July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ngome ya Shah Mafia yabomoka, kada wake ahamia Chadema

Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah

Spread the love

KADA maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mafia, Mohammed Makungu Suleiman amekihama chama hicho. Amehamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaandika Pendo Omary … (endelea).

“Nimeamua kwa hiari yangu kuondoka ndani ya chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema,” amesema Suleiman.

Suleiman, kada wa CCM tangu mwaka 1989 na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM ngazi ya tawi, leo ameikabithi rasmi Chadema kadi yake ya uanachama wa CCM na kukabidhiwa kadi mpya ya Chadema na Mabere Marando, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Tukio la kumkabidhi Suleiman kadi ya uanachama wa Chadema, limefanyika ndani ya ofisi za Chadema jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari na baadhi ya viongozi na wanachama wa chama hicho.

Suleiman alishika nafasi ya uwenyekiti huo kwa miaka 10 tangu mwaka 2004 katika tawi la Kilindoni Mjini, kata ya Kilindoni Mjini, wilaya ya Mafia, mkoa wa Pwani.

Akieleza sababu ya kuondoka CCM Suleiman amesema, “Kuondoka kwangu ndani ya chama hicho na kujiunga na Chadema, kumetokana na kuvutiwa na msimamo wa chama hiki katika kutetea wanyonge, kusimamia rasimali za taifa na kupigania ujio wa Katiba Mpya.”

Aidha, amesema amevutiwa na ziara za viongozi wakuu wa Chadema katika Kisiwa cha Mafia, akiwamo Mabere Marando, Tundu Lissu, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu na Halima Mdee.

“Katika ziara hizo ambazo zilikwenda pamoja na kuhutubia mikutano ya hadhara, viongozi hawa walibainisha mapungufu kadhaa yaliyopo ndani ya serikali na kuonyesha jinsi gani chama kilichoko madarakani hakiwezi kutatua matatizo hayo kwa kuwa ni sehemu ya kile kilichoelezwa,” Suleiman amefafanua.

Akitoa mfano wa mapungufu hayo amesema, “Viongozi hawa wameeleza jinsi mabilioni ya shilingi yalivyotumika kwa ujenzi wa gati, ambalo halitumiki kutokana na kukosa ubora. Badala ya kujenga gati, serikali imejenga daraja na kuliita gati.”

Pia, amesema viongozi hao walieleza jinsi serikali ilivyotoa fedha kwa ajili ya kulipa fidia kwa watu wanaokatiwa minazi yao kupitisha umeme, lakini fedha hizo zimetafanwa na wajanja wachache serikalini na kuacha wananchi wa Mafia kuwa masikini.

“Baada ya kutathimini hayo, dhamira yangu imenisuta kuendelea kuwa sehemu ya udhalimu huu dhidi ya wananchi wa Mafia….

“Hivyo basi, sasa nimedhamiria kwa dhati, kutumia nguvu zilezile, kukiondoa CCM madarakani kupitia Chadema na washirika wake katika UKAWA,” amesisitiza Suleiman.

error: Content is protected !!