August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ngono na mwanafunzi yaleta msukosuko Ushirombo

Spread the love

TUMBO John Madaraka, Afisa Tarafa wa Siloka, Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita, yupo matatani kwa kufanya ngono na mwanafunzi, na kusababisha ashindwe kufanya mtihani wa taifa wa kidato cha nne mwaka 2015, anaandika Ansbert Ngurumo.

Anatuhumiwa “kumbaka” Winifrida Richard (18), akiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Uyovu, Februari 2015, na kufumaniwa akiwa naye chumbani kwake, katika Kijiji cha Kanembwa, Kata ya Uyovu, majira ya saa nne usiku.

Waliofanya fumanizi ni Richard Peter, baba mzazi wa Winifrida, akiwa na wanakijiji wengine wawili. Hata hivyo, hakuna kesi iliyofunguliwa mahakamani kuhusu tukio hilo katika mahakama yoyote, wilayani humo. Badala yake, tukio hilo limeleta mpasuko, talaka na ufukara katika familia ya Richard.

Anasimulia: “Mimi nilihusika kufumania, nilikwenda nilimkuta nyumbani kwake, mnamo saa nne usiku, lakini tulikaa pale mpaka saa tisa nadhani na nusu. Wakati ule sasa kumejaa watu, ikabidi nimuite mzee, binti, na majirani, tukaone tuwaite polisi, wakakwepa kuja, kumbe alishawaandikia meseji.

“Ikabidi niwafuate mguu kwa mguu sasa. Nafika njiani napokea simu kwamba binti ametoroka. Nikahoji, ‘ametorokaje wakati wote mko hapo?’  Basi katika hali hiyo, akawa ananiomba mwenyewe mhusika (Tumbo) kwamba nifanye mawasiliano naye, kwamba anilipe shilingi ngapi tulimalize.

“Mimi nikamwambia, ‘wewe ni mtumishi wa serikali unajua utaratibu wa wanafunzi, unawezaje kufanya mambo haya ukiwa mtumishi mwenyewe? Mimi sina muda wa kufanya maongezi na wewe.’ Katika hali hii tulivutana sana.

“Hatimaye, kulikucha asubuhi, nikaona hii kitu inakuwa ngumu, nikaenda kwa diwani alfajiri, nikamwamsha, nikamweleza tukio, akashauri twende kituo cha polisi, tukaenda, Runzewe.

“Jinsi ya kumkamata wakawa wameshindwa, wanasema wana taarifa hizo tangu jana yake usiku lakini ilikuwa ngumu kidogo, wanashindwa wafanyeje. Tukamwambia (polisi), ‘sasa tutafanyaje? Kinachotakiwa ni wewe utuambie tufanye nini hapa.’

“Akatuchenga. Alivyokuwa anatuchenga, kwa kuwa tuna namba za OCCID, tukampigia, akawaamuru wamkamate huyo mtu kwa nguvu. Kumkamata wakashindwa, wakawa wamempigia simu yeye mwenyewe ajilete kituoni, akaja.

“Alipojileta mwenyewe, akaingia pale ndani, akafanya mahojiano, baadaye wakawa wamempeleka Ushirombo, akakaa kule kama siku tatu. Siku ya nne, alikuja katibu tarafa mwenzake anaitwa Murugwa (Lameck), kuja kutuomba jinsi ya kufanya jambo hili kifamilia, kwamba ametumwa na mkuu wa wilaya, ili tuyamalize.

“Akasema tuseme shilingi ngapi ilipwe kama fidia. Sisi tukasema, ‘hatuwezi kusema utupe fidia wakati binti haonekani yupo wapi, na sisi tunajibu nini? Wewe ni kiongozi mkuu, na mkuu wa wilaya anakutuma kuja kufanya madiliano juu ya mwanafunzi…?’

“Tukatofautiana, akasema ngoja nimpigie mkuu tuone anasemaje. Akampigia mkuu wa wilaya simu akaongea naye tukiwa tunasikia kwenye loud speaker. Basi, akasema, ‘mama yake anajua mahali binti huyo alipo.’ Akasema, ‘huyu mhusika (Tumbo) anasema mama ya binti anajua mtoto alipo.’

“He! Tukalewa sasa, tukasema mbona sisi hatujui, yeye anajuaje alipo mtoto? Tukaona inawezekana wana mawasiliano. Katika hali hiyo, tulishindwa kupata mwafaka. Tukasema mpaka binti apatikane, ndo tuweze kujua jinsi ya kufanya.

“Basi bwana; ikaenda hivyo, ikafika mahali wale OCCID na askari wake wakaja kutuhoji, tukawapeleka hadi nyumbani kwake, wakapima eneo, na pale jinsi gari ilivyoingia.

“Walikuwa askari kama watano hivi, wakamaliza, wakarudi nyumbani, nasi tukarudi nyumbani. Tangu hapo ishu ilianza kuyumba.

“…Suala lao lilichengwa upepo kwa sababu baada ya wale viongozi wa wilaya kuwa hawatuungi mkono, wanamtetea kiongozi mwenzao, tukakosa power; na mazingira, si unajua sisi tunaishi kijijini?

