July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ni kina Mdee au Chadema leo

Spread the love

 

HATIMA ya Halima James Mdee na wenzake 18, kuendelea kuupigania ama kuutema, ubunge wao wa Viti Maalum, wanaodaiwa kuupata kinyemela, utajulikana leo Jumatano, 22 Juni 2022, wakati Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, itakapotoa uamuzi wa maombi walioyoyawasilisha mahakamani hapo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mdee na wenzake walifungua maombi mahakamani kupinga kuvuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jambo ambalo lilikuwa linawafanya kupoteza sifa za kuendelea kuwa wabunge.

Walifikia uamuzi wa kukimbilia mahakamani, baada ya Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, kuamua tarehe 27 Novemba 2020, kuwavua uanachama na baadaye mkutano wa Baraza Kuu wa 11 Mei 2022, kusikiliza rufaa zao na kufikia uamuzi wa kuwatimua.

Chadema walifikia uamuzi wa kumtimua Mdee na wenzake, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (BAWACHA), kufuatia kupatikana na makosa ya usaliti, kughushi nyaraka za chama na kisha kujipeleka bungeni kujiapisha kuwa wabunge, kinyume na maelekezo ya chama chenyewe.

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu (CC), Esther Matiko na Ester Bulaya; aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Wengine, ni aliyekuwa Katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA), Nusrat Hanje; aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa; Cecilia Pareso, Agnesta Lambart, ambaye alikuwa mwenezi wa Bawacha na Tunza Malapa, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, mkoani Mtwara.

Katika orodha hiyo, wamo pia Asia Mohammed, aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa Bawacha (Zanzibar), Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Wote kwa pamoja, waliapishwa kuwa wabunge, tarehe 24 Novemba 2020 na aliyekuwa spika wa wakati huo, Job Ndugai.

Mara baada ya Baraza Kuu kubariki uamuzi wa kuwavua uanachama wanachama hao, wote kwa pamoja walifungua shauri mahakamani, ambapo pamoja na mambo mengine, waliomba kuruhusiwa kufungua kesi ya msingi na kutoondolewa bungeni, hadi kesi yao ya msingi itakapomalizika.

Maombi hayo yanapingwa na Chadema, kwa hoja kuwa yamefunguliwa kinyume cha taratibu; tayari mapingamizi hayo yamesikilizwa, 13 Juni 2022.

Peter Kibatala, mmoja wa mawakili katika shauri hilo, akiongoza jopo la mawakili wa Chadema, aliwasilisha hoja tano mahakamani kupinga maombi hayo kupokelewa.

Kwa mujibu wa sheria, iwapo Mahakama itakubaliana na hoja za wadai – Mdee na wenzake – basi wataweza kufungua shauri lao kuu mahakamani na hivyo kuendelea kukalia viti vya ubunge wakati kesi ya msingi inaendelea, lakini ikiwa watakataliwa, basi watalazimika kuondoka mjengoni.

Uamuzi utakuwa na mambo mawili, Mdee na wenzake 18 wana hoja zitakazosimama na kuwa na shauri mahakamani ili Mahakama iwaruhusu kuendelea na madai yao au kutupiliwa mbali.

Mdee na wenzake, wanaiomba Mahakama itengue uamuzi wa Chadema wa kuwavua uanachama, kuchunguzwa mchakato wa kupitishwa majina yao ndani ya Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC) na maombi madogo ya zuio la kuondolewa kwenye nafasi zao.

Kwenye maombi hayo, kina Mdee wanaishitaki NEC, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Bodi ya Udhamini ya Chadema.

Mbele ya Jaji John Mgetta, mawakili wa Chadema, Peter Kibatala, Dickson Matata na Jeremiah Mtobyesya, waliwasilisha mapingamizi kuishawishi Mahakama kutupilia mbali maombi hayo.

Hoja ya awali ya upande huo ulidai waombaji walikwenda kinyume cha sheria kwa kuiweka NEC kama sehemu ya wadaiwa kwenye maombi hayo, kitendo ambacho kinakinzana na Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri.

Katika hoja ya awali, Kibatala alidai mahakamani hapo kuwa mawakili wa waombaji walisaini nyaraka ya maelezo, sehemu ya waombaji kana kwamba waliomba wao, jambo linalokinzana na sheria.

Alisema: “Wenzetu wamejitungia sheria yao, wamesaini sehemu ya waombaji tena wamesaini mara mbili saini zote za mawakili.”

Aidha, mawakili hao walidai kuwa waombaji walishindwa kuthibitisha maelezo na badala yake, wamethibitisha kiapo cha waombaji.

Waliendelea kuieleza Mahakama kuwa maombi hayo yalikwenda kinyume cha sheria, kwa kuwa mlango uliotumiwa kuomba, ni kulazimisha kufanywa na Mahakama, ikiwa tayari Chadema imefanya uamuzi wake kisheria.

Walisema, mlango huo unatumiwa na uamuzi unaofanywa kwenye ofisi ya umma, kwamba kuna uamuzi umefanywa na kuna upande hujaridhisha ndiyo hutumia mlango huo.

Hata hivyo, mawakili wa kina Mdee, wakiongozwa na Aliko Mwamanenge, ulijibu madai hayo kwa kusema, maombi hayo yana miguu ya kisheria na kwamba hoja hizo hazina msingi wowote.

Kwamba, hoja kuwa Chadema haishitakiwi kwa kuwa si ofisi ya umma, siyo halali, kwa kuwa chama hicho ni cha umma na sheria ya vyama vya siasa, inathibitisha kuwa hiyo ni mali ya umma.

Wakatumia sheria inayompa mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kukagua vyama vyote vya siasa, kwamba kwa kupitia sheria hiyo, Chadema kinathibitika kuwa ni chama cha umma.

Shauri hilo lililoanza takribani saa 7 mchana na kumalizika saa 12 jioni, anbapo Jaji Mgetta aliliahirishwa hadi leo kwa ajili ya uamuzi wa hoja hizo.

Wafuasi kadhaa wa Chadema walihudhuria mahakamani hapo wakiongozwa na John Mnyika, katibu mkuu wa chama hicho na walipotoka nje baadhi ya wanawake walibeba mabango yaliyosomeka: “Wanawake acheni ubabe,” na “Njaa imewatia aibu” na “Wasaliti,” huku wakiimba Peoples Power.

error: Content is protected !!