TIMU ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes wanatarajia kucheza michezo miwili ya kirafiki kwa ajili ya kujiweka sawa kabla ya kusafiri kuelekea nchini Mauritania kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Michuano hiyo itaanza tarehe 14 Februari 2021, huku Ngorongoro Heroes ikishuka dimbani tarehe 16 Februari 2021 dhidi ya Ghana kwenye mchezo wa kundi C.
Kocha mkuu wa kikosi hiko Jamhuri Kihwelo amesema kuwa timu hiyo kwa sasa ipo kambini Dar es Salaam ambapo tayari wameshaongea na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, (TFF) kwa ajili ya kuwatafutia michezo miwili ya kirafiki kabla timu haijaondoka.
“Tupo kambini kwa sasa tukijiandaa na mashindano kwa kuwa tumepata bahati ya kushiriki mashindano haya, tuliomba ofisi ya TFF itusaidie kupata mechi mbili za kirafiki na tulitaka tucheze na Morocco ila kwa bahati mbaya tupo nao kundi moja.
“Kilichofanyika ni kutafuta mechi mbili za kirafiki zitakazochezwa hapa ambazo zitachezwa wiki hii kabla ya kuondoka,” alisema kocha huyo.
Tayari TFF wamethibitisha kuwa Ngorongoro Heroes watacheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda ambayo tayari imeshawasili nchini leo mchana tarehe 1 Februari 2021.
Mchezo wa kwanza wa kirafiki utachezwa tarehe 3 Februari majira ya saa 1 usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, huku mchezo wa pili ukipigwa tarehe 6 Februari 2021 kwenye Uwanja huo huo.
Leave a comment