January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NEC msipuuze malalamiko haya, yapate majibu ya kina

Spread the love

ZIKIWA zimebaki siku chache kuingia katika jambo ambalo linasubiriwa watanzania wengi na mataifa ya nje la kupiga kura katika uchaguzi mkuu kumeibuka malalamiko mbalimbali. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Malalamiko mengi yanaelekezwa zaidi katika Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) kwa kutiliwa shaka kwamba kuna mipango ya kuwahujumu wagombea wanaotokana na vyama vinavyounda Ukawa.

Malalaniko haya ni ya msingi sana kuyasikiliza na kuyatolea majibu ya kina zaidi ili kuondoa sintofahamu ambazo watanzania hasa wapiga kura wanaghubikwa nazo.

Hivi karibuni Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinachoungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa), Juma Duni Haji, ameitaka NEC kuruhusu umoja huo kufanya uhakiki wa vituo vya kupigia kura baada ya kubaini uwepo wa takriban vituo 20,000 hewa vya kupigia kura.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Mgombea huyo bila kutafuna maneno alisema Ukawa wamebaini uwepo wa mbinu chafu ya kuongeza vituo hivyo ili Chama cha Mapinduzi (CCM) kiweze kupata ushindi wa goli la mkono.

Kutokana na hali hiyo ya kuwepo kwa wasiwasi wa njama za CCM kushinda kwa goli la mkono kana viongozi wao wanavyojinadi Duni aliwaagiza wagombea wa majimbo na kata nchini kuhakiki vituo vya kupigia kura katika maeneo yao ili kujiridhisha na kubaini kama vituo hivyo ni halali.

Alisema kilichowashtua Ukawa ni takwimu za upotoshaji zilizotolewa na NEC ambazo zinaonesha kuwa watanzania watakaopiga kura ni milioni 23.7, katika vituo vya kupigia kura ni 72,000 na kila kituo kitakuwa na watu wasiopunguza 450.

Mgombea huyo alisema katika hesabu ambazo wamezipitia kutokana na idadi ya wapiga kura vilitakiwa viwepo vituo takriban 53,000 na si vituo 72,000 ambavyo tume imeeleza.

“Kwa hesabu hii basi ukichukua idadi ya wapigakura hao milioni 23.7 ukagawanya na watu 450 ambao wanatakiwa kuwepo kwenye kila kituo, utaona vituo vilipaswa viwe vituo 53,000.

“Hizi ni njama za goli la mkono, unaweza kudanganya vyovyote lakini namba ukitaka kuidanganya haikubali,” alisema Haji.

Haji alibainisha kwa vituo 72,000 kulitakiwa kuwe na wapiga kura milioni 32.4 ambapo katika sensa ya 2012 Watanzania walikuwa milioni 44.92 na kwasasa inakadiriwa kuwa watu milioni 48 haiwezekani watu milioni 32 wakapiga kura.

“Hapa unaona kabisa watu milioni tisa hawapo hapo ndiyo goli la mkono, wakati Lowassa anaanza na kura sifuri, Magufuli anaanza na kura milioni 9 hilo ndiyo goli lenyewe, tunataka tume waturuhusu tufanye uhakiki tujiridhishe ili tuende kwenye uchaguzi,” alisema Mgombea huyo.

Hata hivyo alisema umoja huo umeshtukia mchezo huo na hautakubali mchezo huo ujirudie tena, kwani mwaka 2010 walijiandikisha milioni 20 lakini waliopiga kura ni milioni 8.6 ambapo Rais Jakaya Kikwete alishinda kwa kura milioni 5.7 sawa na 61.7, na kudai haiwezekani watu milioni 12 wawe hawakupiga kura halafu Kikwete akapewa ushindi wa zaidi ya asilimia 50 ambapo hajafikia idadi ya wapigakura kura waliojiandikisha.

Alisema hizo ni vurugu na ubabe ambao unafanywa na serikali yenye madaraka kwa kutumia nguvu nyingi na vyombo vyao walivyonavyo ili kufikia lengo la ushindi wa goli la mkono.

