July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ngurumo ampongeza Rais Magufuli  

Spread the love

ANSBERT Ngurumo, Mhariri na mchambuzi wa habari aliyekerwa na Kiingereza cha Rais John Magufuli wiki iliyopita, amempongeza kiongozi huyo kwa usikivu, hasa kwa kutumia Kiswahili jana Jumatano mbele ya mgeni wake, Truong Tan Sang, Rais wa Vietnam aliyepo nchini kwa ziara ya kikazi, anaandika Pendo Omary.

Ngurumo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Yatosha Development Initiative, taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na masuala ya kina mama na watoto;  na ni Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Hali Halisi Publishers, ambaye katika uchambuzi wake kwenye gazeti la MwanaHALISI Jumatatu Machi 7, mwaka huu, alimtaka Rais Magufuli aachane na Kiingereza (isome hapa), na ajenge utamaduni wa kutumia Kiswahili katika hotuba zake ndani na nje ya nchi kama njia ya kuenzi na kukuza Lugha ya Taifa.

Baada ya siku mbili tu, Rais Magufuli akiwa na mgeni wake mbele ya waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam, alizungumza kwa Kiswahili, tofauti na marais waliomtangulia, ambao wamekuwa wanatumia Kiingereza badala ya Kiswahili, huku wageni wao wakizungumza lugha za mataifa yao.

Akizungumza na Mwanahalisi Online jana, Ngurumo alisema, “Katika hili, nampongeza Rais Magufuli na wasaidizi wake kwa usikivu. Kuna watu walionishambulia kwa kumkosoa rais alipozungumza Kiingereza kibovu mbele ya marais wenzake wa Afrika Mashariki, wakidai kwamba namdhalilisha rais. Lakini sasa yeye amewaumbua; ameona umuhimu wa ushauri wangu. Nashauri aendelee hivi hivi. Popote atakapokuwa aachane na Kiingereza, Kiswahili kinatosha. Wafasili watafanya kazi yao.”

Kiingereza hicho kibovu kilizua mjadala kwenye mitandao ya jamii kwa wiki nzima; na uchambuzi wa Ngurumo umezua gumzo an maoni mchanganyiko. Baadhi ya wananchi wanaunga mkono hoja ya Ngurumo, huku wengine wakimshambulia kw akumkosoa rais kupitia gazetini.

error: Content is protected !!