May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NEC yaahirisha uchaguzi Muhambwe, yasitisha kampeni

Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk. Wilson Mahera

Spread the love

 

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania, imetangaza kuufuta uchaguzi mdogo wa ubunge wa Muhambwe, mkoani Kigoma uliokuwa ufanyike 2 Mei sasa utakuwa 16 Mei 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Uteuzi wa wagombea katika uchaguzi huo ulikwisha fanyika na baadhi ya vyama kikiwemo ACT-Wazalendo, mgombea wake, Julius Masabo, amekwisha zindua kampeni hizo.

Taarifa kwa umma, iliyotolewa leo Ijumaa tarehe 9 Aprili 2021, na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk. Wilson Mahera imesema, kwa mujibu wa kifungu cha 46(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, NEC ina mamlaka ya kufuta siku ya uchaguzi iliyopangwa awali na kupanga siku nyingine.

Dk. Mahera amesema, kwa msingi huo, tume kwa mamlaka iliyopewa “Tume imefuta siku ya kupiga kura katika jimbo la Muhambwe iliyokuwa imepangwa kufanyika 2 Mei 2021 na upigaji kura sasa utafanyika 16 Mei 2021.”

Amesema, kampeni za ubunge katika jimbo hilo, zinasitishwa na zitaanza tena tarehe 1 hadi 15 Mei 2021.

Mabadiliko ya ratiba hiyo, sasa kampeni za uchaguzi zitakuwa kwa siku 15 pekee tofauti na ratiba ya awali iliyokuwa mwezi mmoja kuanzia 3 Aprili hadi 1 Mei 2021.

Uchaguzi huo wa Muhambwe, unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wake, Atashasta Nditiye kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufariki dunia tarehe 12 Februari 2021, kwa ajali ya gari iliyotokea jijini Dodoma.

Hii ina maana kuwa, uchaguzi huo wa Muhambwe, utafanyika siku moja na ule wa Buhigwe nalo la Kigoma.

Uchaguzi wa Buhigwe, utafanyima kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Philip Mpango wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyeteuliwa kisha kuapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

error: Content is protected !!