“Ni vyema Jaji Lubuva akae na sisi atueleze kwanini iwepo namba hii, na wagombea wetu nawaagiza hususan wa upinzani mkafanye uchambuzi wa vituo 72000, maana isije ikawa mkono wa kushoto unapewa halafu wa kulia unaminywa,” alisema Mgombea huyo.

Alisema wasilazimishe mambo bali wawasilikilize wananchi wanataka nini, kwani kuna mataifa mbalimbali yametokea machafuko kutokana na wananchi kuchoshwa na uongozi unaowaumiza.

Aidha alisema Ukawa watakuwa tayari kuueleza umma ambacho tume itakuwa haijakieleza kwani wao ni mawakala wa wananchi.

Jambo lingine ambalo Duni alionekana kulipigia kelele ni kitendo cha serikali kulazimisha kufungwa kwa vyuo vya elimu ya juu na elimu ya kati.

Alisema inasikitisha kuona wazi kuwa kila mtu alihamasishwa kujiandikishia katika kituo chake lakini mwisho wa siku unamnyima haki ya kupiga kura.

Alisema hakuma mtu ambaye anaweza kujitengenezea kitambulisho na kama yupo ni rahisi kumbaini sasa kwanini mtu azuiliwe kupiga kura wakati amejiandikisha na ni raia wa Tanzania.

Hilo kama halitoshi hata Naibu katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika ameonekana kuilalamikia tume juu ya kile kinachodaiwa kuwa ni mizengwe ya kuitafutia CCM ushindi.

Mnyika naye anaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kujibu hoja zinazoibuliwa kuhusiana na Uchaguzi Mkuu ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba 25 na sio kupotosha kwa makusudi huku ikiacha hoja za msingi zinazotolewa zikielea.

Mnyika alisema kuna njama za kuendelea kuchelewesha daftari la wapiga kura kwa vyama vya siasa.

“Hatuwezi kuiacha Tume iendelee kufanya ucheleweshaji wa kutoa orodha ya wapiga kura nchi nzima kwa vyama ili wataalamu wetu wa teknolojia ya kompyuta wayahakiki, siku zimeshabaki chache na tukumbuke mwaka jana muda kama huu vyama tulikuwa tumeshapewa ‘soft copy’ ya daftari na kulifanyia uhakiki,” alisema Mnyika.

Mnyika anaenda mbali zaidi kwa kuitaka NEC kutoa orodha ya wapiga kura wote ili kuondoa sintofahamu inayoweza kujitokeza kutokana na daftari hilo kucheleweshwa kwa vyama vinavyohitaji kuwapatia nakala ya daftari hilo mawakala wao nchi nzima.

Katika hatua nyingine Mnyika ameiasa NEC kuacha upotoshaji, kwa kusema busara ya wasimamizi wa uchaguzi inaweza kutumika kuwaruhusu watu wenye vitambulisho vya kupiga kura watapiga kura hata kama wasipokuwepo katika orodha ya wapiga kura, huo ni upotoshaji mkubwa.

Kutokana na hali hiyo ya sintofahamu katika masuala mazima ya kuwepo kwa takwimu za upotoshaji au la, kufungwa kwa vyuo na kutompigia kura mtu kiongozi yoyote kama hauko katika kituo chako ni vyema yakawekwa wazi ili watu watambue.

Jambo lingine na la msingi ni bora Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikaweka wazi ni sababu gani ambazo zinamfanya mtanzania mwenye kadi ya kupigia kura asipate fursa ya kupiga kura wakati ana kitambulisho harari.

Pia ni vyema watanzania kwa utulivu kabisa wakahoji ni kwanini wasipige kura hata ya rais wakiwa nje ya vituo vyao na kupiga kura ukiwa nje ya kituo chako kunaathiri nini?

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0757213673, email: dansonkaijage3@gmail.com.

error: Content is protected !!