Friday , 1 March 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Ni lini Afrika itaonja siasa safi?
Makala & Uchambuzi

Ni lini Afrika itaonja siasa safi?

Chris Musando, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Masuala Teknolojia wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka Nchini Kenya (IEBC)
Spread the love

Na Rashid Abdallah
NINAJIULIZA ni kwanini siasa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinaendelea kuwa za vilio, vitisho, mateso na hata vifo. Kwamba siasa haitimii mpaka watu wengine wajikute wamo ndani ya hilaki hizo. Inakuaje lakini?

Ukiizunguka Afrika utakutana na siasa za majitaka – siasa zilizojaa fitna, kukashifiana, upotoshaji na mkubwa kumla mdogo. Ndio siasa zinastawishwa na viongozi, ikiwa na maana wanazihamasisha wafuasi waziamini na wao wazitekeleze.

Kenya imeweka mfumo wa matokeo ya urais kuhojiwa na Mahakamani ya Juu (Supreme Court). Lakini, jambo linalosikitisha ni kwamba wale watumishi wanaosimamia mfumo huu, wanatishwa kwa sababu tu walitoa hukumu isiyopendezesha wenye madaraka.

Jaji David Maraga akishirikiana na majaji wengine watano kuunda jopo lililosikiliza na kuamua malalamiko ya mgombea na kundi la upinzani la NASA, walitoa uamuzi wa kufuta matokeo ya urais.

Ni mchakato wa kidemokrasia lakini kwa uzoefu wa siasa barani Afrika, wengine wanaamini ni mapinduzi dhidi ya rais Uhuru Kenyatta anayeomba ridhaa mara ya pili.

Kabla ya uchaguzi kuanza, afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) akihusika na kudhibiti mfumo wa kigitali wa kukusanya na kuhakiki matokeo ya kura, Chris Musando, aliuawa.

Siku kadhaa baada ya tukio hilo, afisa mwengine katika Kaunti (Kata au Wadi) ya Siaya, Mwalimu wa Shule ya Sekondari, Caroline Odinga, naye alibakwa na hatimaye akauawa.

Ukiyaangalia matukio haya yote unaona yalivyo ya kijinga, kinyama na ya ajabu; yanadhihirisha safari ndefu hadi kufikia siasa zilizostaarabika, siasa zenye amani na utulivu wa kweli. Siasa ambazo watu wanapewa fursa isiyopishana ya kushiriki, pasina kuangalia mtu anapenda mrengo gani.

Bahati mbaya kila mtu hutumia uwezo alionao kumnyanyasa mwengine. Hakukuwa na sababu zenye kuingia akilini kwa maofisa wa tume hii kuuawa, wakati wana dhamana ya kusimamia mambo ya msingi kwa maslahi ya taifa.

Wala hakuna haja ya kumtisha na kumpa taharuki ya roho Jaji Maraga na majaji wenzake waliotoa uamuzi wa kufuta matokeo.

Ni Wakenya wenyewe walioweka na kuridhia nguvu imara ya mfumo wa uchaguzi ikiwemo kuipa mamlaka mahakama ya juu kuthibitisha matokeo ya urais.

Pia, usisahau uchaguzi wa mwaka 2007 ulivyosababisha mauaji ya watu wengi. Yote ni matokeo ya siasa zilizojaa kutu za ushamba, miba ya ubabe na tofauti za mitizamo. Haya huchafua tija iliyotarajiwa katika mifumo ya kidemokrasia.

Ukienda Rwanda kwa Jenerali Paul Kagame, moja ya habari ambazo zimetikisa katika vyombo vya habari wiki hii, ni kuhusu mwanadada Diane Rwigara kushitakiwa mahakamani. Diana alitangaza kugombea urais dhidi ya Kagame aliyeomba tena ridhaa ya kuongoza.

Alipelekwa mahakamani baada ya kukamatwa mara kadhaa na kuwekwa kizuini. Ona, ni kama vile Katiba ya Rwanda inakataza rais aliyeko madarakani kupingwa wakati unapokuja uchaguzi mwingine. Kwa hivyo, ni siasa iliyomtia Diana katika mtihani kimaisha.

Jambo la kwanza mara baada ya kutangaza nia ya kugombea urais, ghafla mitandao ikafunikwa na picha zake za utupu, ambazo mwenyewe ameziita “ni za bandia.” Lakini ziliathiri kwa kiasi kikubwa harakati zake za kutaka kuwania urais dhidi ya Kagame. Hatimaye alizuiwa kugombea.

