December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Netanyahu azidiwa mbinu, apiga yowe

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel

Spread the love

USHAWISHI wa Vyama vya Upinzani nchini Israel, umefanikiwa kumpandisha kizimbani Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa taifa hilo kwa tuhuma za ufisadi, udanganyifu na matumizi mabaya ya madaraka. Inaripoti mitandao ya kimataifa…(endelea).

Netanyahu anadaiwa kupokea rushwa katika mfululizo wa kesi.

Anashutumiwa kukubali zawadi za bei ghali kutoka kwa marafiki matajiri, kutoa ‘posho’ kwa vyombo vya habari vinavyoandika taarifa njema kwake na kwa familia yake, pia anadaiwa kupindisha sheria na kutumia ushawishi wake kwa kampuni moja ya simu kupewa mamilioni ya Dola za Marekani kinyume na utaratibu.

Jumapili ya mwisho wa wiki, Netanyahu amefungua historia mpya kwa taifa hilo kwa kiongozi aliye madarakani (waziri mkuu), kupandishwa mahakamani. Kesi yake inasikilizwa mjini Jerusalem, Quds.

Kiongozi huo wa chama cha Likud, amekuwa akishambuliwa na waandamanaji huku wakimwita kwa majina ya fedheha sambamba na kiongozi mlafi, fisadi jambo lililozidisha presha ya kufikishwa mahamani kujibu tuhuma hizo.

Netanyahu anaelekeza malalamiko yake kwa Avichai Mandelblit, Mshauri wa Vyombo vya Mahakama vya Utawala wa Israel, kwamba anashirikiana na watu wengine kwa lengo la kumuondoa madarakani.

Yair Lapid, kiongozi wa upinzani katika Bunge la Knesset amesema, sambamba na kukosoa vikali matamshi ya uchochezi ya Netanyahu, kiongozi huyo anafanya njama za kuibua vita vya ndani huko Israel.

Lapid ambaye ni kiongozi wa chama cha Yesh Atid amesema, matamshi hayo ya Netanyahu ya kuwatuhumu wengine ni kuwachochea polisi, mwendesha mashtaka mkuu, mahakama na hata vyombo vya habari, kinyume na utawala wa sheria.

Amesisitiza, Netanyahu hastahili kuendelea kubakia kwenye nafasi yake ya uongozi.

Ehud Olmert, waziri mkuu wa zamani wa utawala huo sambamba na kumkosoa vikali Netanyahu, amemtuhumu kwa ubinafsi na kutanguliza mbele maslahi yake ndani ya utawala huo.

Tangu Novemba 2018, utawala wa Netanyahu unatikiswa na mkwamo mkubwa wa kisiasa. Novemba 2018, Avigdor Lieberman na chama chake cha Yisrael Beiteinu walijitoa kwenye serikali ya Netanyahu na kulazimisha kuitishwa uchaguzi kabla ya wakati wake.

Uchaguzi huo uliitishwa tarehe 9 Aprili 2019, lakini Netanyahu alishindwa kuunda serikali katika kipindi cha siku 42 alizopewa. Juzi, Netanyahu alifanikiwa kuunda serikali yake kwa kushirikiana na mkuu wa chama cha Buluu na Nyeupe, Benny Gantz.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya wawili hao, Benjamin Netanyahu atakuwa Waziri Mkuu wa Israel kwa muda wa mwaka mmoja na nusu, baada ya hapo Gantz atashika wadhifa huo kwa muda kama huo.

Kuna wasiwasi mkubwa kwamba Netanyahu atavunja serikali kabla ya kufikia muda wa Gantz kuingia madarakani.

Bunge la Israel limelazimika kutunga sheria mpya kumzuia Netanyahu kusaliti makubaliano ya kuondoka madarakani baada ya miezi 18 na kisha kumpisha Gantz amalizie miezi 18 baada ya uchaguzi ulioisha kwenda sawa.

error: Content is protected !!