October 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

NEC: BVR ni tatizo

Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), Dr. Sisti Cariah

Spread the love

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imekiri kuwepo kasoro katika mashine za kielektroniki (BVR), zinazotumika kuandikisha wapiga kura katika daftari la kudumu, kutokana na kugoma mara kwa mara hasa sehemu zenye vumbi sana. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Matatizo hayo yamejitokeza katika mikoa ya Tabora, Singida, Kagera, Dodoma ambako uandikisha huo unaendelea. Pia hata kule ambako NEC imekamilisha uandikishaji, wananchi wamekuwa wakipata usumbufu wa kushinda vituoni kujiandikisha bila mafanikio.

Pamoja na kukiri udhaifu huo, NEC bado imeendelea kujipa moyo na kusisitiza kwamba upigaji kura Oktoba 25 mwaka huu, upo palepale.

Akizungumza na waandishi leo ofisini kwake, jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi NEC, Dk. Sisti Cariah amesema, kwa kawaida mashine hizo, hutakiwa kusafishwa kila baada ya kuandikisha watu 400.

Na kwamba, mashine hizo husumbua sana mikoa ambayo inavumbi sana, “Wakati  mwingine zinagoma kwa muda mrefu na kusababisha foleni kubwa na kupelekea baadhi ya watu kulala nje ya kituo”

Mbali na hilo, Cariah amesema, uandikishaji unaendelea vizuri kwa baadhi ya mikoa na limefikia takribani asilimia 50 kwa maana ya idadi ya mikoa iliyofikiwa.

Hata hivyo, amesema NEC imelazimika kuahirisha kwa siku kadhaa uandikishaji kwa baadhi ya mikoa kutokana na mabadiliko ambayo yanaendelea kufanywa ya mipaka ya kiutawala ya Kata, Vijiji na Vitongoji.

Mikoa hiyo ambayo ilitakiwa kuanza leo ni pamoja na Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Mara, ambapo imesogezwa mbele hadi Juni 16 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Cariah, NEC imeshapokea BVR zote 8000, pamoja na vifaa vingine vyote na hivyo hadi kufikia Julai uandikishaji utamalizika.

Aidha amesema, kwa upande wa Dar  es Salaam na Pwani, uandikishaji huo utaanza Julai 2 mwaka huu, ambapo BVR zaidi ya 3000 zitatumika kufanya kazi hiyo.

“Kwa kuwa Dar inawatu wengi, ndio maana tumeufanya kuwa ya mwisho, ambapo tuna uhakika mashine hazitasumbua tena, maana na mafundi wote watakuwepo kuhakiksha kazi hiyo inaendelea vizuri na kwa muda mfupi” amesema Cariah.

“Nitoe wito kwa wale wananchi wanaojitokeza kujiandikisha mara mbili, waache mara moja kwani ni lazima tutawakamata, hivyo wanajitia hatiani bila sababu ya msingi na sheria itachukua mkondo wake,” amesema.

error: Content is protected !!