Picha hazijatosha, kwa sasa ana msururu wa kesi mahakamani ikiwemo ya kuchochea uasi. Ni kesi zilizozuka ghafla kama moto wa kifuu baada ya kutangaza upinzani.

Sijui kesi hizi zina uzito gani au ukweli upi, lakini ukiangalia namna zilivyozuka, unapata shaka ikiwa zina msingi au za kubambikiziwa kwa lengo la kumchafua.

Kila nchi katika bara la Afrika, ni adimu kufungua historia ya siasa zao na kukuta zimenyooka au zimesalimika na damu au roho za maelfu ya watu zilizopotea kwa dhulma.

Ni aibu kwa siasa za Afrika, wakati huu tunakumbuka kifo cha mwanamapinduzi Ernesto Che Guevara, mzaliwa wa Argentina, ambaye kwa wakati fulani aliishi Afrika akipigania kupanda mbegu za kimapinduzi kwa Waafrika, dhidi ya uonevu wa Wakoloni.

Hata baada ya Wakoloni kutoa uhuru zaidi ya miaka 50, Waafrika wanaendelea kushuhudia siasa zilizojaa chuki na hasadi miongoni mwa wananchi. Majadiliano na fikra ya amani na utulivu wa kweli havipewi nafasi yake.

Tanzania haina tofauti na mataifa mengine yaliyozongwa na siasa za majitaka. Wapinzani wamekuwa wakisakamwa kwa kila namna. Sasa hata ule msingi wa kurudishwa kwa siasa za vyama vingi, unavunjwa ingawa bado unatambuliwa na Katiba na umewekewa sheria.

Siasa zilizojengwa kwa misingi ya ubabe, ukamataji, ubambikiziaji kesi, ukiwa mfunguaji mdomo, unatishwa ili unyamaze.

Ukienda Zanzibar hakuna afadhali. Mfumo wa vyama vingi haujaisaidia nchi kubaki imara kiusalama. Wapinzani wanasakamwa na mwenendo wa kupindua maamuzi ya wananchi wanapochagua viongozi wawatakao waongoze, unashika nguvu kila kukicha.

Watawala wakishadhibiti mambo ya kuhujumu haki ya wananchi kuchagua watakacho, wanatekeleza sera ya kuzima harakati za kudaiwa haki. wanawatumia askari kuendesha operesheni za kushambulia wananchi kwa silaha za moto na za jadi.

Askari hao wanaotumia gari za serikali, hupita mitaani na kushambulia wananchi wenye mtizamo wa upinzani dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Makumi wanajeruhiwa na sasa tayari mashambulizi yamesababisha mtu kukata roho.

Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na nchi kadhaa eneo la magharibi na katikati mwa Afrika, zimo shidani. Wanaoongoza wanasigina katiba na kujibakisha kibabe.

Siasa imegeuzwa na kuwa miba kwa Afrika. Wale waloshikilia mpini wa madaraka, hawasikilizi matakwa ya umma. Sauti ya umma inazimwa kwa kusakamwa viongozi wa upinzani.

Kuna jambo la msingi kila mmoja anapaswa kulizingatia, kuendelea kuvurugwa siasa ni kuendelea kuhujumu Afrika na maisha ya watu wake. Hivyo wale wanaozibovua siasa, watambue wanawaumiza Waafrika pia.

Wala hakuna malaika au mzungu atazuka kuja kuzistaarabisha siasa ikiwa wenye mamlaka hawajaamua kufanya hivyo, waache kufikiria maslahi yao na wawafikirie wanaopata tabu kwa sababu ya siasa za majitaka.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Makala & Uchambuzi

Vijana wanavyoandaliwa kuziba pengo la ujuzi sekta ya madini

Spread the loveMOJAWAPO ya sekta ambazo katika miaka ya 2000 hazikuwa na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Lowassa: Mwanasiasa aliyetikisa CCM, Chadema

Spread the loveWAZIRI Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Edward Lowassa (70) amefariki Dunia...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Uongozi wa Samia kuendelea hadi 2030

Spread the loveKWETU sisi tuliowahi kusoma sekondari, iwe O levo au A...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Bado askari wastaafu wanaonewa

Spread the loveRAIS wangu Samia Suluhu Hassan tunaendelea kumshukuru Mungu kwamba wote...

error: Content is protected !!