June 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Nguvu ya mtazamo chanya hubadilisha maisha

Spread the love

ILIKUWA ni mshangao kwa wazazi wangu waliposikia kuwa watazaa mtoto asiyekuwa na mikono, Nick Vujicic anasema.

“Nilipozaliwa madaktari waliponiona walisema tunasikitika kuwa hatuna chakusema ni nini kimetokea, haya ni maajabu.’’

Nick Vujicic, mwenye umri wa miaka 33, ni mlemavu asiyekuwa na mikono na miguu na ni Rais wa taasisi inayotoa mihadhara kwa lengo la kuhamasisha na kutia motisha. Nick ni Rais wa makampuni mawili na ameajiri watu kadhaa kwenye kampuni zake.

Nick anatatizo la kiafya alilozaliwa nalo linalojulikana kama tetra-amelia syndrome au Phocomelia. Tatizo hilo limemfanya Nick akose mikono na miguu, hata hivyo ana mguu mdogo na vidole. Pamoja na ulemavu huo Nick anauwezo wa kuchapa, kushika vitu na kupiga mpira kwa kutumia mguu mdogo alionao. Pia amekuwa mara kwa mara akipendelea kuogelea na kuruka kutoka angani kwa kutumia miamvuli maalum ya kurukia.

Nick ni mmoja wa watu wachache duniani wenye ulemavu lakini wamekuwa na matumaini na kutokata tamaa kwa kuamini hakuna kinachoshindikana kama unaamua huku ukimtumainia Mungu.

Uwezo huu haukuja tu hivihivi kwa Nick aliyekulia mji wa Melbourne nchini Australia, aliangaika sana akiwa shuleni huku akifanyiwa ubabe na wanafunzi wenzake kiasi kwamba akapata mfadhaiko (depression). Kutokana na manyanyaso hayo alipokuwa na umri wa miaka 10 alijaribu kujiua. Tatizo hili la kunyanyaswa lilimfanya Nick kuanzisha taasisi ya kutetea wanaonyanyaswa na kuzuia wenye mawazo ya kujiua.

Kadri muda ulipokuwa unaenda Nick alibadilisha mtazamo na fikra zake na kuanza kuwa na mtazamo chanya (positive attitude).

Pamoja na ulemavu alionao, alikuwa na ndoto kuhakikisha anakuwa mtu mwenye uwezo wa aina yake bila ya kujali ulemavu wake. Na kweli aliweza kufikia ndoto zake hizo kwa kuwa na uwezo wa kuogelea, uwezo wa kuruka kwa parachute kutoka angani n.k .

Pamoja na kupata shida katika maisha yake ya kila siku mfano kusafisha meno kwa mswaki huku akiwa hana mikono, amebarikiwa na kuwa muongeaji mahiri anayehitajika sehemu mbalimbali Duniani na ameshazunguka kwenye nchi zaidi ya 60 na mabara 5.

Nick amekuwa chachu ya kuwapa matumaini hasa vijana na wafanyabiashara kuwa wanaweza wakiamua, anasema katika maisha hatupaswi kuogopa kupambana, na tusiogope kushindwa kwani hata kama tumeshindwa sisi sio washindwa, kushindwa ni funzo.

Somo kubwa la matumaini analolitoa Nick ni kuwataka Vijana kutoogopa kufanyaa kazi, kutoogopa kujaribu, kutoogopa kujenga marafiki na mitandao chanya, kutokuwa na aibu, amekuwa akiwataka vijana na wafanya biashara kujitoa kujaribu kufanya wanachoiamini wanaweza na katika harakati zao watakutana na watu watakaowatia moyo kama ambavyo yeye alitiwa moyo kuwa anaweza kuwa muongeaji mzuri na akafanyia kazi ushauri huo na sasa ni kati ya waongeaji wakubwawazuri duniani.

Nick mwandishi wa kitabu kinachoelezea maisha yake kinachoitwa Love Without Limits anaishi California na mkewe Kanae na wana watoto wawili. Nick ni msomi mwenye shahada ya Biashara aliyejikita kwenye uhasibu na mipango ya fedha.

error: Content is protected !!