August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ni lini mifugo itakuwa na thamani?

Spread the love

MOJAWAPO ya hatari inayoinyemelea Tanzania ni migogoro kati ya wakulima na wakulima wafugaji inayoendelea katika maeneo mbalimbali hapa nchini, anaandika Michael Sarungi.

Tanzania inashika nafasi ya pili kwa kuwa na mifugo mingi barani Afrika ikiwa na ng’ombe wapatao milioni 25, mbuzi milioni 16.7, kondoo milioni 8, nguruwe milioni 2.4 na kuku wapatao milioni 36.

Kati ya hao ng’ombe milioni 25 takwimu zinaonesha kuwa wa asili ni asilimia 98 ambayo ni sawa na asilimia 2 wa ng’ombe wote nchini wanaofugwa kwa mfumo wa ufugaji wa kisasa.

Tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa, ufugaji wa asili unachangia asilimia 7.4 ya pato la taifa hali inayoonesha umuhimu wa sekta hii hapa nchini.

Kwa miaka mingi sekta hii ya ufugaji imekuwa ikitegemewa na idadi kubwa ya Watanzania kuendesha maisha katika shuguli za maendeleo yao.

Pamoja na kuwa na mchango mpana katika ukuaji wa uchumi ndani ya nchi lakini mtazamo hasi wa  makundi mbalimbali ya watu katika jamii na hata baadhi ya wanasiasa na baadhi ya viongozi ndani ya serikali wakichukulia ufugaji wa asili kama mfumo uliopitwa na wakati bila ya kuja na mbinu mbadala.

Wamekuwa wakiuchukulia kama mfumo uliopitwa na wakati usiokuwa na tija na wenye kusababisha uharibifu wa mazingira ndani ya nchi kiasi cha kusababisha watu hawa kuonekana na kama wakimbizi ndani ya nchi.

Kwa mfano bajeti ndogo ya sekta ya mifugo inayotengwa kila mwaka imechangia kwa kiwango kikubwa kwa kutokupatikana kwa huduma bora za ufugaji wa asili kama vile maeneo ya malisho, masoko, majosho na huduma za ugani.

Hali hii imechangia ufugaji wa asili kukumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ni tishio kwa ustawi wa mfumo huu wa ufugaji asili na jamii kwa ujumla.

Kwa mfano sera ya wanyamapori ya 1998 inazuia uwepo wa mifugo katika maeneo ya wanyamapori ilhali maeneo mengi ya yakitwaliwa kwa ajili ya hifadhi.

Hata sheria ya hifadhi ya mazingira ya 2007 inaainisha kuwa ufugaji wa asili ni mojawapo ya vyanzo vya uharibifu wa mazingira hali inayochangia kuleta migongano kati ya wafugaji wa asili, mamlaka husika na makundi mengine ya kijamii.

Sheria kama hizi na nyingine nyingi ndizo zimekuwa kichocheo cha migogoro inayoendelea nchini miongoni mwa wakulima na wafugaji huku watendaji ndani ya serikali wakitumia migogoro hiyo kama mitaji ya kisiasa.

Wanasiasa wetu wamekuwa ni watu wa kusubiri itokee migogoro ili waende wakatafute ufalme wa kisiasa, hii ni hatari kuwa na viongozi kama hawa.

Mara nyingi migogoro baina ya wakulima na wafugaji asili imekuwa ikitokana na kutotambulika kwa haki ya umiliki wa ardhi ya wafugaji asili.

Ili Tanzania iweze kukabiliana na changamoto zinazokabili ufugaji wa asili inapaswa kuwepo kwa mipango thabiti ikiwepo kutenga rasilimali fedha na watu wa kuweka utaratibu wa kutenga, kulinda na kutetea maeneo ya malisho.

Pawepo na utaratibu unaotambulika kisheria juu ya haki za wafugaji asili ambao wamekuwa na mchango mkubwa ndani ya taifa hili tangia nchi hii ipate uhuru.

Pamoja na jitihada za zimamoto zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa kiserikali lakini mara nyingi upande wa wanasiasa katika ngazi mbalimbali wamekuwa wakitumia migogoro hii ya wakulima na wafugaji kama mtaji.

Wamekuwa wakipotosha kuwa maeneo mengi yanayokaliwa na wafugaji hayana mwenyewe na kusababisha wavamizi kuingilia maeneo hayo kwa nguvu bila ya ridhaa ya vijiji husika vya wafugaji.

Wakulima kwa kupitia wanasiasa wamekuwa wakikataa kutambua haki za wafugaji kumiliki ardhi na hata kupinga uhalali wa vijiji vya wafugaji.

Hali hii endapo itaachwa iendelee inaweza kuja kuwa na madhara makubwa na kukwamisha maendeleo ya taifa ni bora mamlaka husika zikaja na mipangokazi ya kuyamaliza matatizo haya.

error: Content is protected !!