March 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

NEC watangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Liwale

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage

Spread the love

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa Jimbo la Liwale Mkoa wa Lindi, kufutia kujiuzulu kwa Zuberi  Kuchauka aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kupitia CUF. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage,  Mwenyekiti wa NEC,  wakati akitangaza uchaguzi huo leo tarehe  25 Agosti, 2018 Jijini Dar es Salaam, amesema tangazo la uchaguzi linakuja baada ya Tume kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, ameitaarifu Tume kuwepo kwa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Liwale Mkoa wa Lindi, kuanzia tarehe 13 Agosti, 2018, kufuatia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Ndugu Zuberi Mohamed kujiuzulu uanachama wa Chama cha Wananchi – CUF, na hivyo kupoteza sifa ya kuwa Mbunge,” amesema.

 “…kwa mujibu wa vifungu vya 37 (1) (b),(5) na 46 (2) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Tume inatoa taarifa kwa Umma kuwa Jimbo la Liwale lipo wazi.”

Jaji Kaijage amesema fomu za uteuzi kwa wagombea zitaanza kutolewa kuanzia tarehe 07 hadi 13 Septemba mwaka huu, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 13 Septemba mwaka huu, kampeni za uchaguzi zitaanza tarehe 14 Septemba na kumalizika tarehe 12 Oktoba mwaka huu na siku ya uchaguzi itakuwa tarehe 13 Oktoba mwaka huu.

“Tume inavikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, miongozo, na maelekezo yote wakati wa kipindi cha uchaguzi huo mdogo,” Jaji Kaijage amesema.

error: Content is protected !!