“Nilichofanya mimi baada ya kujua mama yake anahusika, nikamfukuza mama yake. Yeye ndo alienda mahakamani sasa, mahakamani hiyo kesi (shauri) ikazunguka, nikajua niko peke yangu na mke wangu, kumbe katibu tarafa mwenyewe ndiye amebeba hiyo kesi (shauri).

“Kwa hiyo tulienda tukahukumiwa nyumba iuzwe kwa thamani ya shilingi milioni 18, mama apewe milioni 6, mimi nipewe milioni 12, na watoto wote nichukue. Nikasema mimi ninayo nyumba moja, sina nyingine, na hawa watoto ni wanane, tutaishije na nyumba yao inauzwa?”

Hukumu ya shauri lao la ndoa Namba 44/2015 ilitolewa na Mahakama ya Mwanzo Runzewe, Bukombe, tarehe 11/09/2015.

Kwa mujibu wa Richard, hadi sasa nyumba haijauzwa kwa kuwa licha ya amri ya mahakama kusema iuzwe kwa sh 18 milioni, wateja wote wanaopatikana wanataka kulipa kati ya Sh 8 milioni na Sh 10 milioni.

Hata hivyo, wameshagawana mali za ndani zilizokuwamo, kadiri ya hukumu. Mama amechukua vyombo vyote vya ndani, na baba amebaki na baiskeli na dumu la plastiki la ujazo wa lita 250.

Winifrida anaishi kwa dada yake wa ukoo, huko huko kijijini. Kuhusu sakata hili, hasa fumanizi, uhusiano wake na Tumbo, na hatima yake ya elimu, Winifrida anasema: “Alinitongoza, akanipeleka kwake… baada ya siku mbili, akanichukua tena kwa gari. Baada ya dakika kama dakika 15 hivi, nikiwa nimetoka chumbani kwake, kuingia kwenye gari, wazazi wangu wakafika na kutufumania. Wakati wanazozana naye, mimi nikafungua mlango, nikakimbia.

“Nasikia walimshitaki, lakini sikujua shauri liliishia wapi. Nilitorokea kwa rafiki yangu, nikajificha. Baadaye walinitoa kwa rafiki yangu na kunirudisha shuleni, lakini niliacha tena kwa sababu afisa tarafa aliendelea kunifuatilia. Misukosuko ilipozidi, nikakimbilia kwa bibi yangu anayeishi Ushirombo.

“Nilikaa kwake kwa miezi kama mitatu hivi, nikarudi nyumbani mwezi wa 12, na kipindi hicho wanafunzi wenzangu walikuwa wameshamaliza mtihani. Natamani nipate fursa ya kufanya mtihani, lakini sijui nifanyeje. Nipo tayari hata kurudia kidato cha pili.”

Daudi Edward, babu mdogo wa Winifrida, anaomba serikali kuu iingilie kati, kwani jitihada zao zimekuwa zinagonga mwamba, kwa kuwa serikali ngazi za chini imekuwa inamlinda mtuhumiwa.

“Ni kweli yalitokea, tukachukua hatua licha ya vitisho vya wakubwa wilayani, mambo yakanyamazishwa na DC (mkuu wa wilaya),” anasema.

Mwalimu Simon Mashauri, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Uyovu, anakiri kuwa Winifrida alikuwa mwanafunzi wake, na hakufanya mtihani wa taifa, na kwamba alitoroka shule, akarudishwa na wazazi, akatoroka tena, lakini shule haikuwahi kupokea taarifa rasmi kuhusu sababu za Winifrida kutofanya mtihani.

“Sina taarifa rasmi za kilichomtokea, mengine nayasikia mitaani, lakini siwezi kuyathibitisha,” anasema.

Hata hivyo, Wilfred Mtuga, mkuu wa shule msaidizi, ambaye ndiye alipokea taarifa hizo, anasema: “Taarifa zilipotufikia tulimuita, tukamhoji, akakataa kusema ukweli; kama shule tukamwadhibu, lakini hata adhabu yenyewe hakuimaliza. Alikaa kama wiki moja hivi, akatoroka tena. Inawezekana alijihisi vibaya kukaa pale maana suala lake lilikuwa limetapakaa kila sehemu kijijini, shuleni, kwa walimu na wanafunzi; nadhani alikuwa ameathirika kisaikolojia, akaamua kujificha. Hakufanya mtihani, ingawa alikuwa ameshasajiliwa kama mtahiniwa.”

Amani Mwenegoha, mkuu wa wilaya, hataki kulizungumzia. Anasema, “sijui jambo hilo, kamuulize wewe. Sijapata lalamiko lolote kutoka kwa mzazi.”

Mtuhumiwa mwenyewe, Tumbo, amekana tuhuma hizo, akisema,  “sijui lolote kuhusu suala hilo,” akakata simu.

