha Magomeni.

error: Content is protected !!