January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ngeleja atumia mafanikio ya wizara kuomba urais

Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja akitangaza nia ya kuwania Urais kupitia CCM

Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja akitangaza nia ya kuwania Urais kupitia CCM

Spread the love

MBIO za kuomba uteuzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kuwania urais Oktoba mwaka huu, zinazidi kupamba moto, ambapo Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ametangaza nia huku akijivunia mafanikio makubwa aliyoyafanya katika sekta hiyo ya nishati na madini. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Ngeleja ambaye pia ni mbunge wa Sengerema, anakuwa waziri wa pili wa zamani katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kutaka apimwe kwenye mbio hizo kwa mafanikio yaliyopatikana katika wizara hiyo ambapo kila mmoja akitamba kuwa ndiye alifanya hayo. Prof. Sospeter Muhongo aliyejiuzulu kwa kashafa ya Escrow ndiye alikuwa wa kwanza kujivunia hilo.

Akiwahutubia wafuasi wake katika ukumbi wa Benki Kuu jijini Mwanza leo, Ngeleja amesema Rais wa awamu ya tano anapaswa kuja na mbinu na mipango ya kuchukia rushwa na umasikini.

Amesema umefika wakati wa kumpata rais ambaye ana hofu ya mwenye Mungu ambaye anaguswa na vitendo vya rushwa pamoja na kusimamia sheria ipasavyo.

Ngeleja amesema endapo atapa nafasi ya kuwa Rais wa Tanzania atahakikisha anapambana na vitendo vya rushwa pamoja na kuinua uchumi.

Ngeleja amesema kabla ya mwaka 2025, Tanzania inapaswa kuingia katika uchumi wa kati, hivyo inahitaji mipango madhubuti ya kuifikisha katika hatua hiyo.

Vipaumbele

Ngeleja alivitaja vipaumbele vyake vinne ambavyo ataingia navyo Ikulu endapo atapa nafasi hiyo kuwa ni pamoja na kuinua uchumi, huduma za jamii, miundombinu ya barabara na utawala bora.

Utawala bora

Amesema atahakikisha serikali inaendesha shughuli zake kwa uwazi katika mambo ambayo hayaitaji usiri na kusimamia uwajibikaji na nidhamu serikali.

Ngeleja amesema endapo atapata nafasi ya kuwa rais atahakikisha anaimarisha mshikamano na taifa kwa kuimarisha Muungano.

 Huduma za jamii

Ngeleja amefafanua kuwa, jukumu lake la kwanza la serikali yake ya awamu ya tano atakayoiongoza ni kuhakikisha anasimamia na kumaliza ubovu wa miundombinu na kuiweka katika ubora.

Alidai kuwa atahakikisha huduma ya maji inaboreshwa na kuwafikishia huduma ya maji katika kila pembe ya taifa ili kufikia malengo ya serikali nyingine zilizotangulia. 

Uchumi

Ngeleja amesema katika awamu yake ya tano atahakikisha anasimamia uvuvi na kilimo kwani asilimia 70 ya Watanzania walio wengi wanategemea kilimo, hivyo atahakikisha anakiboresha.

“Nitahakikisha tunaimarisha kilimo kwa kushirikiana na viongozi wenzangu kwa kuwatafutia wakulima na nyenzo za kufanyia kazi kutoka kulima kwa kutumia mikono kwenda katika kilimo cha kisasa,”amesema.

Kwa mujibu wa Ngeleja, ili kukuza uchumi wa taifa inapaswa kuhakikisha serikali inawekeza zaidi kwa wafugaji, wakulima na wavuvi, jambo ambalo litafanikisha Watanzania kuendelea.

Utetezi kashfa ya Escrow

Ngeleja alipata wakati mgumu kufafanua tuhuma dhidi yake za kunufaika na mgawo wa Sh. 40 milioni kutoka kwa mmoja wa wamiliki wa kampuni ya IPTL, James Rugemalira zilizokwapuliwa katika Benki Kuu ya Tanzania.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Ngeleja kumaliza kuhutubia na hivyo kuruhusu maswali ya waandishi wa habari ambapo, muuliza swali, alimtaka mtangaza nia aeleze anajitengeje na ufisadi wakati yeye ni mtuhumiwa wa ufisadi.

Ngeleja huku akionesha kupoteza umakini, alitumia muda mrefu kujitetea kwa kutumia kauli ya Rais Kikwete alipozungumzia suala hilo na akisema fedha hizo hazikuwa za umma bali watu binafsi.

“Kashfa ya Richmond hainihusu wala sikutajwa licha ya kupangiliwa kwa  Baraza la Mawazi na kuundwa upya na Rais Kikwete. Katika kashfa ya Escrow, Rai Jakaya Kikwete, wakati anazungumza na wazee wa Dar es Salaam, Desemba mwaka jana alinisafisha,”alijitetea.

Ngeleja amesema kutokana na tuhuma hizo kutokuwa za kweli ndo maana Rais Kikwete, alimsafisha kutokuhusika na uchotwaji wa fedha hizo.

“Kama kuna mtu ana ushahidi wa kutosha ajitokeze mbele ya umma kwamba mimi nahusika katika wizi huo na ndo maana hata rais alilizungumzia suala hilo,”amesema Ngeleja.

error: Content is protected !!