January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

NEC kugawa upya majimbo ya uchaguzi

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania, Jaji Damian Lubuva

Spread the love

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imepanga kuyagawa upya majimbo ya uchaguzi nchini. Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva amesema, tume yake tayari imekamilisha ugawaji majimbo hayo na muda wowote itaanza mchakato wa kuyagawa. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jaji Lubuva amesema, tume yake imeamua kugawa majimbo hayo kwa kuzingatia vigezo mbalimbali, ikiwamo idadi ya watu, upatikana wa mawasiliano, hali ya kijiografia na alichoita, “kanuni za uchaguzi wa Rais na wabunge ya mwaka 2010.”

Aidha, Jaji Lubuva amesema, Tume itayagawa majimbo hayo kwa kuzingatia uwepo wa miundo mbinu bora, hali ya kiuchumi kwa kuweka uwiano kati ya eneo moja na jingine, simu na vyombo vya habari kwa ajili ya kupata mwakilishi atakae harakisha maendeleo katika eneo husika.

NEC inatangaza majimbo mapya ya uchaguzi, huku uandikishaji wa wananchi katika daftari la kudumu la wapigakura, ukiwa umedolola.

Amedai kuwa kuna baadhi ya majimbo ni makubwa kulinganisha na majimbo mengine, jambo ambalo linatokana na ongezeko la watu nchini.

“…zoezi hili linatakiwa kufanyika mara kwa mara au angalau mara moja baada ya miaka 10. Ugawaji wa majimbo ulifanyika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, na kwa kuwa sasa tunaelekea katika uchaguzi mwingine, lazma tufanye hivyo,” ameeleza Jaji Lubuva.

Amesema utaratibu utakaotumika katika ugawaji wa majimbo hayo na kubadilisha mipaka, ni kuwasilisha maombi ya kufanya hivyo, yawasilishwe kwa Mkurugenzi wa Halmashauri, kwenda kwa katibu tawala, katibu tawala za mikoa,  kisha kwenda NEC.

Hata hivyo, mara baada ya kuwasilishwa maelezo hayo, baadhi ya wajumbe kutoka vyama vya upinzani wadai kuwa ugawaji huo wa majimbo unafanyika kwa shinikizo la Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Tume imezidiwa na majukumu; wanataka kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, huku muda ukiwa haupo,” alisema Prof. Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF).

Alihoji, “walikuwa wapi siku zote, wakati muda uliobaki hautoshi?”

MwanaHALISI Online lilipomuuliza, Dk. Emmanuel Makaidi, mwenyekiti wa chama cha National League Democrat (NLD) amesema, “NEC inafanya kazi za CCM.”

 Akiongea kwa uchungu, Dk. Makaidi amesema, “Hii ni tume inapangiwa kazi na serikali, siyo kujipangia. Ni tume mbovu kuliko ile ya Jaji Luis Makame.”

error: Content is protected !!