June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NHIF yazindua huduma mpya ya TIKA

Spread the love

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) leo umezindua mfuko wa afya ya jamii ambapo wananchi watapata fursa ya kuchangia huduma za matibabu kwa hiari kwa njia ya kadi (Tiba kwa Kadi-TIKA) ambao unatarajiwa kuanza Januari 1 mwaka 2016. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Aidha, mfuko huo umepangwa kuwepo katika kila wilaya jijini Dar es Salaam. Mfuko huo umezinduliwa rasmi katika Manispaa ya Kinondoni ambapo uzinduzi huo ulienda sambamba na mafunzo kwa watoaji huduma za afya kutoka katika vituo vya afya mbalimbali kwenye manispaa hiyo.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti NHIF, Rehani Othuman amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ni kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi hata wanapokuwa hawana pesa.

Othman amesema, ili kujiunga na mfuko huo wa TIKA kila mwananchi anapaswa kuchangia 40,000 kwa mwaka ambapo pia serikali itamuongezea 40,000 kiasi ambacho kitampatia matibabu ndani ya mwaka mzima.

“Huduma hiyo itakuwa katika vituo vyote vya Hospitali za Serikali ambapo utasajiliwa na kupatiwa kadi. Kila mtu hadi watoto wanatakiwa kulipiwa ili waweze kupata matibabu na pia itaepusha usumbufu kwa watoa huduma kushika mkononi hizo pesa,” amesema Othman.

Lengo lingine amesema ni uboreshaji wa huduma za afya nchini ikiwa ni katika harakati za kupunguza umaskini kwa wananchi na kuboresha huduma za afya katika jamii.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Azizi Msuya amesema kuwa manispaa ndio itachukua jukumu la kutayarisha watoa huduma hao na kuhimiza umuhimu wa utoaji huduma bora kwa wanachama ambao watajiunga kwenye mfuko huo na kuhakikisha kuwa kila kituo kinakuwa na dawa za kutosha kabla ya mgojwa kuugua.

Amesema, watahakikisha TIKA unamwezesha mwanachama kupata huduma kwa mwaka mzima bila kuchangia tena na kuhakikisha kuwa michango yote inayotolewa inaboresha huduma ikiwemo ya kuboresha miundo mbinu na ukarabati wa mawodi na vitanda.

Pia, amewataka viongo wa manispaa wa ngazi zote kulichukulia uzito suala hilo na kuhakikisha wananchi wanaelewa na kujiunga kwa wingi na mpango huo kwani ni ukombozi wa afya zao.

error: Content is protected !!