June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Ngara kuzalisha KW 900 za umeme

Mitambo ya Umeme

Spread the love

WIZARA ya Nishati na Madini, imesema ukaratabati wa mitambo ya umeme Wilaya ya Ngara, ukikamilika itakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa KW 900 ambapo kwa sasa inazalisha KW 800. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage alieleza hayo bungeni leo wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Ngara, Deogratias Ntukamazina (CCM).

Mbunge huyo alitaka kujua kama mitambo hiyo itafanyiwa matengenezo ili kuondoa adha ya kukatikakatika kwa umeme kwa wananchi wa wake.

Katika swali lake la nyongeza alitaka kujua ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi wa Orio Holland kwa kufungua jenereta kubwa mbili ili kuwepo kwa umeme wa uhakika kabla ya umeme wa Rusumo.

Akijibu maswali hayo, Mwijage amesema matengenezo hayo yatagharimu Euro 527,990 sawa na Sh. milioni 215.87 ambapo matarajio ni kuhakikisha umeme unakuwepo wa uhakika.

Amesema pamoja na jitihada hizo, pia Serikali inaendelea na mchakato wa kusambaza umeme vijijini kupitia Mfuko wa Umeme Vijijini (Rea) ambao utachangia kuwepo kwa hitaji la KW 300 za umeme ili kukidhi hitaji la wahitaji wote.

Kwa mujibu wa Mwijage, serikali imeanza mchakato wa kufunga mtambo mwingine wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa KW 650 ambapo ongezeko hilo litafikisha uwepo wa umeme wa KW 1550, hivyo kumaliza tatizo la umeme Ngara ambapo gharama za mtambo huo utagharimu Sh. milioni 370.

Amesema mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wapo wilayani Ngara kukarabati mitambo ya kuzalisha umeme ambapo hadi mwishoni mwa Juni mtambo namba moja utakuwa umekamilika na mtambo namba mbili utaanza kukarabatiwa mapema.

Kuhusu Mradi wa Orio Holland, amesema utekelezaji utaanza baada ya kukamilika kwa taratibu zikiendana na ufunguzi wa ‘Letter of Credit’ ambapo mradi huo utakaokuwa katika vituo vipya utaweza kuzalisha MW 2.5 katika Miji ya Ngara, Biharamulo na Mpanda.

Mwijage ameongeza kuwa, mradi huo utajumuisha ukarabati na upanuzi wa mfumo wa usambazaji umeme na gharamaa za mradi ni Euro 32.76 kwa ufadhili wa Serikali ya Uholanzi na Serikali ya Tanzania itachangia asilimia 50 ya gharama.

error: Content is protected !!