Mathayo Paschal, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Buganza, Kata ya Uyovu, ambaye amekuwa akifuatilia suala hili ili haki itendeke, anasisitiza: “Viongozi wa wilaya wanajua vema sakata hili, kwa kuwa wamehusika tangu awali. Na tulipopokea barua ya Tumbo akitaka kufanya ziara ya vijiji vyetu, tulimgomea, tukasema hatuwezi kutembelewa na ofisa mwenye mwenendo usioridhisha kwenye jamii, hadi tutakapopata majibu ya hatua zilizochukuliwa dhidi yake.”

Barua iliyoandikwa na Tumbo, tarehe 22 Februari 2016, kwenda kwa watendaji wa vijiji na kata, ina kichwa cha habari: “Yah: Ziara ya afisa tarafa katika vijiji vyote kata ya Uyovu kuanzia tarehe 23/02/2016.”

Lengo la ziara hiyo ni “kuongea na wananchi kuhusu masula yafuatayo: zoezi zima la TASAF, ulinzi na usalama, kutoa elimu kwa wananchi juu ya nyaraka mbalimbali za serikali, kama vile afya, elimu na mazingira, na kukagua vikundi vya ulinzi na usalama, sungusungu kuanzia kitongoji.”

Kata ya Uyovu inaundwa na vijiji saba – Azimio, Ibamba, Uyovu, Kanembwa, Buganzu, Kabuhima na Lyobahika.

Barua hiyo imenakiliwa kwa mkuu wa wilaya, mkurugenzi mtendaji wa Bukombe, mkuu wa kituo cha polisi, Runzewe, na mtemi wa sungungu, Siloka.

Hata hivyo, ziara hiyo haikufanyika kwa sababu mwenyekiti wa kijiji cha Buganzu, alimwandikia barua mkuu wa wilaya ya Bukombe, tarehe 26 Februari 2016, ambayo pamoja na mambo mengine, inasema:

“Yapo masuala muhimu ya kuwekwa sawa na kurekebisha yahusuyo tabia na mwenendo wa utendaji kazi katika maisha yetu, miongoni mwetu viongozi ili kulinda heshima na kudumisha imani ya raia kwetu.

“Tunaona ni bora na tunashauri tukae viongozi pekee – vijiji, kata na tarafa – kupewa majibu juu ya kashfa ya (Tumbo) kujihusisha na mapenzi na mwanafunzi kiasi cha kumzuia kufanya mtihani wa kidato cha nne; utozaji wa faini kubwa bila risiti kwa kukiuka viwango na taratibu zilizowekwa na serikali kuu au halmashauri; unyanyasaji wa wenyeviti wa vijiji na vitongoji (kuwaweka ndani bila kosa na bila kesi) vinavyofanywa na afisa tarafa (Tumbo)…”

Barua hiyo imenakiliwa kwa mkurugenzi mtendaji wa Wilaya ya Bukombe, diwani wa Kata ya Uyovu, na Tumbo.

“Mkuu wa wilaya hawezi kusema hajui suala hili. Nilimkabidhi barua hii kwa mkono wangu, nikamsainisha kwa dispatch. Baadaye akatoa amri nikamatwe,” anasema Paschal.

Kutokana na mzozo huo, Tumbo alifungua shauri polisi, akiwataka wamkamate Paschal kwa kile alichoita “kukataa amri halali.”

Hata hivyo, mkuu wa polisi Bukombe, baada ya kufanya uchunguzi wa suala lenyewe, aliandika barua kwa mkuu wa wilaya, yenye kumbukumbu BKE/A.24/27/131, tarehe 12/ Machi 2016, yenye kichwa cha habari: “Yah: malalamiko ya Tumbo s/o John dhidi ya Mathayo s/o Paschal.”

Barua hiyo, iliyosainiwa na L.A Nyandahu-SP, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bukombe, inasomeka, “kimsingi, suala (hili) lilichunguzwa kupitia sheria mbalimbali kuweza kubaini kama kosa lililofanyika ni la jinai au ni la kinidhamu. Ofisi yangu imebaini kuwa kosa hili kwa ujumla ni la kinidhamu.

“Nashauri mkurugenzi mtendaji wa wilaya kupitia kwa mwanasheria wa halmashauri, afisa tarafa na mwenyekiti huyo wa kijiji waelimishwe misingi na mipaka ya majukumu ya kila mmoja ili kuweka nidhamu kazini na kuepusha migongano ya kimadaraka isiyo ya lazima.”
Murugwa, Afisa Tarafa wa Ushirombo, anajihami akisema, “sikutumwa na DC kusuluhisha. Nilisikia watu wanasema hivyo, lakini walinipakazia tu.”
Mama yake Winifrida hajapatikana kueleza anachojua kuhusu sakata hili. Mbali na mawasiliano ya maandishi kati yao na viongozi wa serikali kuhusu sakata hili, polisi nao hawakupatikana kujibu maswali ya nyongeza.

Kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya mwaka 1998, mtuhumiwa anapotiwa hatiani kwa kutembea na mwanafunzi, hata kama wamekubaliana, adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela. Iwapo msichana atakuwa na umri chini ya miaka 18, hukumu ni kifungo cha maisha jela.

error: Content is protected !!