August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NHC yaendelea kukunjua makucha

Spread the love

SIKU tatu tangu Rais John Magufuli, kulitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuendelea na shughuli ya kuwafukuza na kukamata mali za wapangaji wanaodaiwa kodi na shirika hilo zikiwemo taasisi za serikali, kazi hiyo imeendelea tena leo, anaandika Pendo Omary.

Rais Magufuli alitoa siku saba kwa wizara na taasisi za umma zinazodaiwa na NHC kulipa deni hilo la sivyo shirika hilo litoe nje mali za wadaiwa hao.

“Wasiolipa wote watoe nje kama ulivyomtoa yule jamaa (Freeman Mbowe), hata kama akiwa rais halafu halipi kodi mtoe nje,” alisema Rais Magufuli wakati akihutubia wananchi wa zilizokuwa nyumba za Kota eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam.

Mapema leo asubuhi, NHC imetumia kampuni ya udalali ya OXMart kutoa nje kuzishikilia mali za kampuni ya Centre Point Limited katika nyumba ya NHC iliyopo mtaa wa Samora.

“Centre Point Limited inadaiwa Shilingi 96 milioni na tunawaondoa huku tukishikilia mali zao kwa siku 20, mpaka pale mmiliki wake atakapolipa deni. Asipolipa, mali zake zitauzwa kwa mnada,” amesema Japhet Mwasenga, Meneja wa Kitengo cha Ukusanyaji Madeni NHC.

MwanaHALISI Online imeemtafuta bila mafanikio mmiliki wa kampuni ya Centre Point Limited ili kupata kauli yake kuhusu hatua iliyofanywa na NHC.

error: Content is protected !!