January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ngurumo: Naiachia mahakama kesi yangu

Spread the love

ANSBERT Ngurumo, aliyekuwa mgombea Ubunge katika Jimbo la Muleba Kaskazini kupitia Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015, amesema ameiachia mahakama iamue hatima yake kesi yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi kwenye jimbo hilo. Anaandika Faki Sosi.

Ngurumo amefikia hatua hiyo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba kugoma kusikiliza ombi lake la kupunguziwa gharama za dhamana ya kesi namba 9 ya mwaka 2015. Katika kesi hiyo, Ngurumo anapinga matokeo yaliyompa ushindi wa ubunge, Charles Mwijage (wa CCM), ambaye sasa ni waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji.

Akijibu swali la mwandishi wa habari hii aliyetaka kujua maendeleo ya kesi hiyo, Ngurumo amesema baada ya mahakama kugomea maombi yake, hakuwa tayari kulipa Tsh. 15 milioni cha dhamana. Fedha hizo ni nje ya gharama ya kesi isiyopungua Tsh. 40 milioni.

Akiandika kujulisha marafiki na wana Chadema katika jimbo lake, alisema: “Napenda kukujulisha kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba imekataa kunipunguzia kiasi cha dhamana ya kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wanataka nilipe kwanza shilingi milioni 15 mahakamani ili kesi ianze kusikilizwa.

“Baada ya kushauriwa na kutafakari, nimeona kiasi cha Tsh 55 milioni (ambazo zingejumuisha dhamana na gharama ya kesi) kinaweza kutumika katika jukumu jingine la kujenga jamii yetu. Nimeamua kuiachia mahakama iamue hatima ya kesi yetu.”

Huku akisisitiza kuwa sheria hii inayomtaka mlalamikaji kulipa kiasi kikubwa cha fedha mahakamani kama dhamana, ilitungwa kulinda watawala, mafisadi na matajiri, na kuminya haki za watu wa kawaida wasiotumia fedha chafu kusaka uongozi, Ngurumo amesema anajipanga kuzindua harakati mpya kwa ajili ya kujenga na kuimarisha upya jamii ya wana Muleba.

error: Content is protected !!