October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ngono vyuoni: Rais Magufuli afura

Rais John Magufuli

Spread the love

VITENDO vinavyoashiria ngono katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), vimemchefua Rais John Magufuli. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba ya MUST leo tarehe 3 Mei 2019, Rais Magufuli amekerwa kuona wanafunzi wakikumbatiana wakati akiwasili chuoni hapo.

“Wakati nakuja nimemuona kijana amekumbatiana na kijamaa mmoja, nikasema angekuwa binti yangu, ningeteremka nimzabe kibao, wote wawili,” amesema Rais Magufuli na kuongeza;

“Haiwezekani akumbatiwe na jamaa ambaye hajatoa hata mahari… kukumbatiana kwanini ufanye barabarani? Kwanini usiende bwenini ukakumbatiane mpaka ulewe kukumbatiwa?.”

Rais Magufuli amesema, vitendo vya kujihusisha na ngono vyuoni vinaathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu ya wanafunzi, na hata kusababisha serikali kutofikia malengo yake ya kuwa na vijana wasomi, kwa ajili ya kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa.

“Unashindwa kuelewa walikotoka na wanakoelekea, serikali imetumia pesa, unafikiri huyu akienda darasani atafaulu? Never (haiwezekani),” amesema.

Amewataka wanafunzi wote nchini kutumia muda wa masomo vizuri, kwa kutochanganya na masuala ya mapenzi.

Aidha, amewataka wahadhiri wa vyuo kutowashawishi wanafunzi kufanya nao vitendo vya ngono, huku akiwataka baadhi yao wenye tabia ya kufelisha mitihani wanafunzi wanaowakataa kujihusisha nao kimapenzi, kuacha kabisa.

“Niwaombe walimu muwe wakali kwenye elimu hakuna siasa. Lakini msiwaonee wanafunzi kwa interest (manufaa) zenu, kwa sababu saa nyingine mnawaambia wachague kufeli au kubembelezwa.

“Mtabembelezwa na wangapi? kila mwaka mnabembelezwa, mtabembelezwa na wangapi?” amehoji Rais Magufuli.

Hata hivyo, ametoa wito kwa wanafunzi hao kusoma kwa juhudi kwa kuwa, serikali inatoa fedha kuwahudumia.

“Nazungumza sababu nawasihi watoto wangu someni ili gharama zinazotumiwa na serikali zitoe matokeo mazuri, tusijenge taifa la vilaza.

“Natoa wito huu kwa wanangu wanachuo tunatoa fedha kwa ajili ya kusomesha nyie mkatambue majukumu yenu.  Mtuonee huruma wazazi wenu hizi fedha ni kodi zao,” Rais Magufuli.

error: Content is protected !!